MEI mwaka 2003 tukiwa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam tulitembelewa na
mgeni kutoka Chama cha SWAPO
cha Namibia. Wakati huo nchini
Namibia (na Afrika kwa ujumla)
kulikuwa kuna mjadala kuhusu
kubadili katiba ya nchi hiyo ili
kumruhusu Rais Sam Nujoma
kugombea kipindi cha tatu.
Mgeni huyu alikuwa Katibu Mkuu wa
Umoja wa Vijana wa SWAPO na
alialikwa na vijana wa CCM pale
Mlimani, kina Wilman Kapenjama na
Martin Shigella. Walimleta kwenye
moja ya kumbi za semina ili kufanya
mjadala kuhusu Afrika. Nilimuuliza
swali kwamba msimamo wake nini
kuhusu mabadiliko ya Katiba ya
Namibia ili kumwezesha Nujoma
kugombea kipindi cha tatu cha urais.
Akanijibu kwamba wao vijana wa
SWAPO wanaunga mkono lolote
ambalo Sam Nujoma atataka! Mmoja
wa washirika wa mkutano ule Kitila
Mkumbo, alisimama na kumwambia
kijana yule hupaswi kufuata mtu,
fuata misingi. Alitoa kauli hii kwa
ukali kidogo. Nadhani ndiyo maana
bado ni kauli ambayo imenikaa
mpaka hivi sasa.
Hivi sasa hapa nchini kumezuka
wimbi la wanasiasa kuwa na
makambi ambayo yanatokana na
ufuasi kwa mtu au kiongozi wa kambi
husika badala ya ufuasi kwa misingi
ya chama cha siasa au basi angalau
misingi ya kambi husika ya chama
hicho. Makambi ni utamaduni ambao
umeshamiri zaidi ndani ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) ingawa hata
vyama vya upinzani sasa vimeingia
kwenye mtego huo hatari sana kwa
demokrasia.
Huu ni mfululizo wa makala sita,
zitakazokuwa zinaelezea misingi
mbalimbali ya chama ambacho mimi
ni mwanachama, CHADEMA, na
namna ambavyo viongozi mbalimbali
wa chama hicho wamekuwa
wakisimamia kwa vitendo misingi
hiyo. Makala hizi zitakuwa zinatoka
kila wiki ya mwisho ya mwezi katika
kipindi cha nusu ya kwanza cha
mwaka 2013. Chama cha siasa ni
jumuiko la watu wenye nia moja na
lengo moja la kisiasa.
Ni mchanganyiko wa watu wenye
kuunganishwa na misingi fulani.
Misingi hii inapokosekana au
kupondwapondwa basi uwepo wa
jumuiko hilo linaloitwachama cha
siasa unakuwa shakani. Kwa kutolea
mfano wa chama changu, CHADEMA,
ni chama cha siasa ambacho tangu
kuanzishwa kwake kimekuwa wazi
kabisa kuhusu misingi yake
inayosimamia. Iwapo wana
CHADEMA watashindwa kuheshimu
misingi ya chama basi uhai wa
chama hicho utakuwa shakani na
hatimaye hata uhai wa mfumo imara
wa vyama vingi nchini Tanzania.
CHADEMA sasa imejijenga kama
chama cha siasa kinachopinga
ufisadi, kinachosimamia uwajibikaji
na uwazi katika uendeshaji wa
serikali, kinachopigania siasa za
ukweli, kinachotetea haki za raia
haki za kuishi na kushiriki siasa,
kinachotetea rasilimali za nchi.
Katika katiba ya chama hicho kuna
misingi 12 ambayo chama
kimejengwa juu yake. Iwapo
wanachama wake watasimamia kwa
dhati misingi hii badala ya kusimamia
watu, kamwe hapawezi kutokea
malumbano yasiyo na msingi
yanayopoteza malengo ya ukombozi
mpya kwa Mtanzania. Inasikitisha
sana hivi sasa kwenye siasa za
Tanzania, kwa vyama vyote vya
siasa, kumekuwa na ufuasi wa watu
badala ya ufuasi wa misingi.
