Akinyi Must Die (Ni lazima Akinyi Afe)

Akinyi Must Die (Ni lazima Akinyi Afe)

Akinyi Must Die (Ni lazima Akinyi Afe) - 02



Sauti ya kiume "Bwana Yesu asifiwe kanisa?"

Ilikuwa ni sauti ya Muinjilisti ikisikika vema tokea kanisa la Kiinjili la kilutheri Tanzania,maeneo ya Nyamhongolo.

Waumini "Aminaaaa"

Ilikuwa ni jumapili nyingine tulivu ambayo ilikuwa ni utaratibu wa mama Deo kila ifikapo siku hiyo yeye na familia yake hujumuika pamoja na waumini wengine kwa ajili ya kumsifu na kumuabudu Mungu.

Muinjilisti "Kama ilivyokuwa imetangazwa na uongozi wa kanisa,leo itakuwa siku ya kipekee ya wageni ikiambatana na kuwaombea watoto wadogo na kuwakabidhi mikononi mwa Bwana"

Muinjilisti aliendelea "Nadhani mbele yenu kama mnavyoona kuna ugeni mkubwa,sisi kama kanisa mara zote wageni wanapotutembelea huwa tunakawakarimu kwa nyimbo na mambo mengi,lakini pia huwa tunawapa fursa ya kusalimia kanisa,pia Baba mchungaji atakuja kuwakaribisha vyema wageni wote waliopata nafasi kuabudu pamoja nasi siku ya leo"

Muinjilisti "Basi tusiendelee kupoteza muda nimuombe mzee wa kanisa aje amkaribishe Baba mchungaji"

Mzee wa Kanisa "Bwana wetu Yesu Kristo apewe sifa"

Waumini "Ameeen"


Aliendelea "Nisingependa kupoteza muda kwa maana mengi yamesha semwa na Muinjilisti wetu wa Kanisa,hivyo nichukue nafasi hii kumkaribisha Baba Mchungaji"

Aliendelea "Baba mchungaji karibu sasa kisemeo ni cha kwako"


Baba Mchungaji "Ahsante sana Mzee wetu wa kanisa lakini pia nimshukuru Muinjilisti Siphael Lelo kwa ukaribisho wa Utangulizi,Mungu awabariki sana"

Baba Mchungaji "Ndugu waumini wenzangu,leo ni siku ya pekee sana kusimama tena mbele yenu,napenda nimshukuru mwenyezi Mungu kwa kunipatia fursa hii ya pekee,kama mtakumbuka wiki iliyopita nilitangaza hapa ya kwamba,jumapili ya leo ambayo ni siku ya Bwana,tutapokea wageni ambao wataungana nasi katika kumuabudu Mungu,mbali na mambo mengine pia mlitangaziwa itakuwa ni siku maalumu kwa ajili ya kuwaombea watoto wetu wadogo na ambao hawajawahi kukabidhiwa mikononi mwa Bwana"

Aliendelea "Basi nisipoteze muda kwasababu muda nao umetuacha sana,nipende kuwakaribisha wageni wote waliotutembelea leo lakini kwa upekee nipende kumkaribisha Mchungaji Timotheo Owino kutoka kule Kisumu Kenya ambaye yeye na Mkewe leo wameona watubariki kama kanisa kwa kuabudu pamoja nao"

Aliendelea "Lakini pia nipende kukukaribisha Pastor kwa ajili ya kutuendeshea ibada pia utakuwa na jukumu la kuwaombea watoto wadogo na kuwakabidhi mikononi mwa Bwana"


Baada ya muda wa ibada kuisha,ilianza kazi rasmi ya kuwaombea watoto,kila mwanamke au familia ya baba na mama ambao walikuwa na mtoto mdogo walipaswa kusogea mbele ili kuwekwa mikononi mwa Bwana.Basi kwakuwa familia nzima ya mama Deo ilihudhuria ibada hiyo,hawakusita kwenda mbele na yule mtoto mdogo kwa ajili ya mibaraka ile ya maombezi.

