Original poster -
Mtambuzi | May 14, 2012
BADILI: Unapojikuta kwenye hali usiyoipenda, unaweza kufanya
jitihada za kuibadili au kubadili mtazamo wako kuhusu hali hiyo. Ikiwa
uko katika uhusiano unaodhani haukusaidii kwa mfano, unaweza kwenda kwa
washauri nasaha, unaweza kuzungumza na mwenzi wako na kujaribu kuufanya
uhusiano huo uwe bora zaidi ama waweza kubadili mtazamo wako wa namna
uhusiano wenye faida unavyotakiwa kuwa.
Mara nyingi huu ni uchaguzi mgumu sana kuufanya kwa sababu inaweza
ikalazimu kumkabili mtu mwingine kutoka katika tabia isiyo na faida
kwako. Kubadilika kunatuondoa kwenye nafasi yetu tuliyoizoea na ambayo
tunaiona inatufariji na kunahitaji ujasiri mkubwa kufanya hivyo.
Kuamua kuacha kumtegemea mpenzi kukupa furaha na kutafuta furaha kutoka
vyanzo vyenye kuaminika zaidi siyo jambo rahisi, lakini ni muhimu.
JIONDOE: Kama umeshindwa kubadili hali kwa sababu yoyote ile
umeshindwa kumfanya mtu abadili tabia yake kwa mfano, ni bora kujiondoa,
ondoka kabisa. Kujiondoa kunakufanya uondokane na hali isiyofurahisha
na kunasafisha njia kwako kwa ajili ya kuchagua jambo jingine mbadala.
Ni wazi,watu wengi hukimbilia kuchagua njia hii, hukimbilia kujiondoa
kwa sababu huogopa sana kujaribu njia ya kwanza ya kubadili hali ama
kubadilika wao wenyewe.
Lakini ingawa kukimbilia hatua hii bila kujaribu ya kwanza si busara,
kuna wakati ambapo kujiondoa ni hatua pekee ifaayo kuchukua. Hata hii
nayo inahitaji ujasiri mkubwa kwa sababu, mara nyingi akili zetu
hutuweka katika nafasi ya kutumia methali ya Zimwi likujualo kama
utetezi wa kuendelea kuvumilia madhila yasiyo muhimu tunayokumbana nayo.
KUBALI: hatua ya mwisho unayoweza kuchukua kukubali. Ziko hali
ambazo huwezi kuzibadili na kukwepa ukweli wa jambo hilo, ni sawa na
wendawazimu. Hebu mfikirie mfungwa wa kisiasa kama ilivyokuwa kwa mzee
Nelson Mandela wa Afrika Kusini na wenzake. Wakati alipokuwa
akishikiliwa jela, asingeweza kuibadili hali ile, wala asingeweza kuamua
kuondoka. Hakuna jingine aliloweza kufanya ila kukubali hali halisi na
kufanya kila analoweza kuishi katika hali hiyo. Kuna wakati kukubali
linakuwa ni chaguo la kwanza tunalopaswa kuelekeza macho yetu, wakati
tukiwa tunafikiria njia bora ya kubadili hali au kujiondoa.
Nina hakika kila mtu anapotazama mambo yanayozunguka maisha yake,
atakutana na moja ambalo haridhishwi nalo kwa asilimia 100. Utafanya
nini kushughulikia hilo, utajaribu kubadili hali au mtazamo wako wa
hali? Uko tayari kujiondoa ikiwa una hakika huwezi kubadili hali au uko
tayari kubadili mtazamo wako kuhusu jambo hilo ili uweze kuendelea nalo?
Uko tayari kukubali kile ambacho huna uwezo wa kukibadili na wala
huwezi kujiondoa?
Nafasi ni yako kutumia busara zako kuchagua.