Watu si mawe, hugeuka. Misingi
inabaki misingi. Ama unafuata
misingi hiyo au unajiunga na chama
kinachofuata misingi unayoitaka, au
unaanzisha misingi mingine katika
chama kipya. Ufuasi wa mtu kwenye
chama cha siasa unapaswa
kuangaliwa kwa ufuasi kwa misingi
inayojenga chama hicho. Ufuasi wa
kiongozi wa CHADEMA unapaswa
kupimwa kwa kuangalia ni namna
gani kiongozi huyo anatekeleza kwa
vitendo misingi ya chama iliyotajwa
hapo juu (kupinga ufisadi, kusimamia
uwajibikaji).
Uadilifu wa mwanachama wa chama
hicho utapimwa si kwa uaminifu kwa
kiongozi au mwanachama mwingine
wa chama au kikundi cha
wanachama, bali kwa uaminifu na
utekelezaji wake wa misingi ya
chama. Kiongozi au mwanachama
atakuwa ni msaliti iwapo anakwenda
kinyume cha misingi ya chama.
CHADEMA imejipambanua wazi wazi
katika utetezi wa rasilimali za taifa,
kwamba utajiri wa nchi uwe ni ardhi,
madini, misitu, maji, gesi asilia
vinatumika kwa maendeleo ya
Watanzania na si kwa kikundi cha
watu wachache. Hata masuala ya
rasilimali fedha pia imekuwa mstari
wa mbele kama chama kisichotaka
mchezo kabisa na kutapanywa kwa
mali za taifa.
Katika miaka ya hivi karibuni
kumekuwa kuna malalamiko
makubwa ya wananchi kuhusu
uporaji wa ardhi, migogoro ya ardhi
kati ya wafugaji na wakulima na kati
ya wanavijiji na wawekezaji.
Malalamiko haya yalikuwa
yanaandikwa na vyombo mbalimbali
vya habari vya hapa nchini na hata
nje ya nchi. Katika Bonde la Mto Rufiji
maelfu ya ekari za ardhi
yamegawiwa kwa wanaoitwa
wawekezaji wakubwa kwa ajili ya
kulima miti ya mibono kaburi.
Kule Mkoa wa Katavi katika Wilaya
ya Mulele kumekuwa na sintofahamu
kuhusiana na ardhi ambayo ilikuwa
inakaliwa na wakimbizi kutoka nchini
Burundi na sasa kugawiwa kwa
wawekezaji. Kilosa mkoani Morogoro
kumekuwa na vurugu za mara kwa
mara zikihusisha wakulima na
wafugaji.
Mkoani Manyara na mkoani Mbeya
kumekuwa na malalamiko ya
wananchi kuhusu mashamba
yaliyokuwa ya NAFCO na sasa
yamebinafsishwa kwa wawekezaji
ambao wamehodhi ardhi bila
kuifanyia uzalishaji wowote ilhali
wananchi hawana ardhi. Msingi
mkubwa hapa ni kulinda maliasili ya
nchi kwa ajili ya matumizi ya kizazi
cha sasa na vizazi vijavyo. Kuzuia
uharibifu wa rasilimali za nchi
unaofanywa na kikundi cha watu
wachache dhidi ya wengi ama
unaofanywa na kizazi cha sasa dhidi
ya vizazi vijavyo ni kazi ambayo
chama hicho kimeifanya kupitia
wabunge wake.
Mwanachama au kiongozi yeyote wa
CHADEMA ambaye hasimamii msingi
huu anakwenda kinyume cha chama
na anapaswa kutafuta chama kingine
ambacho kitampa uhuru wa
kuruhusu rasilimali za nchi kutumika
vibaya. Viongozi wa chama hicho na
hasa wabunge wanapaswa kuwa
mstari wa mbele kusimamia msingi
huu. Malalamiko ya wananchi
yalikuwa ni malalamiko tu
yanayoibuka na kuzama mpaka pale
mbunge kijana alipoamua
kushughulikia suala hilo, si kwa
kupiga kelele au kuendeleza
kulalamika, bali kwa kutumia njia za
kidemokrasia kupitia Bunge.