Mchungaji Owino " Nilipomshika kichwa huyu mtoto ili nimuombee,nimehisi nguvu zinanitoka ghafla ndani yangu na najihisi roho wa Bwana amenishukia"

Aliendelea "Huyu mtoto anaitwa nani?"

Mama Deo "Mmh! ni stori ndefu Pastor"

Mchungaji Owino "Anaitwa ni stori ndefu!?"

Mama Deo "Hapana Pastor hana jina"

Mchungaji Owino "Oooh!, ok kaa pale nisubiri nifanye huduma hii nakurudia nikimaliza maana mwanao anakitu cha pekee sana mama"


Haikuchukua muda yule mchungaji Timotheo Owino kumaliza ile huduma,alipokamilisha alimuita mama Deo kwa ajili ya mahojiano zaidi na kutaka kufahamu upekee wa yule mtoto.Mama deo hakutaka kuficha kitu alimsimulia yule mchungaji kila kitu kuhusu yule mtoto.

Mchungaji Owino "Haleluya,nakushukuru sana Mungu wa Mbinguni kwa ajili ya kiumbe huyu"

Aliendelea "Sasa kama ndivyo nakuomba huyu mtoto kuanzia leo aitwe AKINYI,na pia mimi na mama mchungaji tutazungumza na nitashirikisha na uongozi wa kanisa pia na kama ikiwapendeza nyinyi nyote basi tunaomba tuondoke na huyu binti mzuri tukamtunze"

Mama Deo " Sawa baba mchungaji sisi hatuna tatizo ila ni vema serikali ya mtaa akiwemo Mwenyekiti na Mjumbe wakafahamu suala hili maana huyu mtoto nilikabidhiwa mimi nimuangalie"

Mchungaji Owino "Basi leo jioni tutakuwa wageni nyumbani mwenu nahitaji tushiriki maombi na familia yako"

Mama Deo "Karibu sana baba mchungaji"

Baada ya ibada mama Deo na familia yake hawakutaka kupoteza muda waliianza safari ya kurudi nyumbani ili kujiandaa kwa ugeni ule jioni ya siku hiyo.Mchungaji Timotheo Owino pamoja na mkewe waliongea na uongozi wa lile kanisa ikiwemo mchungaji ambaye alikuwa mwenyeji wake na wakapewa baraka zote za kuitembelea ile familia ya mama Deo kwa usiku ule.

Sasa ilipofika jioni mchungaji Timotheo Owino Okumu na mkewe waliongozana na muinjilisti Siphael Lelo aliyekuwa akiyafahamu makazi ya waumini wa kanisa lake mpaka kwa familia ya mama Deo.

Ilipofika usiku mama Deo alipokea Ugeni mzito ukiongozwa na Muinjilisti Siphael Lelo aliyekuwa Muinjilisti wa Kanisa alilokuwa akiabudu la Kilutheri Tanzania kwa Usharika wa Ilemela aliyeambatana na Mchungaji Timotheo Okumu Owino pamoja na Mkewe.

Mama Deo "Karibuni sana jamani"

Mchungaji Owino "Ahsante sana binti yangu"

Baada ya kupata chakula na kujumuika wote kwa pamoja katika maombi usiku ule,Mchungaji Timotheo Owino aliyekuwa ameambatana na mkewe pamoja na Muinjilisti Siphael Lelo,waliamua kuondoka kwa makubaliano kwamba,baada ya siku tatu kuwepo pale kanisani wangeomba kuondoka na kile kitoto kichanga kurejea kwao nchini Kenya endapo wangekubaliwa na Uongozi wa kanisa pamoja na mamlaka za kiserikali.

Uongozi wa kanisa ulichukua jukumu la kufuatilia lile suala la mtoto kwa mamlaka husika za nchi ikiwemo jeshi la polisi kwasababu upelelezi wa kesi ya msingi ulikuwa bado haujakamilika,hivyo mama Deo angechukua jukumu la kuwakabidhi yule mtoto pengine angekuwa mwenye atia kulingana na sheria za Jamhuri.

