Anna Mghwira; Siasa safi, mama mwema anayeishi

Suphian Juma

Senior Member
Apr 2, 2019
133
546
ANNA MGHWIRA, SIASA SAFI, MAMA MWEMA ANAYEISHI.

Ukiachana na Televisions kadhaa ambazo nilizowahi kufanya nazo kazi, mitandao ya kijamii imenisaidia kwa asiliamia zaidi ya 90 kunikutanisha na watu maarufu, na muhimu katika Taifa letu. Kwangu mimi Suphian, Mitandao ya kijamii ni Ofisi kama Ofisi zingine za watu wengine. Matokeo ya matumizi chanya ya mitandao ya kijamii ndiyo yaliyonikutanisha na Mgombea wa Kwanza Mwanamke wa kiti cha Urais Tanzania, Mama Anna Elisha Mghwira.

Nakumbuka ilikuwa mwaka 2015 pale Makumbusho Dar, kwenye Mkutano Mkuu wa ACT wazalendo ambapo Mama Anna kama Mwenyekiti wa Chama hicho baada ya kutoa hotuba kwa wagombea Ubunge wa Chama hicho, ndipo tulikutana na kuzungumza mambo kadhaa kuhusu siasa za Taifa na kipekee siasa za Singida kwani mimi na yeye ni wazawa wa Mkoa wa Singida na Kabila moja la Kinyaturu.

Wajibu wangu wa kwanza ulikuwa ni kumsaidia katika kufungua, kusimamia na kuziendesha akaunti/kurasa zake za mitandao ya kijamii. Wajibu huu niliufanya kiufasaha na hatimaye kupelekea Chama na yeye kukubali na kuamua kuniteua kuwa MSAIDIZI WAKE BINAFSI (PERSONAL ASSISTANT).

Mama Anna aliniamini sana. Alinionesha kila aina ya upendo ikiwemo kunipa nafasi ya kujifunza mambo mengi ya siasa na ya maisha kwa ujumla kupitia yeye.

Tukiachana na kumsaidia eneo la mitandao ya kijamii na kumjengea mahusiano mazuri na vyombo vya habari vya ndani na nje ya Nchi, lakini pia nilishirikiana kwa kiwango kikubwa na rafiki yangu Ado Shaibu (Katibu Mkuu wa Sasa wa ACT Wazalendo) katika kufanya Utafiti na kuandaa hotuba zake kama Mgombea Urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka 2015 nchini.

Mama Anna alikuwa kiongozi asiyeogopa mijadala, alipenda kutoa mawazo yake bila woga. Alipenda kutafiti mambo. Mwaka 2015 kwenye mjadala wa MKIKIMKIKI ulioratibiwa na Taasisi ya TWAWEZA (kama sikosei) ulioongozwa na Bi. Maria Sarungi, nadhani mlioona alivyoongea kwa ustadi, alivyojibu maswali kiufasaha na kuidadua Ilani ya Chama chake kwa lugha rahisi.

Mama Anna alipenda Siasa Safi, hakupenda siasa za matusi wala kutishiana. Nakumbuka sometimes tulikuwa tunamwandikia hotuba yenye ukali kidogo lakini akifika kwa hadhira atatamka maneno hayo kwa staha au kuchagua maneno yake bila kuathiri ujumbe lengwa. Hakika alikuwa mwanasiasa mstaarabu wa hali ya juu sana.

Ukiniuliza ni Mgombea gani alifanya siasa safi Uchaguzi Mkuu wa 2015, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, hakika bila kumumunya maneno nitaanza kumtaja Mama Anna Mghwira. Tulizunguka karibia nchi nzima, Mama Anna alizungumza MASUALA tu, hakugusa kabisa PERSONALITIES za wagombea wenzake. Alijikita kwenye kuainisha na kutolea suluhu kero za wananchi katika eneo husika alipofanya mkutano.

Mambo magumu na ya kukera wananchi aliyazungumza kwa STAHA ya hali ya juu na kutuliza munkari wa wananchi. Alikuwa mfariji wa dhati wa wenye shida. Staili hii ya siasa naifananisha na anayoifanya Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan. Unamsema vibaya, ila anakujibu kwa wema.