Katika Mkutano wa Tisa wa Bunge la
10, Mbunge wa Kawe alifanikiwa
kupitisha hoja bungeni kuhusu
usimamizi bora wa ardhi ya
Tanzania. Kiongozi huyu aliona kuwa
kuna changamoto zilizoanishwa hapo
juu lazima zifanyiwe kazi kwa faida
ya wananchi wa kizazi cha sasa na
kizazi kijacho.
Bunge bila kujali itikadi za kisiasa
lilipitisha azimio la kutaka kufanyika
kwa tathmini ya ardhi nchi nzima ili
kuweza kufahamu ni ardhi kiasi gani
imegawanywa mpaka hivi sasa na
kwa nani. Lengo ni kuweka maamuzi
ya kisera kuhusiana na ugawaji wa
ardhi ili kulinda wananchi maskini
ambao kila kukicha wamekuwa
wakinyanganywa ardhi kwa
kisingizio cha uwekezaji.
Haya ni mafanikio ya kazi za
waabunge wa CHADEMA
wanaosimamia misingi ya chama
kwa kutekeleza kwa vitendo misingi
hiyo. Kutokana na hoja yenyewe ya
ardhi inavyo nufaisha watu binafsi au
vikundi vya watu ambao Mbunge wa
Kawe, Halima Mdee, anawafahamu
au asiowafahamu, mbunge huyu
angeendekeza ufuasi wa watu badala
ya misingi ya chama asingefanikiwa
kufanya masuala haya mazito kwa
nchi, yenye mafanikio kwa wananchi
wote bila kujali vyama vyao.
Faida kubwa ya ufuasi wa misingi ni
kwamba mafanikio yoyote
yanayopatikana katika utekelezaji wa
misingi ya chama,kila mwanachama
anajivunia nayo. Hata hivyo, pale
ambapo chama kimegawanyika kwa
misingi ya ufuasi wa watu au vikundi
vya watu ni nadra mafanikio ya
misingi ya chama inayotekelezwa na
mwanachama ambaye wewe si
mfuasi wake kuyaona kama ni
mafanikio ya chama.
Mafanikio yote yatakayopatikana
kutokana na hoja yenye kuhusiana na
ardhi yanapaswa kuwa mafanikio ya
kujivunia kwa wana CHADEMA wote.
Chama hicho kisione aibu kujivunia
mafanikio ya viongozi wake
wanaotekeleza misingi kwa vitendo.
Mwelekeo wa siasa za zama hizi ni
ya ufuasi wa misingi na si ufuasi wa
watu. Mfuasi wa misingi hawezi
kuyumbishwa kwani misingi
haiyumbi.
Mwezi ujao nitatolea mfano msingi
wa kupinga ufisadi ambapo tutaona
kuhusu usimamizi kwa vitendo wa
vita dhidi ya rushwa na ufisadi
kupitia kwa viongozi wa chama
hicho.
Chanzo: Tanzania Daima | 30
Disemba 2012
MWAKA 1995 Tanzania ilifanya
Uchaguzi Mkuu wa kwanza tangu
irejeshe mfumo wa vyama vingi na
Chama cha CHADEMA kilikuwa
kimeshiriki uchaguzi huu bila ya
kuweka mgombea urais hivyo
kulazimika kumuunga mkono
mgombea wa Chama cha NCCR-
Mageuzi, Augustino Lyatonga
Mrema.
Katika uchaguzi huu wa mwaka 1995
CHADEMA ilipata asilimia sita ya kura
zote za wabunge nchini na kupata
majimbo matatu ya Kigoma Mjini,
Karatu na Rombo. Kilishika nafasi ya
tatu katika vyama vya upinzani
baada ya Chama cha Wananchi (CUF)
na NCCR-Mageuzi.