Mamlaka za nchi ikiwemo Ustawi wa jamii pamoja na Jeshi la polisi baada ya kujiridhisha kwamba taasisi ya kikanisa ndiyo ilikuwa ikimuhitaji yule mtoto ilitoa ruksa ya kwamba wamchukue wakamtunze na wahakikishe wanampatia mahitaji yote muhimu ya kibinadamu na wawe wanatoa taarifa muhimu kwa uongozi wa kanisa ili kuwezesha kufahamu maendeleo ya mtoto.

Kweli!,baada ya ziara ya kikanisa ya mchungaji Timotheo Okumu Owino kukamilika walimchukua yule mtoto mdogo ambaye walimpatia jina la Akinyi na kuondoka naye kuelekea nchini Kenya katika kaunti ya Kisumu.


AFTER 15 YEARS SOME WHERE IN TARIME (BAADA YA MIAKA 15 MAHALI FULANI TARIME)



Sauti ya kiume "Mama mseti"

Sauti iliendelea kuita "Mamaa mseetiii"

Mama Mseti "Abheeeee"

Sauti ya kiume "Tacho omahe(Hebu njoo)"


Aliendelea "Hivi ulishamueleza Bhoke lile suala?"

Mama Mseti "Nilimwambia lakini alikuwa analia anasema hataki"

Sauti ya kiume "Tarehe 16 ni wiki ijayo,hivyo hakikisha unapeleka jina lake kwa mzee Machera"

Mama Mseti "Sawa"

Katika kijiji cha Magoto wilayani Tarime,sherehe za tohara na ukeketaji zilipambana moto,ilikuwa ni ufahari kijana mwenye umri mdogo kupata tohara ya kimila na kiutamaduni isiyokuwa na ganzi ndani yake kwani ilionyesha ujasiri wa hali ya juu,pia kama ungeweza kuvumilia tohara ile iliyokuwa na maumivu makubwa,basi iliashiria kwamba ungeweza kupambana hata na Simba.Pamoja na tohara zile kwa vijana wa kiume,pia kulikuwa na ukeketaji kwa mabinti wadogo ambao walianza kuvunja ungo,suala la ukeketaji kwa mabinti wadogo licha ya kuacha maumivu na makovu kwa mabinti lakini lilileta heshima na ufahari kwenye familia aliyotekea binti husika.Hivyo kila ilipokuwa ikifika mwezi wa 11 wa kila mwaka kulikuwa kukifanyika sherehe kubwa za kimila na kiutamaduni,zilipishana tu tarehe kati ya tohara na ukeketaji lakini mwezi ulikuwa ni mmoja.

Mama Mseti "Juzi nimeongea na baba yako nimejaribu kumueleza lakini haelewi mwanangu"

Mama Mseti alikuwa akiongea na binti mrembo aliyekuwa na sifa za kila aina za kuitwa mwanamke mzuri,ingawa alikuwa na umri mdogo lakini alikuwa na akili ya kupambanua mambo kama mtu mzima.

Binti "Lakini mama kwa nini baba anataka kunifanyia hivi?"

Mama Mseti "Mwanangu baba yako unamfahamu namna alivyomkali,pia ukikataa kufanyiwa ukeketaji mimi atanipiga mpaka aniue maana nitakuwa nimevunja mila na desturi zetu"

Mama Mseti aliendelea "Nakuomba uvumilie tu mwanangu,mbona mwenzio Wesiko alifanyiwa na sasa yupo mzima tu"

Mama mseti aliendelea kumshawishi binti Bhoke ili akubali kufanyiwa ukeketaji ili kuiheshimisha ile familia.Bhoke aliingia ndani akaanza kulia sana akiamini ule ukeketaji ulikuwa unaondoa sifa ya usichana wake.
Hakupenda kusikia kitu kinaitwa ukeketaji na ilikuwa ikimuumiza sana kuona mama yake pamoja na baba yake wakilazimisha lile jambo,yeye aliamini wazazi wake ndio wangekuwa mstari wa mbele kulikataa lakini haikuwa hivyo.Ilikuwa kabla ya ukeketaji majina yote ya mabinti waliofikisha umri wa kukeketwa yalipelekwa kwa Ngariba,Ngariba aliyefahamika kwa wakati huo na asiyekuwa na huruma hata kidogo alifahamika kwa jina moja la Nyanchimweru aliyekuwa mke wa mzee maarufu hapo Kijijini Magoto aliyefahamika kama Mzee Machera Wanyonyi.

