Date::12/23/2008
ATCL yawatupia mzigo Mramba, Chenge, Lowassa
Leon Bahati
Mwananchi
SAKATA la kusimamishwa kwa Shirika la Ndege Tanzania Tanzania (ATCL) katika kuto huduma limechukua sura mpya baada ya Ikulu pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu, Basil Mramba na Andrew Chenge kuhusishwa hivyo kutakiwa kutoa maelezo.
Wengine ambao nao watatakiwa kutoa maelezo kuhusiana na suala hilo ni Ofisi ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi pamoja na maofisa watendaji wa Wizara ya Miundombinu wakati ikiwa chini ya mawaziri wawili wa kwanza wa serikali ya awamu ya nne, Basil Mramba na Andrew Chenge.
Habari za kuaminika zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana zilieleza kuwa maelezo yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa ATCL, Balozi Mustapha Nyang'anyi kwa Waziri wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa wiki iliyopita, zimehusisha vigogo hao katika kiini cha matatizo ndani ya shirika hilo.
Wiki iliyopita, Dk. Kawambwa alimpa siku saba Nyang'anyi kutoa maelezo yanayohusu sababu zilizosababisha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Anga (TCAA) kunyang'anywa ATCL leseni ya kurusha ndege.
Nyang'anyi aliwasilisha maelezo hayo wiki iliyopita na kutaja baadhi ya mamlaka hizo za serikali kuwa zilipatiwa maelezo ya kina kuhusu hali ilivyo ndani ya ATCL pamoja na mapendekezo yanayotakiwa kufanywa, lakini hakuna kilichofanyika katika kuliokoa shirika hilo.
Waziri Kawambwa pamoja na timu ya wataalamu wake waliyapitia maelezo hayo mwishoni mwa wiki walibaini kuwa katika kufikia maamuzi ya utetezi huo, inabidi wapate maelezo ya kina kwa mamlaka hizo ambazo kwa nyakati tofauti siku za nyuma, walitakiwa tarifa ili wanusuru shirika hilo.
Dk. Kawambwa jana aliliambia gazeti hili kuwa bado wanaendelea kushughulikia maelezo hayo ya bodi na kuahidi kutoa tamko rasmi baada ya kukamilisha mchakato.
Chanzo chetu ndani ya wizara hiyo, zilisema kuwa mkakati huo umefikia mahali pagumu kwa kuwa mbali na kupata maelezo ya vigogo kadhaa, itabidi wachunguze msimamo wa serikali tangu ilipoazimia kuvunja mkataba na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA).
"Utetezi wa bodi umetupa wakati mgumu na wala sifikiri kama maamuzi yanaweza kutoka mapema," kilieleza chanzo hicho kikifafanua:
"Ofisi nyeti sasa zimehusishwa... Maamuzi hayawezi kufikiwa mpaka tupate kauli zao, kama ni kujikwaa itajulikana ni wapi."
Ingawa chanzo hicho hakikuweza kuweka bayana namna watakavyoweza kupata maelezo ya mamlaka hizo, lakini kimeweka wazi kuwa chunguzi huo, utafanywa pia kwa kuzingatia mikakati na mipango ya serikali kwa ATCL kuanzia utawala wa serikali ya awamu ya tatu.
Kulingana na maelezo ya bodi, serikali ya awamu ya nne ilipoamua kuvunja mkataba na SAA, iliweka maazimio ya kutoa fedha za kuifufua ATCL jambo ambalo halikutekelezwa.
Miongoni mwa mambo ambayo yamo kwenye maelezo hayo na ambayo pia Balozi Nyang'anyi aliwahi kulieleza gazeti hili ni serikali kutotekeleza ahadi yake ya kulipa deni la ATCL linalofikia Sh19 bilioni pamoja na mtaji wa dola za Marekani 67 milioni.
Wakati huo huo, serikali imetoa zaidi ya dola 100,000 kwa ajili ya kusafirisha maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Anga (TCAA) kwenda kukagua karakana zinazotumika kufanyia matengenezo ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) nchini Kenya na Afrika Kusini.
Sehemu ya fedha hizo pia itatumika kwa ajili ya kununua vipuri vya ndege ambavyo ni kwa ajili ya matengenezo madogomadogo ya dharura kwenye karakana ya ATCL.
Habari zilizopatikana jijini Dar es salaam jana na kuthibitishwa na Waziri wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa zilisema kuwa mkakati huo ni sehemu ya kuhakikisha kuwa ATCL inarejeshewa haki yake ya kurusha ndege waliyonyang'anywa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Anga (TCAA).
Katika kufanikisha hilo, alisema serikali imekusudia kutumia dola za Marekani 273,000 kwa ajili ya kufanikisha kusudio hilo.
Hata hivyo, Dk. Kawambwa hakuwa tayari kuelezea kwa undani taarifa ya serikali kutoa zaidi ya dola 100,000 kwa ajili ya kusafirisha maofisa wa TCAA na ununuzi wa vipuri, kwa maelezo kwamba ni suala la kiutendaji zaidi.
Wakati huo huo, Ofisa Uhusiano wa TCAA, Abel Ngapemba alithibitisha kuwa wataalamu wake wanaendelea kupitia nyaraka mbalimbali za ATCL zilizopelekwa mahususi kusahihisha kasoro zilizoonekana ndani ya shirika hilo.
Hata hivyo, alisema ni vigumu kueleza iwapo kuna uwezekano wa ATCL kurejeshewa leseni yake katika siku za karibuni kwa maelezo kuwa wataalamu wa TCAA, kwa sasa wametingwa kiasi kwamba imekuwa vigumu kupata upenyo wa kueleza hatua waliyofikia.
"Wataalamu wetu wamekuwa wakifanya kazi usiku na mchana. Hata walipo siyo rahisi kuwasiliana nao maana 'wako-buzzy' (wametingwa) sana," alisema Ngapemba.
ATCL ilikuwa imeahidi kukamilisha mpango wa masahihisho wa nyaraka zake ndani ya siku 10 ambazo ziliisha jana.
Ngapemba alisema kuwa ATCL tayari imewasilisha vielelezo hivyo na sasa inasubiri maamuamuzi ya TCAA.
TCAA waliinyang'anya ATCL baada ya kubainika kuwa na kasoro kadhaa kwenye nyaraka zake za kuendeshea shirika ambazo ni kinyume na kanuni za Umoja wa Mashirika ya Ndege Duniani (IATA).
Serikali iliamua kuingilia kati na kusaidia fedha za kufanikisha mpango wa ATCL kurejeshewa leseni yake baada ya kubaini kuwa shirika hilo linakabiliwa na hali mbaya ya fedha.