Zitto amesema kiongozi yeyote ambaye hatengenezi mrithi wake, basi huyo ni kiongozi ambaye amefeli. Anasema tayari chama chake kimetengeneza vijana wengi wenye uwezo wa kuongozi hata yeye asipokuwepo.
“Muda wangu wa uongozi unakwisha Machi 30, 2024. Kama hatujengi watu wa kutosha, nani atakuja kuwa kiongozi? Lakini kwa sababu Watanzania wamezoea ukiwa kiongozi wa chama cha upinzani, wewe ni wa kudumu, hilo ni jambo la ajabu sana.
“Mimi kama kiongozi ninasema hapana, nimetumia muda wangu kwa mujibu wa katiba yetu, wa miaka 10 na actually (hakika) nimerudisha nyuma kwa sababu ilikuwa nimalize mwaka 2025, nimesema hapana, hatuwezi kubadilisha uongozi mwaka wa uchaguzi, turudi nyuma tufanye mwaka 2024,” anasema.
Alisema Machi 2024, watakuwa na kiongozi mwingine wa ACT Wazalendo na kwamba jopo la viongozi kivuli linawapa machaguo ya kwenda kusema fulani anafaa, na hilo analiona kuwa la muhimu zaidi kwenye siasa.
Zitto anabainisha kwamba amekuwa akijizuia kusema ili kuwapa nafasi viongozi wengine kusema kupitia wizara wanazozisimamia katika baraza kivuli la chama hicho. Anasema kupitia hilo, viongozi wengine wanajulikana na kupata ujasiri wa kufanya siasa.
“Tuna watu ambao wana uwezo mkubwa. Ukiangalia reaction ya wanasiasa kwenye suala la Loliondo, ukilinganisha na wanasiasa wa vyama vingine na siasa ambayo Bonifasia Mapunda aliifanya kwenye suala la Loliondo, unaona tofauti kwa sababu sisi kuna vijana wanafanya utafiti na kulifahamu jambo,” anasema kiongozi huyo.
Mwanasiasa huyo ambaye alikuwa mbunge wa Kigoma Mjini, anawataka wanahabari kuwapa nafasi viongozi wao ili waweze kutetea masilahi ya Taifa kupitia baraza kivuli ambalo limeundwa na ACT kuziba pengo la kukosekana kwa baraza kivuli bungeni.
Likiwepo la kusema nitasema
Zitto alikuwa mkosoaji mkubwa wa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli na kila lilipotokea jambo hakusita kujitokeza na kukemea vikali jambo hilo hadharani na kuitaka Serikali kuchukua hatua.
Baada ya Rais Samia kuingia madarakani, Zitto amepunguza ukosoaji kama alivyokuwa huko nyuma, jambo ambalo limekuwa likiibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii ambapo watu wamekuwa na mapokeo tofauti.
Hata hivyo, yeye anaeleza kwamba kama kuna jambo lolote lenye masilahi mapana kwa umma, lazima aingie. Anasema pale panapohitajika kusema atasema kama kiongozi wa ACT Wazalendo.
“Moja ya mambo ambayo nilikuwa kinara wakati wa utawala wa Magufuli ilikuwa ni kutetea watu, watu wanaotekwa. Ndiyo maana mlisikia namzungumzia Ben Saanane, Simon Kanguye, Erick Kabendera nje na ndani ya Bunge.
“Sasa, mnataka niseme vile, nionyeshe nani katekwa, sema fulani ametekwa hukusema, biashara fulani imevunjwa hukusema, mwandishi wa habari fulani amekamatwa hukusema. Kila msimu una shughuli zake.
“Msimu wa kushangilia, wewe ukizomea, watu watakuona juha. Msimu wa kushangilia, wewe ukizomea watu watakuona zwazwa. Msimu wa Rais Magufuli ulikuwa ni msimu wa kuhami demokrasia, angalau zibakie sauti chache za kupigania demokrasia,” anasema Zitto.
Anaongeza kwamba msimu wa Rais Samia ni msimu wa kusimamia mageuzi yanayotakiwa katika nchi ili angalau nchi irudi katika mazingira yaliyokuwepo kabla ya mwaka 2015. Alisisitiza kwamba misimu hiyo miwili ni tofauti.
MWANANCHI