Ngida1
JF-Expert Member
- Aug 25, 2009
- 586
- 206
Kila siku saa 12.00 asubuhi, mwanafunzi wa darasa la kwanza wa Shule ya Msingi Hananasif, Abdallah Mkwama huamka na kujiandaa kwenda shule.
Maisha yake ni ya kusikitisha. Hayafanani na wanafunzi wenzake wengi.
Anaishi kwenye kibanda cha mabati kilichojengwa juu ya kifusi cha iliyokuwa nyumba yao ambayo ilikumbwa na bomoabomoa katika Bonde la Mto Msimbazi, jijini Dar es Salaam.
Mwanafunzi huyo hulala kwenye godoro chakavu lililojaa vumbi. Mbu na wadudu wengine imekuwa sehemu ya maisha yake.
Hana uhakika wa kupata chai, chakula cha mchana wala jioni, ingawa mama yake hujitahidi kuhakikisha mtoto huyo hakosi masomo wala chakula, walau kidogo.
“Nalala juu ya kifusi, naamka hapo kwenda shule, Najisikia vibaya kulala hapa, usiku kucha mbu wananiuma, sina raha hata kidogo. Nikikumbuka mama yangu hana uwezo wa kutuhamishia sehemu nyingine kwa kukosa pesa, huruma na huzuni hunijaa lakini navumilia tu,” anasema Abdallah.
Operesheni ya kubomoa nyumba zilizojengwa mabondeni, kando ya mito na fukwe za bahari ya Hindi ilianza kutekelezwa Desemba mwaka jana, hadi sasa zaidi ya nyumba 700 zimevunjwa.
Awali ilikadiriwa kuwa zaidi ya nyumba 8,000 zingevunjwa jijini Dar es Salaam chini ya operesheni hiyo inayoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) na halmashauri za manispaa za Jiji la Dar es Salaam, lakini baadaye walipoanza kuweka alama ya X ziliongezeka hadi kufikia zaidi ya 15,000.
Baadhi ya wananchi waliokumbwa na operesheni hiyo hawana mahali pa kwenda hivyo kulazimika kuanza maisha mapya juu ya vifusi vya vyumba zao zilizovunjwa.
Hali imekuwa mbaya zaidi kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, hata wajawazito.
Maisha ya Abdallah
Kwa Abdallah ni kama bahati mbaya. Ameanza masomo yake ya darasa la kwanza mwaka huu wakati familia yake ikikosa mahali pa kuishi.
Licha ya kuishi kwenye mazingira magumu yanayohatarisha afya yake, Abdalah hajawahi kukosa masomo yake tangu shule zilizpofunguliwa mapema wiki iliyopita.
Kwake si hoja kama siku hiyo mama yake atafanikiwa kumuandalia chai ya asubuhi au hapana, kila akiamka ratiba yake hubaki pale pale, hujiandaa na kwenda shule.
“Siku nyingine mama huwa hana hela za kununulia sukari wala kitafunwa, nikijua hivyo huwa nakwenda na njaa, lakini nikirudi mchana nakuta ameniwekea vitumbua,” anasema Abdallah.
Mama wa mtoto huyo, Stamily Samata anasema awali hakutaka Abdallah aanze darasa la kwanza baada ya nyumba yao kubomolewa na kukosa mahali pa kuishi, lakini mwenyewe alipinga na kusisitiza lazima aende shule.
Anasema Abdallah kila alipokumbuka kuhusu kuanza darasa la kwanza, aliomba anunuliwe vifaa na sare ili shule ikifunguliwa aanze masomo yake.
“Baada ya kubomolewa nyumba, nilitaka aanze darasa la kwanza mwaka ujao kwa sababu hapa nilipo sijui kesho kitatokea nini, maisha yangu ni magumu kuliko kawaida, lakini mtoto hakutaka kunisikiliza, akalazimisha nimpeleke shuleni basi nikampeleka,” anasema Stamily.
Dada wa mtoto huyo, Tausi Mkwama anayesoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Hananasif analalamikia ugumu wa maisha unaoikabili familia yao tangu walipokumbwa na bomoabomoa.
Hata hivyo, Tausi anajipa moyo akisema hali hiyo haitakuwa chanzo kwa wao kukatisha masomo.
“Kila siku nikiamka namsaidia mdogo wangu, huwa tunaenda wote shuleni. Kuna wakati nikikaa darasani machozi hunitoka, nakumbuka siku nyumba yetu ilivyovunjwa na maisha haya tunayoishi sasa,” anasema Tausi.
Anasema maisha yao ya awali hayakuwa mabaya na kwamba familia hiyo ilimudu gharama zote ikiwamo chakula, mavazi, elimu na vitu vingine muhimu.
Vifaa vya shule vya Abdallah
Stamily anasema kwa kuwa Abdalah alisisitiza kuanza masomo yake licha ya kukosa pa kuishi, yeye alilazimika kukopa fedha kwa ajili ya kununulia mahitaji ya shule.
“Nilikuwa na Sh 25,000, nikamnunulia sare za shule, viatu, soksi na daftari. Sijaweza kulipia muhuri kwenye shati lake la shule, lakini hiyo haitaathiri usomaji wake kwa sasa,” anasema Stamily.
