Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI II -- 38*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Mosi, Sarah kutambua kama Jona anaishi kwa Miranda. Na pili, Lee kummaliza makamu wa raisi ndani ya nchi ya Mongolia.

Litakalojiri, si mimi wala wewe anayejua. Ila ni wazi kiti kilikuwa cha moto.

ENDELEA

Basi na muda ukasonga kama ilivyo ada. Ilipogonga saa nne ya usiku, mtu mmoja akazama ndani ya jengo la Miranda. Mwanaume huyu alikuwa amevalia suti nyeusi na barakoa nyeusi usoni.

Ni ajabu mtu kuvaa suti katika kazi kama hizi. Mtu huyu alijibana nyuma ya ukuta, akatazama usalama. Kulikuwa ni kimya na sebuleni alikuwa amekaa Miranda na Marwa wakitazama televisheni.

Huku vyumbani kote kulikuwa gizani. Na kule getini mlinzi alikuwa amejilaza kwenye kiti chake akichokonoa meno. Hakuwa anajua kinachoendelea.

Mwanaume yule mwenye barakoa akajongea dirisha la kwanza, akachungulia. Akatoka hapo akaizunguka nyumba kwa nyuma, kisha akatazama tena dirisha lingine.

Mara akasikia sauti ya kitu kikitembea. Akajibania kwenye ukuta kwanguvu, mkono wake wa kuume akiushikizia kiunoni ambapo aliweka silaha, bunduki ndogo.

Alipotulia hapo kwa sekunde nne, akagundua hamna hatari yoyote. Basi akaendeea tena lile dirisha na kuchungulia. Chumba hicho ndicho alalacho Marwa. Tayari ameshatazama anacholala Miranda, na anacholala Jona, ila hakugundua kitu. Kulikuwa na giza na pupa zake hazikumfanya akaona jambo zaidi tu ya mwili uliofunikwa nusu shuka.

Basi alipotoka tena hapo akawa amebakiza sehemu moja tu. Matumaini yake yote yakawepo hapo kuwa ndiyo itakuwa mahali penye kitu wanachokitaka.

Ila hakujua chumba hicho kilikuwa ni cha mfanyakazi wa ndani. Na msichana huyo hakuwa amelala. Ni muda mfupi ametoka kuoga na kumbe ndiye yeye ambaye vishindo vyake vilisikika hapo kabla.

Basi bwana yule mwenye barakoa, akachungulia. Akameona mwanamke huyu akijifuta. Napo akagundua si penyewe. Ila sasa akashindwa kutoka hapo upesi. Macho yake yaliganda kwenye mwili wa mwanamke ulio uchi.

Japo ilikiwa ni giza, akatumbua macho aambulie chochote kitu.

Akachukua hapo kama sekunde sita, msichana akagundua jambo. Akageuza shingo yake kutazama dirishani, mwanaume yule mwenye barakoa akajificha upesi.

Hakufanikiwa kumwona.

Mwanaume yule akanyata na kurudi kule alipojibania mara ya kwanza alipozama ndani. Akatulia hapo kwa sekunde kama nne tena, kisha akaanza kurejea zoezi lake kwa mara nyingine ili ahakiki kabla hajaondoka na jibu la mtu wanayemtafuta hayupo hapo.

Akapitia dirisha la kwanza. Salama salmin. Akiwa kwenye dirisha la pili, akasikia vishindo vikubwa! Haraka akajivuta na kujibana kwenye kona ya mbele.

Alisimama hapo kwa tahadhari sana. Na vishindo vile alivyosikia havikukoma, vikaendelea kujita kumfuata. Akatambua wazi kuwa ajaye ni mlinzi.

Sasa zoezi likawa linaendea kubadilika. Hakutaka kuacha alama yoyote hapa ila ikaanza kuonekana itashindikana maana endapo mlinzi huyu akimwona, basi hatoweza kumwacha hai.

Vishindo vikaendelea kusonga. Miguu hii ya mlinzi ilikuwa inaburuza haswa. Sijui alijifunzia wapi ulinzi huyu bwana. Alipiga hatua nne zaidi, na hamaki akajikuta mikononi mwa mvamizi!

Kilichosikika hapo ni mtu akigugumia tu, na mlinzi akawa amemaliza habari yake. Akatuliwa chini taratibu na yule jamaa sasa akawa yupo huru zaidi. Sasa akatazamia madirisha yaliyobakia.