Mwaka huo CHADEMA iliingia
kwenye uchaguzi chini ya viongozi
waasisi wa chama mzee Edwin Mtei
kama Mwenyekiti, Brown Ngwilulupi
kama Makamu Mwenyekiti na Bob
Nyanga Makani kama Katibu Mkuu.
Mwaka 2000 Tanzania ilifanya
uchaguzi Mkuu wa pili, na CHADEMA
kilikuwa kimeshiriki uchaguzi huu
kwa mara nyingine bila ya kuweka
mgombea urais. CHADEMA
ilishirikiana na CUF kuweka
mgombea mmoja Prof. Ibrahim
Lipumba.
Mwaka huo chama chetu kilipata
asilimia tatu ya kura za wabunge na
jumla ya wabunge wanne na kushika
nafasi ya nne katika vyama vya
upinzani baada ya vyama vya CUF,
TLP na UDP.
Katika uchaguzi wa mwaka 2000
Mzee Makani alikuwa Mwenyekiti,
Dk. Willibrod Slaa Makamu
Mwenyekiti na Dk. Amani Kabourou
kama Katibu Mkuu. Miongoni mwa
wabunge wapya wa CHADEMA
waliochaguliwa mwaka 2000 ni
pamoja na Freeman Mbowe kutoka
Jimbo la Hai.
CHADEMA ilipoteza Jimbo la Rombo,
ikaongeza Hai na Moshi Mjini na
kulinda Karatu na Kigoma Mjini. Ni
vema ieleweke kuwa tangu mfumo
wa vyama vingi uanze mikoa ya
Kigoma, Arusha na Kilimanjaro
imeweka rekodi ya kutoa mbunge
angalau mmoja wa chama hiki.
Karatu ni wilaya iliyoweka rekodi ya
kuchagua CHADEMA mara nne
mfululizo tangu mfumo wa vyama
vingi uanze.
Mazingira haya ya chama cha tano
kwa wingi wa kura katika vyama
vyote vya siasa nchini ndiyo
mazingira iliyoingia nayo CHADEMA
katika uchaguzi wa mwaka 2005.
Mazingira ya kukatisha tamaa, kwani
ujanja mjini haukuwa kwa CHADEMA;
bali CUF au TLP na zaidi CCM.
Mazingira ya kijana ukisema upo
CHADEMA vijana wenzako
wanakuangalia jicho la mshangao na
hata kuchekwa.
Haya ndiyo mazingira ambayo alirithi
Freeman Mbowe, kama mwenyekiti
wa CHADEMA.
Mbowe alianza harakati zake za
kuimarisha CHADEMA kwa
kukusanya vijana mbalimbali,
wanachama wa CHADEMA na wasio
wanachama, kutoka makundi
mbalimbali ya jamii kama wanafunzi
wa vyuo vikuu, waandishi wa habari,
wanasiasa kutoka vyama vingine na
hata vijana wanaharakati katika
NGOs nk.
Moja ya msingi wa CHADEMA ni
kujenga chama chenye kutoa fursa
ambapo kila mtu, bila kujali asili na
hali yake, anaweza kutimiza na
kufanikiwa kadiri ya vipaji vyake.
Kwa mwanasiasa mwingine yeyote
nafasi hii ilikuwa ni nafasi nzuri ya
kujitengenezea fursa yeye
mwenyewe kwa kuhamasisha ufuasi
wa watu badala ya ufuasi wa misingi
ya chama. Badala yake, Mbowe
alitoa fursa kwa kila mwanachama
kuchangia katika kuendesha na
kuimarisha chama. Na hii ndiyo
ilikuwa kauli ya Mbowe kila wakati
kwamba chama ni fursa.. Tuone ni
namna gani Mbowe alitumia misingi
ya CHADEMA kwa kujenga na
kuimarisha chama.
Kazi hii ya kukusanya watu
mbalimbali na mikakati ya kuanza
kusambaza chama kwa kufanya
ziara za wabunge na baadhi ya
viongozi wa chama ilianza mwaka
2003 ambapo wanasiasa wengi
vijana waliokata tamaa na siasa za
vyama vyao walianza kuona
matumaini ndani ya CHADEMA.