Sauti ya kiume "Hivi hela zangu nilizoweka chini ya mtungi zimeenda wapi?"

Alikuwa mzee Gisiri Mnanka au Baba Mseti akimuuliza mkewe.

Mama Mseti "Mi hata sijui"

Baba Mseti "Hujui!,tatigha kundetera Obhokangi(Acha kuniletea ujinga),nazitaka hizo hela"

Mzee Gisiri alikuwa akimuuliza mkewe Mama Mseti kuhusu hela zake huku akiwa mwenye Jazba asiyekuwa na mzaha hata kidogo.

Mama Mseti "Sasa jamani hizo hela nichukue nipeleke wapi!"

Mama Mseti aliendelea kujitetea kwa kutolea ufafanuzi kwa upole na sauti ya hamaki na mshangao.

Baba Mseti "Nikirudi jioni kutoka mnadani nizikute hizo hela"

Ilikuwa ni sauti ya Mzee Gisiri iliyojaa jazba na msisitozo huku akifungua mlango na kuondoka zake.Mama mseti aliwaza sana ni nani atakuwa amechukua hela za mumewe ambaye ni mkorofi kupita kiasi.
Alianza kuzitafuta zile hela ndani ya nyumba bila kuambulia chochote.
Jioni ile mama Mseti alimsubiri Bhoke binti yake atoke shule uenda akawa anafahamu kuhusu hela za Baba yake,mama Mseti aliendelea kusubiri bila mafanikio ya kuonekana Kwa Bhoke,aliamua kuondoka mpaka kwa rafiki yake Bhoke ambaye aliitwa Wesiko Gisunte ili kuona kama mwanae amepita kwa huyo rafiki yake.

Wesiko "Kwani hajarudi?"

Aliendelea "Aliponipitia twende shule alikuja akasema nimsindikize Senta akapande gari anaenda Nyabitocho kupeleka hela za ng'ombe baba yake kamtuma,akaniambia atawahi kurudi"

Mama Mseti "Huyu mtoto anataka kuniingiza kwenye matatizo"

Mama mseti aliendelea kujisemea huku machozi yakimtoka akimhofia zaidi mumewe.

Wesiko "Kwani hamkumtuma?"


Mama Mseti "Amechukua hela za baba yake katoroka"

Wesiko "Sasa itakuwaje bhamure"

Wesiko ambaye alikuwa rafiki yake kipenzi na Bhoke alionekana kushangaa sana.

Mama mseti alirudi nyumbani kwake huku akiwaza namna itakavyokuwa.Haukupita muda mzee Gisiri akawa amerudi nyumbani na mama Mseti kumueleza kila kitu.

Baba Mseti "Huyo atakuwa amekimbia Saro(ukeketaji)"

Mzee Gisiri Mnanka alieleza kwa jazba sana kiasi kwamba ungejichanganya mbele yake ilikuwa ni halali yake.

Aliendelea "Nilikwambia tangia mwanzo uwe makini na huyu mtoto lakini ukawa mbishi,ona sasa,hii aibu tutaiweka wapi mama Mseti?,hivi unadhani jamii itatuchuliaje?,huyu mtoto asipopatikana na wewe uondoke hapa la sivyo nitakuua!"

Muda huo mama Mseti alikuwa ametulia tuli kama maji ya mtungi maana alifahamu kabisa angenyanyua mdomo wake,basi ingekuwa mwisho wa maisha yake.Asubuhi na mapema mzee Gisiri alienda kumuamsha kijana wake mkubwa aliyeitwa Mseti ambaye hakuwa mbali na Boma la Baba yake na kumueleza namna hali ilivyokuwa,Mseti alichukua Baiskeli akambeba Baba yake wakaanza safari ya kuelekea kijiji cha Nyabitocho ili kumtafuta binti Bhoke.

Bhoke "Nauli ya kuelekea Musoma ni ngapi?"

Ilikuwa ni sauti ya Binti Bhoke akimuuliza mmoja wa Kondakta wa Hiace zilizokuwa zimepaki stendi ya Tarime mjini zikiwa na ruti ya kuelekea Musoma.

