AZAKI zataka utendaji serikali ya Rais Magufuli uwe kigezo serikali zijazo

Pistol

Senior Member
Oct 13, 2015
194
86
Asasi za kiraia nchini (Azaki) zimesema utendaji kazi chini ya kiwango na uwajibikaji mdogo kwa baadhi ya viongozi wa umma, umetokana na mfumo mbovu uliokuwapo muda mrefu ambao haumfanyi kiongozi kuwajibika ipasavyo.
Aidha, zimetaka mfumo wa sasa wa serikali ya awamu ya tano unaowawajibisha viongozi wasiosimamia vyema

majukumu yao, uwekwe katika kumbukumbu rasmi, ili kila serikali inayoingia madarakani ifuate muongozo huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Azaki nchini, Francis Kiwanga, serikali ya awamu ya tano, isiishie kuwasimamisha na kuwafukuza kazi watendaji wabovu, bali pia iboreshe mifumo ya upatikanaji na uteuzi wa nafasi za watendaji kwa kuzingatia sifa na vigezo maalum.


"Mfumo huu wa watendaji kutokuwa wawajibikaji umekuwapo kwa muda mrefu kwa hiyo ubadilishwe ili serikali zote zitakazokuja zifuate mfumo utakaowawajibisha viongozi wazembe. Azaki tumekuwa tukilizungumza hili mara kwa mara tukitaka kubadilishwa mfumo ikiwamo kuwapo kwa Katiba ambayo ina maslahi kwa taifa," alisema.


Kiwanga alisema utekelezaji wa mpango wa malengo endelevu utatekelezeka iwapo kutaimarishwa ushiriki wa asasi hizo pamoja na serikali kugharamia na kutunisha mfuko katika masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.


"Kumekuwa na kasi kubwa ya kupungua kwa ufadhili na wafadhili kwa kuwa wanadai matokeo zaidi ya kazi za Azaki, ni wakati wa serikali sasa kuweka rasilimali za kutosha zitakazoweza kutoa ruzuku kwetu bila ya kuwategemea wafadhili wa nje," alisema Kiwanga.

Naye mgeni rasmi katika tamasha hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sihaba Nkinga, alizitaka Azaki ziongeze uwazi, uwajibikaji kwa wadau ikiwamo serikali, wafadhili ili kuimarisha ubia miongoni mwao.


"Tunapaswa kupitia upya dhamira zetu, kuwa tayari kujifunza na kutoa mchango uliokusudiwa, kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kwenda sambamba na dhamira ya Rais Dk. John Magufuli ya kuwawezesha Watanzania kujiletea maendeleo, kuondokana na umaskini kupitia kauli ya hapa kazi tu," aliongeza kusema Nkinga.

CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom