Baba Askofu Stephen Munga: Acheni kucheza karata ya Udini, hoja ijibiwe kwa hoja

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,492
54,895
ACHENI KUCHEZA KARATA YA UDINI - HOJA IJIBIWE KWA HOJA

FB_IMG_1692602346700.jpg
Suala la mjadala wa mkataba tata wa bandari sio mchezo wa kamari. Hapo hatufanyi majaribio katika kuhoji na kujibu hoja. Pia hapo tunatazama mambo mapana ya taifa kwa vizazi vingi vijavyo. WATU WENYE AKILI TIMAMU NA NGUVU YA KUFIKIRI HUPAMBANA KWA HOJA. WALIO DHAIFU WA AKILI NDIO HUTUMIA MUSULI NA MIKUKI NA BUNDUKI NA MAHABUSU KUDHIBITI WENYE NGUVU YA HOJA.

Tukumbuke hoja za awali kuanzia maamuzi ya bunge kukubali mkataba huu tulitembea katika barabara mbovu. Kumbukeni wazungumzaji wa awali wakiwemo maprofesa Shivji na Tibaijuka; wakifuatiliwa na jamii ya wanasheria na baadae sehemu ya wenye nchi (wananchi). Tulidhani serikali na bunge wagejibu hoja zile kwa ufasaha na urahisi kumbe sivyo. Pia tulidhani itakuwa safari ya ndugu watembeao katika njia moja ili kufikia mwisho mmoja kumbe sivyo. Kabla safari haijafika mwisho tumegeukana na kuitana wahaini na kutiana minyororo. Sasa limetoka tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki lililojipambanua kwamba ni sauti ya watu na hivyo ni sauti ya Mungu. Tungali tunasikilizia.

Jambo lingine la kufadhaisha kabisa ni pale tunaposikia watu wengine wakifanya mjadala wa mkataba tata wa bandari kama mchezo wa karata katika kamari. Katika mchezo huo wanashusha karata ya udini. Wanawaona wanaohoji, na kipekee tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki kama mchezo wa kamari ya udini. Hizi ni fikra dhaifu na finyu. Tunapenda kuweka wazi kwamba wapo Watanzania ambao watatetea maslahi ya taifa hili na kamwe hawatakubali kudhoofishwa kwa dhihaka au kuchafuliwa kwa namna yeyote. Penye hoja tujibu kwa hoja. Shutuma sio hoja.

Ni hivi: Tunaongelea maslahi ya taifa. Tunaongelea mambo mazito ya uzalendo (patriotism). Hatufanyi sensa ya wakristo na makanisa au waislamu na misikiti. Ninaposimamia mambo ya imani yangu kwa Mungu najua kwamba hayo ni kwangu na wale ninaoshiriki nao imani moja. Katika mkataba wa bandari tunaongelea juu ya heshima na enzi kuu (sovereignty) ya taifa kuu la Tanzania. Katika heshima na enzi kuu ya taifa hili Mungu alilotupa hakuna aliye juu ya katiba na sheria za nchi hii tulizojiwekea. Kwa mtazamo huo, tunapozungumzia juu ya maslahi ya nchi sisi sote tunakalia vigoda vinavyolingana. Ni pale tu mfumo wa utawala unapokuwa kandamizi ndipo uwiano huo wa ushiriki katika kuzungumzia maslahi na heshima ya taifa huvurugika. Kucheza karata ya udini katika mambo mapana ya maslahi ya taifa ni sawa kutaka paka avute mkokoteni uliobeba tembo.

Tukumbushane kwamba katika hoja za wale wanaoona mapungufu katika mkataba tata hakuna anayekataa uwekezaji. Tena ieleweke kwamba sio suala la kuikataa serikali au kumkataa Rais. Nionavyo mimi wanaosaidia serikali na Rais ni wale wanaohoji mambo kwa wazi na kwa nia njema. Maadui wakubwa wa serikali na Rais ni wale wanafiki wanaosema kuna giza kumbe kuna nuru; na kwamba kuna nuru wakati kuna giza. Hili ni jambo la kulinda mambo ya msingi (matters of principle) ili taifa libaki kuwa taifa.

Hoja za msingi ni kwamba tunakubali uwekezaji kwa manufaa mapana ya taifa. Lakini pia kwamba ziwepo juhudi za makusudi za kuwajengea uwezo na nidhamu ya kiwango cha juu wawekezaji wazalendo. Lazima hawa wasaidiwe kufikia kiwango cha kuwa na sifa za ushindani za viwango vya kimataifa. Njia sahihi ya kukabili tatizo sugu la ukosefu wa ajira kwa vijana ni kujengea uwezo na nidhamu taasisi za ndani ili ziwe vitovu vya kukua kwa uchumi na kutengeneza fursa za uhakika za ajira. Kucheza karata ya udini katika fikra pana za maslahi mapana ya kijamii ni kuleta kasumba mbaya. Kama dini yako haikupanui upeo wa kufikiri kwako na kuona maslahi mapana ya jamii basi dini yako haitusaidii. Usipoifuga dini yako vizuri yaweza kuwa sumu kwa maendeleo ya jamii.

Pia, Soma
 
Hao ni wakutazama tu, wacha waruke ruke na hao mashekhe wao na story zao za kutunga vile wapendavyo, muhimu wakimaliza maigizo yao, wajue tu, bado tunataka ule mkataba wa hovyo wa bandari uvunjwe.

Kauli ya kusema "tusichanganye dini na siasa" ni kauli ya kitapeli, na ya kijanja, yenye lengo la kututoa kwenye mjadala muhimu, ili baadae mjadala huo urudishwe kwa kikundi kile kile cha wale waliokosea, tusidanganyike kwa hilo.

Katiba ya JMT 1977 inazungumzia uhuru wa kutoa maoni, uhuru huu umetolewa kwa ujumla wake bila kuangalia maoni yatolewayo yanawalenga wakina nani, haijalishi wawe wanasiasa au vinginevyo, yeyote nje ya kundi hilo anaruhusiwa kutoa maoni yake kuwalenga wahusika, muhimu asivunje sheria za nchi.

Hii kauli ya "tusichanganye dini na siasa" ina nia ovu ndani yake, inatuwekea mipaka tulio nje ya siasa tusiwaulize kulikoni wale wanaotukosea wakiwa siasani, hawa hatutawaacha salama, lazima wajibu maswali yetu kwa usahihi, tena pale ambapo maswali yetu yanahusu rasilimali za taifa, hapo ndio tuheshimiane zaidi kwa majibu sahihi na kuridhisha, sio ngonjera za udini.
 
Asante Baba Askofu Stephen Munga

Tunamshukuru Mungu pia kwa tamko la TEC kwa sababu linazidi kutuonyesha mambo ambayo yalifichika na kuibua watu ambao hawajawahi kulitakia mema Taifa la Tanzania zaidi ya kufikiri kujinufaisha wao na vizazi vyao.

Mbaya sana.
 
Back
Top Bottom