Akanyata na kunyata. Akatazama lile dirisha la chumba anacholala Jona, hapo akasita kidogo. Akajiwa na fikra. Kamaa kule sebuleni yupo mwanaume na mwanamke, na kile chumba kingine yupo mwanamke, hichi yupo nani?

Kabla hajaacha dirisha hili, akachomoa kurunzi yake ndogo na kumulika ndani. Mwanga wa kurunzi hii ulikuwa mdogo, kaduara kake ka mwanga kalikuwa chenye ukubwa wa sarafu ya mia mbili.

Akaangaza usoni mwa mtu yule aliyekuwa amelala, akagundua ni Jona! Akajikuta anatabasamu.

Ila sasa alivyo mjinga, asiondoke akataka kwenda kwenye lile dirisha la msichana wa kazi akatazame tena. Basi akanyata na kufika hapo, akachungulia. Hakumwona mwanamke.

Akazubaa hapo kwa sekunde kama tano akiangazaangaza maana ilikuwa giza. Ila punde akasikia sauti ya mguu ukiburuza. Akaangaza upesi. Kidogo akatokea mtu konani, alikuwa ni Miranda!

Mwanaume yule mwenye barakoa akatupa risasi mbili. Miranda akawahi kujificha ila alikuwa tayari amejeruhiwa. Bega lake la kushoto lilikuwa linachuruza damu!

Bwana yule mvamizi asipoteze muda akadaka ukuta na kurukia nje. Miranda naye akajaribu, ila maumivu ya mkono yakampatia shida. Japo alifanikiwa, ila hakuwa ndani ya muda. Kwa mbali akaona gari likiyoyoma kwa kasi!

Akarudi zake ndani. Sebuleni akamkuta msichana wa kazi ma Marwa. Haraka wakampatia huduma ya kwanza kwa kumtia dawa ma kumfunika jeraha. Uzuri risasi haikupenya ndani, bali iliparaza bega na kwenda zake.

Wakiwa wanampatia huduma hiyo, msichana wa kazi akaeleza namna alivyotilia shaka kwamba kuna mtu nje. Na zaidi hisia zake hizo zikathibitishwa na sauti ya mguno. Kumbe ndo ile iliyokuwa ya mlinzi.

Hapo Miranda akapata maswali. Ni nani yule mtu na alikuwa anafanya nini. Kwa akili ya kawaida, baada ya kujadili, wakagundua watakuwa ni watu wa Sheng. Na hapo walikuja sababu ya kumtafuta Jona ndiyo maana walikuwa wanapeleleza dirishani.

Sasa wakapata shaka. Kama watu hao watakuwa wamegundua kuwa Jona yupo hapo, watafanya nini?

**

Ngo! Ngo! Ngo!

Shao akafungua mlango. Uso kwa uso akakutana na kijakazi wake aliyevalia suti. Akamkaribisha ndani na wakaketi sebuleni. Kijakazi yule akampa mrejesho wa kazi waliyotoka kufanya.

Amemwona Jona, yupo mikononi mwa kijakazi wa BC. Ila akaeleza pia ameonekana alipokuwa akifanya kazi hiyo. Hapo Shao akaghafirika!

Akalalama kazi imeharibika kwani watu hao watachukua tahadhari kutokana na tukio hilo. Hapo hamna kazi yoyote iliyofanyika!

Akamtaka kijakazi huyo aende zake amwache mwenyewe afikirie cha kufanya. Kijakazi akaenda zake. Shao akafikiri sana. Mwishowe akaona sasa cha kufanya ni kuanza kupanga mipango ya kuwashambulia wakina BC maana ameshajua Jona yupo mikononi mwao.

Akawaza kama kazi hiyo anapaswa kumshirikisha Sheng, akaona haina haja. Ataifanya na kuimaliza mwenyewe.

**

Hakuwa amepumzika siku hii nzima. Kutwa allikuwa kwenye safari, na hata usiku huu hakuwa mtu wa kupumzika bali yupo kazini.

Tayari Lee ameshazama ndani ya Mongolia, kitambo tu. Na tayari alishasonga eneoni ambapo anatakiwa kufanya tukio. Eneo ambapo makamu wa raisi wa China yupo kimalazi.

Eneo hilo lilikuwa linalindwa na watu lukuki hapo nje. Na pia huko ndani walikuwa watu kadhaa wakienda huku na kule.

Lee akatoa hadubini na kupekua eneo hilo kila pande. Alikuwa umbali wa kama kilomita mbili na nusu. Aliporidhika na alichokipata kwa hadubini, akairejesha begini alafu akavalia barakoa.

Mwanaume akazama kazini.


***
 
Back
Top Bottom