MwanaDiwani
JF-Expert Member
- Mar 22, 2013
- 5,536
- 2,268
Raia Kikwete akiwa na Askofu wa kanisa katoliki jimbo la Mbinga, Mhashamu John Ndimbo.
---------------------------------------------------------------------------------------
VIONGOZI wa dini wameendelea kumpa moyo Rais Jakaya Kikwete, wakati huu wa mchakato wa kupata Katiba mpya.
Juzi, Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Mbinga, Mhashamu John Ndimbo, alimtaka kuendelea kuwa na moyo wa uvumilivu kwa watu wanaomkashifu.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake kuhusu msimamo wa baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia bunge hilo, Askofu Ndimbo alisema msimamo huo, unawanyima wananchi haki yao ya msingi.
"Kwanza nampa sana pole Mheshimiwa Rais wetu, Jakaya Kikwete, kutokana na tuhuma nyingi zinazoelekezwa kwake. Mimi ninachomuomba, aendelee kuwa na moyo wa uvumilivu kwa watu hao kwani mti wenye maembe, ndiyo unaopigwa mawe kila siku. Hizo ni chuki binafsi ambazo naamini haziwezi kumkatisha tamaa," alisema Askofu Ndimbo.
Askofu Ndimbo alisema kitendo cha wajumbe hao wa Ukawa, kukataa kuendelea na mchakato huo, ni dhambi kwa kuwa wanachofanya sicho walichotumwa na wananchi.
Askofu alisema kuendelea na msimamo huo, ni kunyima wananchi waliowatuma haki yao ya msingi. Aliwataka walegeze msimamo huo na kuhudhuria vikao hivyo, kwa kuwa msimamo huo, umeanza kukosa mantiki baada ya baadhi ya wajumbe kutoka umoja huo, kuanza kuhudhuria vikao hivyo vya Bunge Maalumu la Katiba.
Askofu Ndimbo amesema wajumbe hao, walitakiwa kuzungumza hoja zao ndani ya Bunge na ingewasaidia kueleweka kwa wananchi na kama hawataki, ni bora waachie ngazi ili wapatikane watu watakaokuwa tayari kushirikiana na wajumbe waliopo, kuandaa Katiba bora, itakayomaliza kero zilizopo.
Alisema kutokuwepo kwa wajumbe hao katika Bunge Maalumu la Katiba, kutachelewesha kupata Katiba mpya na hata ikipatikana, haitakuwa bora, kwa kuwa itakuwa imeundwa na wajumbe wachache.
Kiongozi huyo wa dini alionya kuwa Bunge Maalumu la Katiba, halipaswi kuwa chombo cha kutafuta umaarufu wala sehemu ya chama kufanya kampeni, bali sehemu ya kutimiza majukumu waliotumwa na wananchi, kwa kupanga mipango itakayowapunguzia mzigo wa umasikini na kupunguza pengo kati ya walionacho na wasionacho.
Alitaka vyama vya siasa, kutafuta maeneo mengine ya kufanyia mambo yao na wasitarajie kuungwa mkono na wananchi, kutokana na tabia zao za matusi na dharau wakiwa bungeni, kwani vitendo hivyo ni kinyume na madili na viapo vyao.
Alisema kumlaumu Rais kwa kila jambo ni kumuonea na lazima Watanzania waelewe kuwa matatizo yaliyopo, hayawezi kumalizwa kwa siku moja au na mtu mmoja, bali kwa kushirikiana kwa pamoja na kuvumiliana na hata kunapotakiwa kukosoana, basi watumie busara zaidi na siyo kutumia jazba na matusi kwa viongozi.
Aliwaonya Watanzania kuwa watulivu na kuacha kujiingiza katika mambo yatakayochelewesha maendeleo, kwani muda wanaotumia kufanya hivyo, ni vyema wautumie katika maendeleo ili kuongeza tija na kipato kwenye familia zao.
Pia, aliwataka Watanzania wasiruhusu wanasiasa kuwatumia kama ngazi ya kutaka kufanikisha mambo yao.
"Tusikubali kuwa ngazi ya wanasiasa, tutumie muda wetu kufanya kazi za maendeleo kwani bado tunakabiliwa na changamoto za kila aina katika Taifa letu," alisema.
Kauli hiyo ya Askofu Ndimbo, ni sehemu tu ya mfululizo wa kauli za viongozi wengi wa dini, kumpa moyo Rais Kikwete katika kusimamia mchakato huo, na kuwataka Ukawa kurudi bungeni. Pengine na ushauri huu wa mtu wa Mungu, nao ni vyema kuupa nafasi na kuutafakari.
Chanzo: Habarileo