Mwaka 2004 mwezi Machi, Mbowe
akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa
tatu wa CHADEMA, hivyo kuwa na
mamlaka zaidi ya kuleta mabadiliko
katika chama. Wanasiasa vijana
kama Shaibu Akwilombe, Antony
Komu na Msafiri Mtemelwa
(aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa
Vijana wa NCCR-Mageuzi) walijiunga
na CHADEMA.
Wanasiasa wanataaluma kama
Mwesiga Baregu nao pia walijiunga
na CHADEMA kipindi hiki. Kuna
kipindi tulikuwa tunajiita Real Madrid
maana tulikusanya mastaa wote
kutoka vyama vya upinzani.
Chama, kwa kupitia misingi yake,
kiliwapa wanachama hawa nafasi
kubwa sana ya kuchangia kwa
mawazo katika kuimarisha chama na
Mbowe alijitahidi sana kutoa fursa hii
kwa kila mwanachama aliye tafuta
nafasi ya kuchangia.
Hata Mbunge wa sasa wa Mtera,
Livingstone Lusinde, alijiunga na
CHADEMA kipindi hiki. Freeman
Mbowe aliifanya kazi hii ili kutoa
fursa kwa Watanzania wengine
kujenga chama imara cha siasa
nchini ili si tu kuimarisha demokrasia
nchini bali pia kutoa mbadala kwa
chama tawala na hata vyama vingine
vya upinzani. Utekelezaji wa msingi
huu wa chama umelipa. Haikuwa
kazi rahisi, bali ni kazi makini yenye
ujasiri wa kuepuka kujifanya Mbowe
ndiye chama na badala yake kujenga
chama taasisi ambapo wanachama
wanaweza kusema demokrasia
ndiyo CHADEMA.
Chini ya uongozi wake, Mbowe
ameshirikiana na viongozi wenzake
kupandisha chama kutoka chama
cha tano mwaka 2000 mpaka chama
cha pili mwaka 2010. Miongoni mwa
Watanzania waliopata fursa ya
kuchangia mabadiliko katika nchi
kupitia juhudi hizi za Mbowe ni
pamoja na mwandishi wa makala hii
na makumi ya wabunge katika Bunge
la Kumi, mamia ya madiwani walio
katika halmashauri mbalimbali nchini
na maelfu ya viongozi katika serikali
za vijiji sehemu mbalibali nchini. Sisi
kama wanachama tulipewa nafasi
nzuri ya kukichangia chama kwa
mawazo mbalimbali, na ni umoja wa
mawazo yetu yote, matendo yetu
sote, kila mmoja kwa nafasi yake,
kwa uwezo wake, ndio ulisaidia
chama kwenda mbele.
Wakati huo, na hadi leo, vyama
mbalimbali vilionekana kuwazuia
wanachama wao kutoa maoni huru
kuhusu uendeshaji wa chama au
hata uendeshaji wa taifa. CHADEMA
kilikubalika kama chama chenye
demokrasia, na haki za kila
mwanachama ziliheshimika. Haki ya
kupendekeza maoni binafsi na
kuyatetea hadi mwisho ni haki ya
msingi inayochangia katika
kutofautisha CHADEMA na vyama
vingi nchini.
Pamoja na kwamba haki hizi zipo
katika misingi ya asili ya CHADEMA,
ni haki ambazo ziliimarishwa zaidi
katika kipindi cha Mwenyekiti wa tatu
wa CHADEMA, Mbowe. Hii ndiyo
misingi ambayo kila mwanachama
wa CHADEMA anapaswa kujivunia na
kuiendeleza ili kuendelea kutoa fursa
kwa Watanzania kujenga upya nchi
yao kupitia CHADEMA.
Iwapo Mbowe angeendekeza ufuasi
wa watu au angetumia nafasi yake
kama mwenyekiti kuwashawishi
wanachama wawe na ufuasi wa
watu, angepofuka na kamwe
asingeweza kufikia mafanikio
makubwa na ya kutiliwa mifano kama
haya ya kujenga asasi imara ya
chama cha siasa. Mifano dhahiri ipo
kwenye vyama fulani fulani hapa
nchini ambapo vyama vilipoanza tu
kuwa chama mtu badala ya chama
asasi vilianza kuporomoka
mporomoko usiozuilika.
