Zingatia wanaokutegemea unapoandika wosia | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Zingatia wanaokutegemea unapoandika wosia

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Pdidy, Sep 9, 2010.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Sep 9, 2010
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,375
  Likes Received: 5,660
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  KWA watu wengi wa jamii za Kiafrika hudhani kwamba mtu kuandika au kutoa wosia juu ya mali zake, ni mkosi na anayeandika anaonekana ni mtu anayejichulia au kujitabiria kifo.
  Hata hivyo, hiki ni mojawapo ya vitu vinavyosaidia kuilinda familia na jamii kwa ujumla inapotokea mtu aliyeandika wosia huo anapofariki.
  Kwa mujibu wa kifungu namba mbili cha sheria ya Usimamizi wa Mirathi ya Tanzania, wosia ni tamko la mwisho la mtu anayetoa tamko hilo, akielezea jinsi gani mali zake zitunzwe au kufanyiwa kazi pindi atakapofariki.
  Kwa minajili hiyo, mtu aliyetoa tamko hilo, anatakiwa kutoa tamko ambalo ni la mwisho katika matamko yote aliyowahi kuyatoa wakati wa maisha yake juu ya maisha yake.
  Wosia unaweza kuwa wa maneno ya mdomo na vilevile unaweza kuwa wosia uliondikwa kwa maandishi. Hata hivyo, kwa wosia wa maandishi au ule wa mdomo, kuna masharti kadhaa ambayo yanahitajika kutimizwa kwa wosia huo kuwa na nguvu kisheria.
  Mtu anayeandika wosia kimsingi anatakiwa kuwa na mali ambayo anaimilika yeye binafsi (siyo ya ubia au aliyopewa kutokana na wadhifa wake) na vilevile wosia lazima uoneshe nia ya mtamkaji kuhusu kutoa mali zake (pamoja na fedha) kwa watu au mtu fulani na vilevile ndugu msomaji unatakiwa ujue kwamba wosia utakuwa na nguvu kisheria pale tu ambapo mwandishi/mtoa wosia huo atakapokuwa amefariki dunia.
  Kwa wosia wa mdomo hadi uwe una nguvu kisheria, ni lazima ushuhudiwe na watu wasiopungua wanne na kati ya hao,wawili ni lazima wawe watu kutoka katika ukoo wake.
  Hali si tofauti sana kwa upande wa wosia unaondikwa kwa maandishi,kwani wosia huu ni lazima ushuhudiwe na watu wasiopungua wawili na kati ya hao mmoja ni lazima awe ni mtu kutoka katika ukoo wa mtoa wosia.
  Zaidi ya hayo, wosia hauwezi kuwa na athari yeyote kisheria kama mtoa tamko la wosia hatatia saini yake aidha kwa maandishi au kwa kuweka dole gumba. Hii ina maana kwamba mahakama haitautambua wosia huo kama hautakuwa na sahihi ya mtoaji wa tamko hilo.
  Hata hivyo, wosia hata kama utakuwa na vigezo vyote vinavyotakiwa lakini kama mtoaji wake alitoa tamko lake akiwa katika hali ya kuchanganyikiwa akili au kulazimishwa/kushurutishwa, hii ni mojawapo ya vigezo vya kukataa kuidhinisha wosia au mirathi kwa mtu yeyote na mahakama.
  Wosia vilevile ni lazima umtaje mtu atakayeutekeleza au kwa lugha ya Kiingereza anaitwa ‘Executor.’ Huyu ni mtu ambaye mtoa wosia atamchagua katika wosia wake na ndiye atakayepewa majukumu yote ya kuangalia jinsi gani matakwa ya mtoa wosia yatatimizwa.
  Ni kweli kwamba mtu anaweza kuandika wosia na kuufuta wakati wowote na mara zote anazotaka. Sheria haina pingamizi juu ya jambo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mtoa wosia anaweza kubadilisha mawazo yake wakati wowote ule.
  Hata hivyo, wakati wowote mtu atakapokuwa anaandika wosia, ni lazima aandike kwamba wosia huo ni wa mwisho kabisa kati ya wosia mwingine aliowahi kuuandika.
  Hata hivyo, mahakama imepewa uwezo kisheria kutengua au kubatilisha wosia wowote kama haukidhi vigezo vya kisheria kuufanya uwe halali. Katika hali kama hii, familia itatakiwa kumchagua mtu asimamie mirathi kana kwamba marehemu hakuacha wosia wowote kwani wosia wake hautakuwa na nguvu yoyote kisheria.
  Ikiwa baada ya kifo cha mtu aliyeandika wosia, kukapatikana wosia mwingine tofauti na iliyoandikwa siku na tarehe tofauti, basi wosia wa tarehe ya mbele ndiyo utahesabika kuwa halali na siyo wa tarehe ya nyuma yake.
  Hapa sheria inatumia busara kwamba mpaka wosia mwingine uandikwe ina maana marehemu alibadili mawazo yake na ndiyo maana akaandika wosia mwingine. Wosia unapata nguvu kisheria pale tu aliyeandika akifariki dunia.
  Hii ina maana kwamba, hata kama mathalani, mtoto wa marehemu ndiye aliyeandikwa atarithi shamba la marehemu, mtoto huyo hatakuwa mmiliki halali wakati mwandishi wa wosia huo atakapokuwa hai, ila tu pale atakapofariki dunia ndipo mtoto huyo ataweza kuwa mmiliki halali wa shamba hilo. Kimsingi ni haki ya mwandika au mtoa wosia kubadilisha wosia wake wakati wowote autakao. Vilevile ni haki yake kumpa urithi mtu yeyote atakayekuwa amemchagua katika wosia wake. Hata hivyo, mwandishi wa wosia ni lazima azingatie watoto ambao ni wategemezi kwake pale atakapokuwa kuwa anaandika/anapotoa wosia wake.
   
Loading...