Kondakta "Kwa wewe mwanafunzi ni elfu moja miatano"

Bhoke alichomoa hela alizokuwa ameziweka kwenye mfuko wa sketi yake ya shule aliyokuwa amevaa mpaka wakati huo.

Bhoke "Hii hapa"

Kondakta "Matiko,hebu mkatie huyu mtoto tiketi acha kushangaa bhana"

Kondakta "Ingia ukae pale nyuma jirani na yule mama"

Baada ya kupewa tiketi yake Bhoke alipewa pia utaratibu wa kukaa ndani ya ile gari,binti Bhoke aliingia na kuelekea nyuma kabisa ya siti jirani na mama mmoja wa makamo.

Wakati huo mzee Gisiri na mwanaye Mseti walipofika pale kijijini Nyabitocho walianza kumsaka Bhoke bila mafanikio yoyote.Waliendelea kutafuta maeneo mbalimbali pale kijijini ikiwemo kuuliza watu aliyofahamiana nao lakini hakufanikiwa.

Baba Mseti "Sasa atakuwa ameenda wapi?"

Aliendelea "Nitampata tu,we subiri uone"

Mzee Gisiri alisema kwa jazba huku akiendelea kumtafuta Bhoke binti yake.



Itaendelea............................
 
Mi hata najua basi,
Vipi amekukumbusha yule jamaa wa skuli?
Mimi nimezaliwa mkoa wa Mara wazazi walikua wafanyakazi huko..so jirani na kwetu kulikua na familia kuna kina Akinyi...Odongo...nimesahau na wengine..
 
AKINYI MUST DIE (NI LAZIMA AKINYI AFE) - 01


Mvua kubwa iliyoambatana na ngurumo,radi na upepo mkali zilikuwa zikilindima Kaskazini mashariki mwa Tanzania katika jiji la Mwanza,maeneo ya Buswelu.Ilikuwa ni mvua kubwa kiasi kwamba kila raia alishitushwa na namna mvua ile ilivyokuwa ya kuogofya kwasababu haikuwahi kutokea mvua kubwa kama ile kwa miaka ya karibuni!

"Mama Deoooooooo....!,mama deoooooo....!,jamani mama deo njoo uone!"

Ilisikika sauti ya mwanamke mmoja aliyekuwa akikinga maji ya mvua akimuita mwenzie.

Mama deo " Jamani Jeny kuna nini?"

Jeny " Hebu tizama!"

Mama deo " Nitizame nini!?"

Mama deo " Aahh jamani,mbona wanawake wanakuwa katili na wenye roho mbaya kiasi hiki!"

Aliendelea " Huyu si mtoto?"

Jeny " Ndiyo maana nimekuita mwenzangu uje uangalie maana nimeshituka kukiona hichi kichanga"

Mama deo " Aliyekiweka hapa nani?"

Jeny " Mimi sijui,nilipotoka nje kukinga maji nimekuta kimenyeshewa halafu kinalia"

Mama deo " Hebu ingia ndani kwangu niletee kitenge changu kipo nyuma ya mlango"

Alikuwa ni mtoto kichanga ambaye alikuwa ametelekezwa kando ya nyumba ya mzee Masumbuko ambako kwa muda huo Jeny na mama Deo walikuwa miongoni mwa wapangaji,haikujulikana ni nani alimtelekeza mtoto huyo na kwanini alifanya hivyo.

Mama Deo " Jamani halafu kazuri!"

Aliendelea kusema " Ngoja nimsubiri Baba deo akirudi twende kwa mjumbe tukaripoti"

Haikuchukua muda Baba deo aliporudi kutoka kwenye mihangaiko yake ya kila siku,mke wake alimueleza kila kitu kuhusu kichanga kile na walishauriana kwa jioni hiyo kuelekea kwa mjumbe ili kutoa taarifa.