Dhumuni mojawapo la kisiasa la
CHADEMA, kwa mujibu wa katiba
yake ni kuendeleza na kudumisha
demokrasia katika mfumo wa vyama
vingi vya siasa, kujenga utamaduni
wa demokrasia katika jamii kwa
kutambua haki za wengi katika
maamuzi na pia kutambua haki za
wachache kusikilizwa, kuheshimiwa
na kulindwa, sambamba na kukubali
ushindani huru, wa haki na wa wazi
katika uchaguzi.
Dhumuni hili ni ushahidi tosha wa nia
ya CHADEMA kujenga taifa la
kidemokrasia lenye uvumilivu wa
kisiasa na kurutubisha mawazo
tofauti. Msingi huu na msingi wa
fursa imekuwa nguzo kubwa sana
iliyoifikisha CHADEMA katika
mwelekeo usiosimama wa kilele cha
mafanikio ya chama cha siasa,
kushika dola kufanya mabadiliko
makubwa yenye maendeleo kwa
wananchi wa Tanzania. CHADEMA,
kama chama kinachopendekeza
misingi hii kinajivunia pia kua mstari
wa mbele katika vyama
vinavyoendeshwa kwa kuheshimu
misingi hii.
Utekelezaji wa dhumuni na misingi hii
na misingi iliyoelezwa katika makala
zilizotangulia (kuhakikisha rasilimali
za nchi zinawafaa wananchi, kupinga
ufisadi) unahitaji uumini wa misingi
na si uumini wa watu. Ujasiri wa
kuamini misingi ya chama na
kuitekeleza kwa vitendo kama
alivyofanya Freeman Mbowe ni
ujasiri wa kuigwa na mwana
demokrasia yeyote mwenye
uzalendo, umakini, uadilifu na utu
kwa Tanzania.
Chama kilichojaa ufuasi wa watu
kitapasuliwa na nyufa za uongo, fitna,
chuki, majungu na kujipendekeza.
Chama cha misingi ndiyo chama
tunachopaswa kujenga na kujivunia
nacho.
Ni ujasiri wa kufuata misingi ndiyo
unaweza kumfanya kiongozi mwenye
timu iliyojaa watu wenye vipawa
mbalimbali na uwezo mkubwa wa
kuvutia wafuasi kama CHADEMA
kuweza kumudu jahazi na
kuliendesha vema. Freeman Mbowe
ameuweza mtihani huu mpaka sasa
na kuendelea kufaulu mtihani huu ni
moja ya silaha kubwa kwa CHADEMA
katika juhudi zake za kuchukua
uongozi wa taifa letu.
Misukosuko ya hapa na pale,
inayosababishwa na wafuasi wa
watu badala ya wafuasi wa misingi
ya chama, haitakwisha. Hata hivyo,
kipimo cha uwezo wa uongozi ni
namna kiongozi anavyoshughulikia
misukosuko. Ufuasi wa misingi ya
chama ndio dawa ya kukabili
misukosuko. Ufuasi wa watu ni sumu
ya kukimaliza chama.
Makala inayo fuata itazungumzia
namna gani CHADEMA ilishinda
uchaguzi mdogo wa madiwani na
ubunge wa Arumeru kwa kupitia
misingi ya chama.
Makala hii ni sehem ya tatu juu ya
sita (3 out of 6) ya series za "fuata
misingi sio watu"
Link to sehem ya kwanza : Kutetea
rasilimali za nchi (Inayomuongelea
Ndugu Halima Mdee) (1 out of 6)
Link to sehem ya pili: Vita dhidi ya
Ufisadi (Inayomuongelea Dk Slaa)(2
out of 6)
**********************
Hiyo ni makala ya Zitto katika
Tanzania daima gazieti la leo tarehe
6,jimapili 2013.....