Akufaaye kwa dhiki

Akufaaye kwa dhiki

Tamu3

Member
Joined
Feb 17, 2023
Posts
28
Reaction score
18
AKUFAAYE KWA DHIKI

1.
Hapo za kale zamani, hadithi inaanzia,
Kijiji cha ndani ndani, mume na mke likaa,
Nyumba yao ya majani, humo waliishi pia,
Akufaaye kwa dhiki, huyo rafiki wa kweli.

2.
Walikuwa wakulima, wafugaji vile vile,
Walizalisha mtama, nawo kwa wingi mchele,
Wakajawa na heshima, ndani ya kijiji kile,
Akufaaye kwa dhiki, huyo rafiki wa kweli.

3.
Walikuwa wakarimu, kwao hawo majirani,
Waliishi kwa nidhamu, kwa wengine mfanoni,
Kukiwa na jambo gumu, liitwa suluhisheni,
Akufaaye kwa dhiki, huyo rafiki wa kweli.

4.
Ikifika kiangazi, mazao yote livuna,
Kiweka uangalizi, ghalani yakashonana,
Pia kuzuia wezi, mazao wakiyaona,
Akufaaye kwa dhiki, huyo rafiki wa kweli.

5.
Pale kwao kijijini, palikuwa na mnada,
Mazao waliuzeni, ili watatue shida,
Mengine yalibakini, kama ya kesho ziada,
Akufaaye kwa dhiki, huyo rafiki wa kweli.

6.
Desturi kijijini, sherehe ni kiangazi,
Mazao yakivunweni, kula inabaki kazi,
Fahali akachinjweni, hawa wawili wazazi,
Akufaaye kwa dhiki, huyo rafiki wa kweli.

7.
Ndafu alipokauka, na vyakula wamepika,
Mke akarukaruka, mayowe akipayuka,
Adai nyumba yawaka, watu wakakurupuka,
Akufaaye kwa dhiki, huyo rafiki wa kweli.

8.
Wachache watu lifika, ili moto kuuzima,
Lakini walipofika, likuta wali na nyama,
Walikula wakachoka, walisaza wakihema,
Akufaaye kwa dhiki, huyo rafiki wa kweli.

9.
Mmoja akauliza, lipiga yowe la nini,
Moto haujaunguza, haukuwepo darini,
Vipi mmetupumbaza, na tuje penu nyumbani,
Akufaaye kwa dhiki, huyo rafiki wa kweli.

10.
Mwenyeji akajibia, jibu lililo makini,
Janga tulisingizia, rafiki mwema kujua,
Nyumbani mlowadia, ni watu wema tambua,
Akufaaye kwa dhiki, huyo rafiki wa kweli.

11.
Wengine liposikia, yowe langu nalipiga,
Hapa hawakutokea, si kwa sababu ni woga,
Bali walipuuzia, yowe tulilolipiga,
Akufaaye kwa dhiki, huyo rafiki wa kweli.

Denny Jeremias Kitumbika,
Mtunzi wa mashairi na ngano za Kiafrika
mufindi Tanzania 7.4.2023

1710780580480.jpg
 
Back
Top Bottom