TANESCO
Official Account
- Jul 12, 2014
- 4,595
- 2,115
HATUA YA KWANZA
MAOMBI YA MWANZO
Je mteja anaweza kuchukua fomu ofisi yeyote ya tanesco?
Mteja anaweza kuchukua fomu ya maombi ya umeme katika ofisi yeyote ya shirika bila kujali kuwa eneo hilo linahudumiwa na ofisi husika. Ila atapaswa kurudisha ofisi ya maeneo ambayo makazi yake yapo ili kurahisisha kufanyiwa vipimo (service line survey)
JE KUNA GHARAMA ZOZOTE KATIKA UCHUKUAJI WA FOMU?
Fomu za maombi ya umeme zinatolewa bure kabisa kwa wateja wote.
VITU MUHIMU VYA KUZINGATIA WAKATI WA KUCHUKUA FOMU
1. Hakikisha umeme umefika maeneo yako na kama ni mradi uwe umekamilika.
2. Hakikisha mtandao wa nyaya ndani ya nyumba yako (wiring) umefanyika kupitia mkandarasi aliyesajiliwa.
3. Kitambulisho kinachomtambulisha muombaji wa umeme mfano leseni ya udereva, hati ya kusafiria, kitambulisho cha kazi (hii inasaidia shirika kumtambua mteja husika)
4. Kwa mwombaji wa mita ya ziada (meter separation) jina litakalotumika ni la mwenye nyumba kama linavyosomeka katika mita ya awali. Vinginevyo mteja atapaswa kutumia uthibitisho wa ruhusa ya mwenyenyumba kama atakuwa ni mpangaji. Lazima mteja aje na namba ya mita (kama zipo zaidi ya moja aje nazo zote) ili kuhakiki kama kuna yenye deni.
5. Kwa waombaji wanaomba kwa ajili ya ofisi, makapuni au taasisi za serikali au binafsi anapaswa kuja na leseni ya biashara, tin namba, udhibitisho wa usajili wa kampuni. Au udhibitisho wa ofisi ya serikali husika.
6. Kwa wapangaji wa nyumba za taasisi au makampuni waje na barua za waliopangisha zinazoonyesha kuwe wenye nyumba hizo wameridhia mita husika iwe na jina la mpangaji husika.
7. Shirika linapenda kuwaomba wamiliki wa nyumba kupenda kufika ofisi zetu wenyewe ili kuzuia udanganyifu ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu
HATUA YA PILI KUWEKA MCHORO, PICHA NA KUINGIA MAKUBALIANO YA KUFUNGIWA UMEME NAKUREJESHA FOMU
Endapo mteja atakidhi vigezo na masharti ya hatua ya mwanzo na kupatiwa fomu ya maombi ya mwanzo anatakiwa afanye yafuatayo
1. Kuisoma fomu kwa umakini mkubwa na kukubailiana na vigezo namba moja mpaka kumi na mbili. Mteja akijiridhisha kuwa amekubaliana na masharti yote ataweka sahihi sehemu husika (ukurasa wa pili wa fomu ya maombi ya umeme)
2. Kumpatia mkandarasi aliyesajiliwa ili achore mchoro wa mtandao wa nyaya (wiring diagram) wa nyumba husika pamoja na kugonga muhuri. (gharama ni makubaliano baina ya mteja na mkandarasi husika), wakandarasi wanapatikana kwenye ofisi zao maeneo mbalimbali, orodha ya waliosajiliwa pia inapatikana kwenye ofisi za tanesco. Mteja anapaswa kupewa orodha na kuchagua mkandarasi anayemtaka yeye.
3. Mteja atapaswa kuweka picha moja ya mwombaji wa umeme
4. Kisha mteja atarudisha fomu hiyo iliyokamilika ofisi ya eneo ambalo makazi yake yako (inayomudumia)
HATUA YA TATU- KUFANYIWA VIPIMO (SURVEY)
Mara baada ya mteja kurejesha fomu iliyojazwa kikamilifu, mteja atapangiwa tarehe ya kufanyiwa vipimo (survey). Mafundi watafika kwenye nyumba au sehemu inayoombewa umeme ili kutathimini gharama atakazolipia mteja kwa kuzingatia umbali wa eneo ilipo miundombinu ya umeme kama nguzo na transfoma na uwezo wa umeme huo kuunganisha kwa wateja wapya.
HATUA YA NNE: - KUPATIWA MAKADIRIO YA GHARAMA KIASI GANI ALIPE ILI AFUNGIWA UMEME
Mara baada ya kufanyiwa tathimini mteja anaweza kupatiwa makadirio ya gharama ya kiasi gani alipe ili kufungiwa umeme. Makadirio haya huweza kutumwa kwa njia ya nukushi, ujumbe mfupi wa meneno, barua pepe au mteja kufika ofisini na kuchukua barua. Viwango vya muda wa kutoa makadirio kama inavyoonekana kwenye jedwali hapo chini:
MAELEZO
Muda wa makadirio
Kama miundombinu iliyopo itatumika (ndani ya mita 30 kutoka kwenye nguzo iliyokaribu)
Ndani ya siku 7 za kazi
Ujenzi wa njia ya nyongeza unahitajika (mita 30- 100)
Ndani ya siku 10 za kazi
Kama mfumo mpya wa usambazaji unahitajika kujegwa au mfumo wa umeme mkubwa unahitajika kuongezwa kwa ajili ya kiwanda au biashara kubwa (kama hakuna mfumo wa kumuunganishia mwombaji) (zaidi ya mita 100)
Ndani ya siku 14 za kazi
HATUA YA TANO: - KUFANYA MALIPO
Mteja atafika ofisi ya tanesco ili kupatiwa namba ya kumbukumbu (reference number) itakayomuwezesha kufanya malipo bank, mteja atafanya malipo na atapatiwa stakabadhi ya malipo bank (risiti kwa njia ya ujumbe mfupi- sms) (kwa sasa ni bank ya nmb tu), wateja wanahimizwa kufanya malipo yote bank na si kwa mtu mwingine yeyote. Malipo yote yatakayofanyika nje ya mfumo uliwekwa hayatambulika na tanesco. Mteja akishafanya malipo bank husika hatatakiwa kurudi tena tanesco bali tanesco watakuwa na taarifa zake zote na kinachofuata ni kumfungia umeme.
HATUA YA SITA:-KUUNGANISHIWA UMEME
Mara baada ya mteja kufanya malipo viwango vya muda wa kumfungia umeme vitakuwa kama ilivyoonyeshwa kwenye jedwali hapo chini.
MAELEZO
Muda wa kufungiwa
Kama miundombinu iliyopo itatumika (ndani ya mita 30 kutoka kwenye nguzo iliyokaribu)
Ndani ya siku 30 za kazi
Ujenzi wa njia ya nyongeza itahitajika
(mita 30- 100)
Ndani ya siku 60 za kazi
KAMA MFUMO MPYA WA USAMBAZAJI UNAHITAJIKA KUJEGWA AU MFUMO WA UMEME MKUBWA UNAHITAJIKA KUONGEZWA KWA AJILI YA KIWANDA AU BIASHARA KUBWA (KAMA HAKUNA MFUMO WA KUMUUNGANISHIA MWOMBAJI) (ZAIDI YA MITA 100)
Ndani ya siku 90 za kazi
KWA MAULIZO WASILIANA NASI
Kituo cha huduma kwa wateja: - 0768985100/0222194400
Barua pepe: customer.Service@tanesco.Co.Tz
Facebook: www.Facebook.Com/tanesco yetu
Twitter: - www.Twitter.Com/tanesco yetu
Tovuti; www.Tanesco.Co.Tz