Angalia jinsi wasomi wa Vyuo Vikuu wanavyopigwa na maisha mtaani

The Genius

JF-Expert Member
May 29, 2018
820
2,070
Jana nikiwa maeneo ya Palm Village kununua mahitaji ya watoto, kabla sijashuka kwenye gari akaja jamaa mmoja akanisalimia kwa kunichangamkia. Nikadhani ni mtu anayenifahamu, maana imekua kawaida kusalimiwa kwa uchangamfu na watu nisiowajua lakini wao wananifahamu. Kwahiyo sikuona ajabu.

Lakini akaniomba dakika moja ya kuongea na mimi. Nikamruhusu. Akasema "kaka kwanza naomba unisamehe sana kama nitakupotezea muda wako. Mimi naitwa (akataja majina yake) ni mwalimu kitaaluma. Maisha yangu yamekua ya misukosuko sana hata elimu yangu niliipata kwa tabu. Baba yangu alifariki nikiwa mdogo sana na mama yangu hakuweza kunisomesha. Nililazimika kufanya vibarua ili kujisomesha.

Nimehitimu shahada ya ualimu miaka mitatu iliyopita chuo kikuu cha Dar es Salaam lakini sikufanikiwa kupata ajira serikalini. Katika kuhangaika nilipata kibarua cha kufundisha shule moja binafsi, lakini baadae kutokana na idadi ya wanafunzi kupungua, mwenye shule akapunguza walimu mimi nikiwemo.

Maisha hayakua rahisi, nikalazimika kutafuta part time kwenye tuition centres. Nikapata moja maeneo ya Sinza, lakini nako nimefundisha miezi mitano nikapunguzwa maana walimu wa Arts tulikua wengi.

Wiki iliyopita mama yangu alifariki nikaenda Mwanza kumzika. Sikuweza kwenda na familia kwa sababu ya gharama. Siku moja kabla ya mazishi nikapigiwa simu mwanangu mdogo wa miaka miwili amemwagikiwa na maji ya moto akaungua sehemu ya miguu hadi kiunoni. Mke wangu hakua na fedha za kumpeleka hospitali, nikajaribu kuwaeleza ndugu zangu pale msibani wakaruhusu nipewe sehemu ya rambirambi nimtumie mke wangu ampeleke mtoto hospitali.

Ukweli nilijisikia vibaya sana kwa sababu mimi ndio 'firstborn' wa familia na ndiye niliyepata bahati ya kusoma kidogo. Kwahiyo nilitegemewa niwe msaada kwa ndugu zangu lakini na mimi nimekua mzigo, hadi kupewa sehemu ya rambirambi kutatua shida zangu? Nilijisikia vibaya sana lakini sikua na la kufanya.

Tulimzika mama nikarudi Dar kesho yake maana mtoto alikua amelazwa Mwananyamala. Baada ya siku mbili aliruhusiwa kuendelea kuuguza majeraha nyumbani.

Katika harakati ya kutafuta kazi kuna mtu mmoja nilimtumia nakala ya vyeti vyangu mkoani Mbeya anisaidie. Leo asubuhi akanipigia simu kwamba natakiwa kwenye usaili kesho. Nikamwambia kwa muda huu siwezi kupata usafiri, akasema nifanye niwezavyo kesho niwe Mbeya.

Mfukoni nilikua na TZS 22,500/= tu, nikamuachia mke wangu 20,000/= nikabaki na 2,500/= inisaidie nauli ya daladala nifike Ubungo. Lakini nikasikia sauti ikiniambia tembea kwa mguu utakutana na muujiza wako njiani. Nimetembea kwa mguu kutoka Kawe hadi hapa, nimekutana na watu wengi lakini sijathubutu kumwambia yeyote shida yangu.

Nilipokuona wewe nikajisikia amani kukuelezea. Naomba usinifikirie vibaya. Mimi sio tapeli. Vyeti vyangu hivi (anatoa bahasha yenye vyeti kwenye begi na kunionesha). Naweza kukupa namba ya mmiliki wa shule niliyowahi kufundisha au namba ya mke wangu ukitaka kumpigia kujiridhisha (namwambia haina haja).

Akaendelea "Nimeamua kukuambia wewe kama mwanaume mwenzangu japo sikujui lakini moyo wangu umesikia amani kukushirikisha shida yangu. Najua unaweza kunishangaa na kuona najidhalilisha lakini sina namna.

