Waziri wa Maji ameshiriki kikao cha Shukrani na kuagana na watumishi wa Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Umoja wa Mataifa, New York. Watumishi hao wameongozwa na Mhe. Balozi Dkt. Suleiman Haji Suleiman, Kaimu Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Umoja wa Mataifa, New York.
Katika kikao hicho amewashukuru kwa maandalizi na kufanikisha ushiriki wa Tanzania kwenye Mkutano wa Maji wa Umoja wa Mataifa yaani the United Nations 2023 Water Conference uliofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 24 Machi 2023 Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York.
Amesema Kupitia sapoti ya ubalozi wetu tuliweza kuwasilisha hotuba ya taifa kueleza namna Tanzania ilivyopiga hatua katika kuwapatia huduma ya maji wananchi wake pamoja na mipango mbalimbali iliyopo katika kuendeleza sekta ya maji nchini kama sehemu ya utekelezaji wa Lengo namba 6 la Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa. Hotuba hiyo ilitolewa kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 22 Machi 2023.
Vilevile, amemshukuru Mhe Balozi na timu yake kwa kufanikisha kufanya mazungumzo na wabia mbalimbali wa maendeleo ili kujadiliana namna wabia hao wanaweza kuisaidia Tanzania kutekeleza progamu yake ya maji ya mwaka 2023 - 2030 inayotarajiwa kuzinduliwa mwezi Mei 2023.