Wengi huwa wananiuliza kwanini Suphian unatukanwa na hata kudhalilishwa utu wako ila unaishia kunyamaza ama kujibu kwa staha? Nadhani kama hamfahamu basi mjue, ni darasa nilililojifunza kwa watu wa aina ya Mama Anna Mghwira walionizunguka licha ya kuyajua matusi tena huenda zaidi yao watukanaji. Naheshimu USTAARABU KATIKA MIJADALA.

Hata baada ya kampeni na hata alipoteuliwa na Rais Magufuli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mama Anna hakuwa mbali sana nami. Aliweza hata kunipigia simu hata saa nane usiku pindi alipohitaji msaada kwangu ama kunishauri Jambo ambalo aliona nimelitenda visivyo. Si mnajua kwenye siasa sometimes mihemko hutuzidi.

Tulikuwa karibu sana na Mama Anna kiasi ambacho wengi walidhani ni Mama yangu wa kunizaa. Mama Anna alikuwa 'comfortable' kuniagiza vitu binafsi kuliko hata kuomba msaada huohuo kutoka kwa Vijana wa kike waliomzunguka. She trusted me. Nakumbuka hadi Ofisini (ACT wazalendo) walipenda kunitania jina la "Mtoto wa Mama Anna" haha ha

Akiwa na Safari alinitafuta nimsindikize. Akisafiri hata nje ya nchi, nikiwa nchini, akiwa anarudi, lazima atanipigia simu au kunitumia ujumbe wa kumwandalia usafiri airport, na hoteli atakapolala. Alijaa upendo na kujali.

Mama Anna alipenda sana vijana. Kwa nyakati mbalimbali nikiwa MSAIDIZI wake BINAFSI, vijana wengi na Taasisi zao waliniomba kuwakutanisha nae, Mama hakusita. Aliwapa sapoti ya hali na mali. Hakujikweza kwa nyadhifa walizotunukiwa. Mama alikuwa mtu wa watu. She was a man of the people.


Mama Anna alikuwa mtu wa kusoma sana vitabu na kuchambua masuala mbalimbali. Kwenye Laptop yake utakuta kuna maandiko mengi ya siasa na ya kidini. Alilala masaa yasiyozidi sita. Mama Anna alikuwa mwanataaluma. Aliheshimu sana Taaluma ndio maana mara nyingi hakukosa midahalo ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam kama ile ya Kigoda cha Mwalimu Nyerere.

Huyu alikuwa Mama aliyejaa utani. Ukiwa nae huboreki. Ukiwa nae atakuchekesha, atakufurahisha na kukupa matumaini ukiwa na shida au mtihani wowote katika maisha. Alipenda migogoro baina ya watu iishe kwa nasaha tu, na si kwa kutumia taratibu za kisheria. Wananchi wa Kilimanjaro ni mashahidi wa hili.

Mama Anna alipenda Usawa kwa watu. Na hili alilinena na kulitenda hadharani. Ukifuatilia siasa zake akiwa upinzani na hata alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, na hatimaye kuwa mwanachama wa CCM, nyote ni mashahidi, hakuna aliporipotiwa kunyanyasa au kubagua mtu au Kikundi cha watu kwa kigezo cha utofauti wa Itikadi hususani Chama.

Jana Julai 22, 2021 nilipopigiwa simu na kuambiwa Mama yangu huyu Anna ameaga dunia, hadi sasa nahisi kama naota. Kifo kimetunyakulia mtu mwema sana. Inaumiza sana ila hatuna namna zaidi ya kusema kazi ya Mungu haina makosa, na tuendeee kumwombea alale salama daima. Asanteni sana kwa salaam zenu za pole mlizonitumia, na namna mnavyoendelea kumuenzi.

Natamani kuandika mengi, natamani kuona Kitabu chake (Biography) kikielezea Safari ya Maisha yake. Inshallah kitaandikwa.

Lala Salama Mama, nakupenda daima.


Suphian Juma,
Phone: 0717027973
Email: yessuphian@gmail.com
FB_IMG_1626949660771.jpg
 
Neendee vija mohaja wane fika vija mosalimie mama wane mokhanee nemoyanjrie nanguu 💗💗💗💗
 
Back
Top Bottom