Kwakuwa mama deo alikuwa na mtoto mmoja wa kiume ambaye ni deo,alimueleza mjumbe kwamba angekaa na huyo mtoto kama binti yake na angemlea,na endapo mzazi wake angepatikana basi wangemrejeshea.
Mpaka wakati huo hakuna aliyekuwa akifahamu mama wa kichanga hicho ni nani na kwanini ametelekeza mwanaye!.Mjumbe alimruhusu mama deo amchukue yule kichanga na endapo kungetokea sintofahamu basi ilipaswa wampe taarifa mjumbe.

Ilipofika usiku wa saa 3 mvua ikiwa imekata,basi ilisikika sauti ya bwana mmoja ambaye kwa namna alivyokuwa akiongea hapana shaka ungefahamu alikuwa amelewa chakali.

Mlevi "Nyieee watu wa nyumba hii,nifungulieni mlango"

Aliendelea kugonga mlango wa ile nyumba huku akitukana matusi ya nguoni.

Aliendelea "Nyie nguruwee,fungua mlango haraka"

Haikuchukua muda mlango wa nyumba ulifunguliwa na mmoja wa wapangaji wa ile nyumba!

Jamaa mpangaji "Unasemaje?"

Mlevi "Wewe ni nani?"

Jamaa mpangaji "Nimekuuliza unasemaje?"

Mlevi "Nataka mtoto wangu"

Jamaa mpangaji "Mtoto wako?,mtoto wako yupi?"

Sasa wakati wanajibishana pale mlangoni,Baba deo alifungua mlango wa chumba chake maana ilikuwa usiku na kelele zilimshitua.

Baba Deo "Alex mambo vipi,mbona kuna kelele?"

Alex "Huyu jamaa sijui katokea wapi,halafu kalewa kishenzi!"

Baba Deo "Anasemaje?"

Alex "Hebu njoo umsikilize"

Baba deo alisogea mpaka pale mlangoni na kutaka kufahamu ni nini kilikuwa kikiendelea.

Baba Deo aliuliza "We mzee unasemaje?,mbona unasumbua watu wamelala?"

Mlevi "Nahitaji mtoto wangu"

Yule Jamaa aliyekuwa amelewa alikuwa mtu mzima wa makamo na aliendelea kusema kwa sauti ya ulevi.

Baba Deo "Hebu ondoka hapa umelewa"

Japo alikuwa amelewa lakini alionekana kumaanisha alichokuwa akizungumza!.

Mlevi "Nimesema nataka mwananguuuu!"

Yule mzee alibwata kwa ukali kidogo mpaka wapangaji wa vyumba vingine ilibidi waamke kuja kutazama ni nini kilikuwa kikiendelea.Baada ya jamaa kuwa mkali na kukomalia mlangoni,Baba deo alitaka kufahamu na kumsikiliza yule jamaa kwa makini.

Baba Deo "Mwanao yupi unaye mtaka?"

Jamaa baada ya kuona wapangaji wengine wametoka nje kuja kuona ni mtu gani aliyekuwa akiwapigia kelele usiku huo,ilibidi awasimulie namna ilivyokuwa.

Mlevi " Wakati natoka kwa mama Ntalama kunywa pombe,nilipita uchochoroni kukojoa,wakati nakojoa ghafla nilisikia mtoto analia alikuwa kwenye sandarusi"

Aliendelea kusema " Ilibidi nisogee kufunua ili nione kulikuwa na nini,nilipofungua nikakuta ni mtoto mchanga analia,sasa kwakuwa mvua ilikuwa inataka kunyesha nikambeba na kuondoka nae,sasa mimi nakumbuka nilimuweka hapa nje,hivyo naombeni mtoto wangu"

Baada ya kusimulia kisa chote namna ilivyokuwa,kila mtu pale ndani alishangaa.

Baba Deo "Sasa wewe ulimuacha hapa wewe ukaenda wapi?"

Mlevi "Nisingeweza kupanda kule juu ninapoishi na yule mtoto kwakuwa nilikuwa nimelewa,nilimuacha hapa ili niende kwa mama Kichikutula kumwambia aje amchukue mtoto"

Baba Deo "Huyo mama Kichikutula ni nani?"

Mlevi "Ni mpenzi wangu"

Mama deo " Sasa kama wewe ndiye ulimuweka hapa huyo mtoto,kwanini ulimuacha hapa na hiyo mvua au ulitaka afe halafu tupewe mada kesi?"