Wanafunzi wengine
Wakati baadhi ya watoto wakijitahidi kwenda shule licha ya mazingira magumu yanayowakabili, wapo ambao wameshindwa kutokana na familia zao kukumbwa na bomoabomoa hivyo kukosa mwelekeo kwani wazazi wao hawana fedha za kumudu kuwapatia mahitaji ya shule.
Mmoja wa wanafunzi hao, Maua Juma anayetarajia kuingia darasa la saba katika Shule ya Msingi Mkunguni, anasema tangu nyumba yao ilipobomolewa na vifaa vyao kuibiwa hajui hatma yake kielimu.
Yeye na wadogo zake hawajaanza kwenda shule baada ya mama yao kukosa fedha za kuwanunulia vifaa vya shule.
“Hatuna madaftari, sare za shule ziliibiwa na wala mama hana pesa. Ametuambia tusubiri, labda tunaweza kuanza masomo wiki ijayo. Kila kitu kilivurugwa siku walipobomoa nyumba yetu, hatukubakiwa na chochote,” anasema.
Mwandishi wa makala haya alikutana na maua nje ya kibanda chao cha mabati, kando ya eneo lenye maji machafu akiwa amejiinamia.
Mwanafunzi mwingine wa Shule ya Sekondari Msimbazi, Idrisa Jacob anasema hana uhakika wa kuendelea na masomo yake kutokana na ugumu wa maisha unaoikabili familia yake baada ya kubomoewa nyumba zao.
Mazingira ya eneo hilo
Wanafunzi wengi wanasema hali ya afya zao ipo hatarini kutokana na kulala nje, juu ya vifusi bila kuwa na neti baada ya nyumba zao kubomolewa.
Mbali na hofu ya kukubwa na malaria, afya za watoto wengi wanaoishi kwenye bonde hilo baada ya nyumba kubomolewa, zipo hatarini kutokana na kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kikiwamo kipindupindu.
“Hakuna maji safi wala vyoo vya uhakika, tunahangaika na hatujui nini hatima yetu. Tupo hatarini kuugua malaria, kipindupindu na magonjwa mengine yanayotokana na uchafu uliopo hapa,” anasema Jacob.
Maombi kwa Serikali
Wanafunzi hao wanaiomba Serikali kuwasaidia wazazi wao makazi ya kudumu, ili wawe na uhakika wa kusoma katika shule watakazohamia.
“Inawezekana wazazi wetu wameikosea Serikali kiasi cha kupewa adhabu hii kali inayotugusa hata sisi watoto, lakini najua inaweza kutusaidia. Najua ina fedha za kutunza watu wake, najua hatuna thamani wala hadhi ya kuhudumiwa lakini, ituhurumie. Itusaidie, tunaumia na maisha haya yameshatuchosha,” anasema Jacob.
Mjumbe alonga
Mjumbe wa Shina la Kawawa (CCM), ambaye pia ni mjumbe Serikali ya mtaa huo, Erasto Mayani anakiri hali ngumu kwa watoto na wanafunzi wanaoishi eneo hilo.
Anasema wapo ambao hawataweza kuendelea na masomo ikiwa hawatapata msaada wowote wa kibinadamu ikiwamo makazi salama na chakula.
“Tangu tupate dhoruba hii hatujawahi kusaidiwa chochote na Serikali. Tunahitaji chakula na uhakika wa makazi. Hali hii inasababisha baadhi ya wanafunzi hasa kutoka familia duni washindwe kuendelea na masomo,” anasema Mayani na kuongeza:
“Wazazi hawana mwelekeo, wamepoteza mali na fedha zao, hawawezi kusimamia masomo ya watoto. Maisha yetu tangu tubomolewe yamejaa kila aina ya shida.”
Takwimu kwenye eneo lake zinaonyesha kuwa zaidi ya wanafunzi 70 wa shule za msingi na sekondari waliotakiwa kuanza au kuendelea na masomo yao, bado hawajaripoti tangu shule zifunguliwe.
Wazazi walonga
Kwa upande wao wazazi, wanasema hawajui hatma ya watoto wao baada ya kupoteza mwelekeo wa maisha kutokana na bomoabomoa hiyo.
Mama wa watoto wanne, wawili wakiwa sekondari na mwingine mwanafunzi wa shule ya msingi, Fatuma Ismail anasema tangu alipobomolewa nyumba yake, hajui pa kwenda wala hatma ya watoto wake kielimu kwa kuwa hadi sasa hawajaanza shule.
“Siyo rahisi mtoto kuishi mazingira haya ukategemea ataweza kwenda shule na kurudi, hiyo elimu bure inawahusu watoto wa wenzetu siyo hawa wetu,” anasema Fatuma.
“Binafsi naishi kwa kuombaomba, ninachoangalia sasa ni watoto wapate mlo kwanza,” anasema.
Ofisa elimu
Licha ya Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mapunda kueleza ni wajibu idara yake kisheria kuhakikisha wanawasaidia wanafunzi wanaopata dharura bila kujali madarasa wanayosoma, lakini bado hakuna mpango wowote wa kuwasaidia wanafunzi kutoka familia zilizokumbwa na bomoabomoa hiyo.
Akitoa muda kwa wananchi ambao hawajabomolewa kuondoka, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi anasema ujenzi katika eneo la Bonde la Mto Msimbazi ni hatari na kinyume na Sheria ya Mipango Miji.
Chanzo: Mwananchi