Habari kamili....
Zitto awalipua Wazungu
11th December 2012
*Ni uporaji wa
matrilioni
Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto
Kabwe, amewalipua Wazungu kuwa ni waporaji wakubwa wa rasilimali za
Afrika.
Pia ameitaja Uswisi moja kwa moja kwa moja kuwa inakumbatia sera
ambazo zinasaidia uporaji wa rasilimali hizo kwa kuweka vivutio vya kutokulipa
kodi na taratibu ngumu na zisizo wazi katika kufuatilia fedha zilizoporwa katika
mataifa ya Afrika.
Alisema uporaji huo kwa kiasi kikubwa unaziumiza zaidi
nchi nyingi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa njia ya ukwepaji
kodi, rushwa na hila nyingine katika sekta ya uwekezaji.
Zitto ambaye ni
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, alisema hayo wakati akihutubia mkutano wa masuala ya
ushirikiano wa uchumi kati ya Ujerumani na nchi za Afrika.
Mkutano huo wa
siku tatu mfululizo, kuanzia Desemba 9, mwaka huu, unafanyika mjini Berlin,
nchini Ujerumani.
Zitto anatoa kauli hiyo wakati kukiwa na harakati kubwa
nchini za kutaka Watanzania walioficha zaidi ya Dola bilioni 300 katika mabenki
ya Uswisi wawajibishwe ikiwa ni pamoja na kurejeshwa kwa fedha hizo
nchini.
Miongoni mwa watu wanaodaiwa kuficha fedha hizo Uswisi ni pamoja
na watumishi wa umma na viongozi waandamizi.
Katika mkutano wa jana,
Zitto alisema kuwa nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikiporwa maliasili zake na
baadhi ya kampuni za kimataifa kupitia ukwepaji kodi pindi zinapokuja kuwekeza
barani humo.
Zitto alisema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwaka 2012
katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (Unctad), jumla ya
uwekezaji wote uliofanyika duniani kwa mwaka jana ni trilioni 1.5 (Dola moja ni
sawa na Sh. 1,568) lakini kiasi cha fedha kilichotoroshwa kutoka nchi
zinazoendelea kwa mwaka ni wastani wa Dola za Marekani trilioni 0.84 kati yake
Dola trilioni 0.58 zilitoroshwa kutoka Afrika Kusini mwa Jangwa la
Sahara.
Kibaya zidi Zitto alisema wakati kiasi cha Dola za Marekani
bilioni 538 zinaibwa kutoka Afrika kwa nji za rushwa, ukwepaji wa kodi na mbinu
za kutokulipa kodi, ni kiasi cha Dola za Marekani bilioni 80 tu kinaingizwa
barani humo kama uwekezaji wa moja kwa moja na misaada.
"Kwa kila Dola
moja inayokuja Afrika, Dola nyingine saba zinatoroshwa kutoka Afrika kupitia
njia haramu! Hii haikubaliki," alisema Zitto katika mkutano huo unaozungmzia
pia jinsi kampuni zinavyowajibika kwa jamii kwa kurejesha kila
wanachochuma.
Alishauri kuwa uporaji huo ni lazima uzungumziwe kama moja
ya ajenda za ushirikiano wa maendeleo baina ya mataifa ya Afrika na
yaliyoendelea.
Alisema kwa mujibu wa taarifa kuhusu uadilifu wa matumizi
ya fedha duniani ya mwaka jana, kati ya mwaka 2000 hadi 2010, zaidi ya Shilingi
trilioni 1,331.8 (Dola za Marekani bilioni 844) ziliporwa kwa mwaka kutoka nchi
zinazoendelea kati yake ya fedha hizo, asilimia 69 zilichukuliwa kutoka nchi za
Afrika.
Kwa mfano, Zitto aliuambia mkutano huo nchi kama Uswisi na
nyinginezo zenye misamaha ya kodi, zinasaidia sera zake kufanikisha utoroshaji
wa fedha kutoka mataifa masikini ya Afrika na pia zinaweka taratibu ngumu za
uwazi juu ya fedha hizo hali aliyosema inasaidia kuongeza umasikini
Afrika.
Alitaka mataifa rafiki kama Ujerumani kusaidia mataifa ya Afrika
katika juhudi za kukataa uporaji unaofanywa na mataifa yenye sera kama za
Uswisi.
Zitto aliuambia mkutano huo kwamba Tanzania inaongoza kupokea
misaada kutoka nje baada ya Iraq na Afghanistan, lakini bado zaidi ya theluthi
moja ya watu wake wanataabika katika umasikini.
"Hali ni hiyo hiyo katika
nchi nyingi za Afrika. Mageuzi ya Ushirikiano wa Maendeleo ni yale ya
kuwawezesha watu kuamua hatima yao wenyewe," alisema.
Huku akiitaka
Ujerumani kuwa mdau na mshirika wa kusaidia mabadiliko ya kimahusiano ya
uwekezaji ili mataifa ya Afrika yaamue kuhusu hatma yake yenyewe, alimnukuu
hayati Mwalimu Julius Nyerere katika kitabu chake cha Uhuru na Maendeleo
akisema:
"Mtu ajiendeleze mwenyewe akikua au akipata kipato cha
kujitosheleza na kutunza familia yake. Atakuwa hajaendelea kama atapatiwa vitu
hivi na mtu mwingine."
CHANZO: NIPASHE