Mlevi " Wakati nipo kwa mama Kichikutula mvua ilianza kunyesha na sikuweza kutelemka tena huku chini kwasababu mvua ilikuwa kubwa"

Jamaa aliongea kwa kujiamini kulikosindikizwa na sauti ya kilevi yenye dharau na jeuri ya kutosha.Kwakuwa ile familia ya mama deo haikutaka makuu ilibidi wamueleze kwamba yule mtoto walimchukua na wamesharipoti kwa mjumbe na kama ikiwezekana yeye akapumzike pombe zimuishe kichwani na kesho yake wangeamkia kwa mjumbe tena!.Kila mtu alitaka kufahamu mama wa yule mtoto ni nani na kwa nini alimtelekeza mwanaye aliyekuwa binti mzuri asiyekuwa na hatia.

Asubuhi na mapema yule jamaa aliyekuwa Mlevi ule Usiku na mpenzi wake aliyekuwa akiitwa mama Kichikutula walidamkia pale kwenye nyumba ya mzee Masumbuko ili kuangalia uwezekano wa kumpata yule mtoto.Waliondoka wakaongozana wote pamoja na mtoto kuelekea kwa mjumbe wa mtaa.Walipofika kwa mjumbe walieleza namna ilivyokuwa,mjumbe alishauri kulikuwa na ulazima wa kwenda polisi ili taratibu nyingine za kisheria zifuate mkondo.Hawakuchukua muda wakaondoka kuelekea kituo cha Polisi cha Nyakato ili taratibu za kipolisi zichukue nafasi.

Baada ya kuchukuliwa maelezo muda mrefu,polisi walishauri yule mtoto aendelee kutunzwa na mama Deo huku wakiendelea na upelelezi wa kujua mama wa mtoto ni nani na kwanini alitupa mtoto wake!.Polisi walisema upepelezi ungechukua muda wa siku kadhaa na ikiwa ungekamilika wangejulishwa.Polisi walisema yule jamaa aliyemuokota mtoto wangebaki nae kwa masaa kadhaa kwa ajili ya mahojiano na kisha wangemruhusu aondoke.

Siku 72 zilitosha kabisa kwa maafisa upelelezi wa Jeshi la polisi kitengo cha makosa ya jinai kutoka kituo kikuu cha polisi Jijini Mwanza kukamilisha upelelezi na uchunguzi wa uhalifu wa kutelekezwa kwa binti mchanga aliyetupwa na mama yake katika kata ya Buswelu,wilaya ya Ilemela,jijini Mwanza,Tanzania.

Mwenyekiti "Nimepokea wito kutoka kituo cha Polisi cha wilaya,nami nimewaiteni yatupasa tuongozane".

Ilikuwa ni sauti ya Mwenyekiti wa mtaa wa Bulola "A" aliyekuwa akiwapa taarifa mjumbe wa eneo husika pamoja na wahusika akiwemo mama Deo na yule jamaa aliyemuokota mtoto.

Hawakutaka kupoteza muda waliongozana kwa pamoja mpaka kituo cha polisi wilaya ya Ilemela.

Afande "Jina langu ni Cosmas Mchumajanga ,nina Cheo cha Constable wa Polisi pia ni mpelelezi wa makosa ya Jinai katika Kanda ya kipolisi ya Wilaya ya Ilemela pamoja na Nyamagana"

Aliendelea "Wewe uliyemuokota mtoto Ndiye Stephano?"

Jamaa aliyemuokota mtoto "Ndiyo afande,ni mimi"

Afande Cosmas " Ok,hebu kaa hapo"

Afande Cosmas "Sasa kulingana na upelelezi uliyofanywa na askari wetu mahiri,unaonyesha mama wa mtoto alifariki siku ileile ambayo wewe ulimukota yule mtoto,nadhani hapo awali unakumbuka tulikujoji na ukatoa ushirikiano"

Stephano "Ndiyo afande"

Afande Cosmas "Taarifa nilizopokea mpaka sasa hivi kwenye kabrasha zangu hizi nikiwa kama mkuu wa kitengo cha upelelezi kituoni hapa ni kwamba,yule mwanamke alikuwa na watoto mapacha,mtoto mmoja hajulikani alipo,bado tunaendelea kufuatilia kwa karibu na hivi karibuni tutapata taatifa rasmi"

Mwenyekiti wa Mtaa "Kwahiyo afande waharifu wa mauaji wamekamtwa?"