Ombi langu kwako unisaidie 30,000/= tu nauli ya kufika Mbeya nitadandia magari ya IT. Nifike usiku wa leo ili kesho asubuhi niwe kwenye usaili. Sijui mke wangu na watoto wataishije maana kodi tunapoishi imekwisha tangu December mwaka jana. Lakini hilo sijali sana, nakuomba tu unisaidie nauli nifike Mbeya nikafanye usaili, naamini nitapata kazi ili niweze kuitunza familia yangu.

Alipomaliza kuongea nikajikuta nimekua "off mood" ghafla. Ile hamu ya kwenda kununua mahitaji ya watoto ikaisha, nikatoa 90% ya pesa niliyopanga kwenda kufanyia shoping nikampatia.

Nikajiuliza kuna faida gani kuwanunulia wanangu mahitaji yasiyo ya lazima wakati pesa hiyo inaweza kuokoa maisha ya familia nyingine? Huyu jamaa akifanikiwa kupata kazi ataweza kuihudumia familia yake vizuri, tofauti na vitu ambavyo nikiwanunulia akina Nicole baada ya siku chache vimeharibika.

Akaipokea ile fedha kama vile haamini macho yake. Akasema "Naomba unisamehe shida imenifanya nijielezee bila hata kujua jina lako" Nikamwambia naitwa Godlisten.

Akachukua leso na kujifuta machozi, kisha akasema "Godlisten Mungu akubariki sana. Sina neno zuri zaidi la kukuambia, lakini nakuombea Mungu asikupungukie, watoto wako wasione kiu wala njaa. Umenivusha mahali pakubwa sana. Kiasi ukichonipatia nusu nitatuma kwa mke wangu na nusu nitaitumia kwenye safari yangu. Naamini nitafika salama na nitapata kazi"

Akaondoka lakini nikawaza mambo mengi sana. Huyu ni msomi wa kiwango cha degree ya chuo kikuu, imekuaje akafikia hapa? Je kuna wangapi kama huyu wanahanagaika mtaani?

Nilipokua kidato cha kwanza (miaka 20 iliyopita) niliamini ukifika Chuo kikuu wewe ni boss. Ni mtu ambaye jamii ina matumaini makubwa na wewe. Unaweza kutumia elimu yako kufanya mabadiliko chanya kwenye jamii. Lakini leo mhitimu wa chuo kikuu anakosa hata nauli? Anapita mtaani kuomba? Kweli tumefikia hapa kama taifa?

Je, Serikali imefikiria kuchukua hatua yoyote kunusuru hali hii? Kijana kama huyu niliyemsaidia jana wapo wengi mtaani. Bora huyu amekua muwazi, wengine hawasemi wanabaki na shida zao moyoni. Mwisho wa siku wanapata msongo wa mawazo na wanaweza kufanya maamuzi magumu kama aliyofanya yule kijana kule Pugu kwa kujiua.

Nadhani kuna haja ya kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu hali yetu kiuchumi na ajira kwa vijana. Serikali haiajiri, sekta binafsi zina hali mbaya sana, vijana waende wapi? Serikali inapaswa itengeneze mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili ziweze kutoa ajira kwa vijana, lakini kila siku biashara zinafungwa.

Mashule yanafungwa kwa kukosa wanafunzi, NGO zinafungwa kwa kukosa fund, biashara zinafungwa kwa kushindwa kujiendesha. Yani kila siku mamia ya watu wanarudi mtaani baada ya kupoteza ajira. Vijana nao wakitaka kujiajiri wanashindwa kwa sababu urasimu ni mkubwa sana. Lakini tunazidi kuzalisha wasomi kila mwaka. Waende wapi? Wafanye nini?

Malisa GJ
 
Hii mbona ipo ndugu!!!!

Tunasaidiana sana mtaan huku japo ni kimya kimya!!!!

Hii awam tunaopata msoto....max!!, (kidogo) wengi wetu ni wale ambao tuliambulia ajira enz ya Jk!!! Ama...Wenye connection ya bussines!!!

Juu ya yote Minne sio mingi tutavuka tuu!!!!!
 
Inawezekana akawa na shida kweli, lakini mkwara ambao ningempiga ningejua tu kama ni tapeli au la, ninge mwambia kijana una bahati sana, mimi pia hapa nilipo naelekea mbeya, itakuwa vyema sana tukiongozana.

Huku namsoma kwa umakini lugha ya mwili na kwenye sura nikisubiri jibu, hapo lazima tapeli umjue tu, mwili unaongea ukweli kuliko maneno ya mdomoni.
 
Back
Top Bottom