Afande Cosmas "Hapana,ila bado askari wangu wanaendelea kufuatilia kwa ukaribu,unajua baada ya upelelezi inaonekana yule mwanamke alikuwa ametekwa,sasa watu tuliyowahoji kwenye maeneo husika wanasema lile eneo ambalo huyu bwana Stephano alilomuokota yule mtoto,walikuja watu wakiwa wamevaa vinyago (mask) usoni wakiwa wawili akiwemo na mwanamke mmoja ambaye yeye hakuvaa kinyago,sasa wanasema baada ya kushuka kwenye gari aina ya Prado lisilokuwa na namba za usajili walimshusha mwanamke mmoja aliyekuwa na watoto wadogo wakaanza kumpiga,na namna alivyokuwa dhaifu inasemekana walianza kumpiga kabla ya kuletwa pale"


Afande Cosmas aliendelea "Sasa nadhani wale jamaa walipoona watu wameanza kuwa wengi wakishangaa kilichokuwa kikiendelea wakamchukua yule mama wakampakia kwenye gari wakaondoka naye,nadhani lengo lao ilikuwa kumuua yeye na watoto wake, nadhani wakati wanaondoka hawakujali kwamba kuna mtoto mmoja wa yule mwanamke walimuacha pale chini na lengo lao walidhani angekufa lakini kama mjuavyo ya Mungu huwa ni mengi "

Mama Deo "Kwahiyo afande yule mtoto mwingine hajapatikana?"

Afande Cosmas "Kiukweli yule mtoto hatujampata,ila kama nilivyosema bado askari wangu mahiri wanaendelea kulifuatilia hili tukio kwa ukaribu na kila kitu kitaenda sawa,naomba tu mnipe ushirikiano wenu kila ninapowahitaji"

Mwenyekiti wa Mtaa "Kwahiyo Afande yule mwanamke ndugu zake wameuchukua mwili wake?"

Afande Cosmas "Hapana,kwa namna alivyokuwa ameharibika imebidi jeshi la Polisi kwa kushirikiana na manispaa wameona iwe busara kuuhifadhi ule mwili,unajua mwili wenyewe sisi tuliukuta kule Nyashishi,kiukweli ulikuwa umeharibika sana,hao washenzi tutawapata tu maana mkono wa serikali ni mrefu na lazima sheria itachukua mkondo wake,wala msiwe na hofu"

Mama Deo "Ni kweli huyo mwanamke ndiye mama wa huyu mtoto afande?"

Afande Cosmas "Sisi tuna mkono mrefu sana na tumehakikisha ndiye,siwezi kusema hapa kila kitu ila kwa taarifa za kiiterejensia siwezi kueleza tumepata wapi taarifa,kama nilivyosema msiwe na wasiwasi nyie subirini tu mtaona namna jeshi lenu linavyofanya kazi kwa weledi na umakini mkubwa"

Afande Cosmas aliendelea "Basi sawa,nyie kaendeleeni na shughuli zenu na tutakapowahitaji nadhani tutawajulisha ili mtupatie ushirikiano"

Haikuwa siku nzuri sana kwa mama deo maana kama mwanamke alikuwa na kila sababu ya masikitiko.

Mama Deo "Daaah!,kuna watu wana roho mbaya kama shetani"

Mjumbe wa mtaa "Wala hata usijali shemeji watajulikana tu,hii serikali iko makini"


Waliianza safari ya kurejea makwao asubuhi hiyo,njiani kila mtu alikuwa akisema lake ilimradi tu kunogesha maongezi.

Kadiri siku zilivyosonga ilimlazimu mama deo kumlea yule binti kama mwanae.


Itaendelea ..............
@UMUGHAKA in da house.....karibu tena kwa story yenye mafunzo
 
Back
Top Bottom