Trump amewasili.
Mei 13, kutokana na mwaliko wa rais Xi Jinping wa China, rais Trump aliwasili Beijing kwa ajili ya ziara ya siku tatu nchini China, ambayo ni ziara ya kwanza ya kiserikali nchini China katyika wa muhula wake wa pili.
Katika miaka ya hivi karibuni, uhusiano kati ya China na Marekani umeshuhudia misukosuko mbalimbali, kuanzia vita ya biashara hadi vita ya teknolojia, kuanzia Mlango-Bahari wa Taiwan hadi Bahari ya Kusini ya China.Lakini safari hii, ziara ya Trump ina mambo matatu ambayo si ya kawaida sana.
Jambo la kwanza ni mabadiliko katika sauti ya Marekani.
Katika miaka michache iliyopita, ripoti ya Mkakati wa Ulinzi wa Kitaifa wa Marekani ilisema waziwazi kwamba China ni "tishio namba moja." Lakini kabla ya ziara ya Trump nchini China, toleo jipya la ripoti hiyo lilitolewa—maneno hayo hayapo tena. Badala yake yalikuwa: kutafuta “uhusiano wa utulivu, amani, biashara yenye uwiano na kuheshimiana."
Trump mwenyewe pia amesema hadharani: "Mafanikio ya China lazima yaheshimiwe," na kwamba Marekani na China "zinaelewana vizuri sana."
Kutoka "tishio namba moja" hadi "lazima yaheshimiwe," kila mtu anajua ni raundi ngapi za makabiliano zimepita.
Kwa ufupi, Marekani inafanya mahesabu yake. Wito wa "kutenganisha na kuvunja minyororo" ni wa kutisha, lakini ni nani anayeteseka hatimaye? Biashara za Marekani na watu wa kawaida wanateseka. Ushuru mkubwa umesababisha mfumuko wa bei usiodhibitika, unaowakasirisha wapiga kura; vikwazo vinazuia mauzo ya chip za Silicon Valley, na Wall Street inapoteza faida.
Ni wazi, Trump hayupo hapa Beijing kubishana—yuko hapa kutafuta jinsi ya kushirikiana kwa njia ambayo itanufaisha zaidi "Marekani Kwanza."
Jambo la pili ni kwamba maudhui ya majadiliano yalikuwa ya kivitendo sana.
Kwenye mazungumzo yao, wakuu hao wawili wa nchi wamefanya majadiliano ya kina kuhusu biashara, Taiwan, na masuala mabalimbali ya kimataifa. Mada hizi zinawakilisha hoja za mikwaruzano na pia maeneo yanawezekana kwa ushirikiano wa siku zijazo.
Biashara imekuwa msingi wa uhusiano wa China na Marekani. Hivi sasa, Marekani inaweka ushuru mkubwa kwa bidhaa za China, na kufanya bidhaa za China kuwa ghali nchini Marekani, bei ambazo haziwezi kuvumiliwa na wateja wa Marekani na mfumuko wa bei kuwa mkubwa. Hata hivyo, timu za biashara za nchi hizo mbili zimefikia makubaliano yenye uwiano na chanya kwa ujumla, ambayo ni habari njema kwa watu wa nchi zote mbili na dunia nzima. Wakati huo huo, viongozi wa biashara zaidi ya kumi kutoka sekta za biashara na viwanda wameandamana na rais Trump katika ziara yake, jambo ambalo limeonyesha jinsi rais Trump anavyozingatia sana kupanua soko la China.
Suala la Taiwan ndilo hatari kubwa zaidi katika uhusiano wa China na Marekani. Rais Xi Jinping amemwambia Trump waziwazi wakati wa mazungumzo kwamba ikiwa suala la Taiwan litashughulikiwa vizuri, uhusiano wa China na Marekani unaweza kudumisha utulivu kwa ujumla; la sivyo, nchi hizo mbili zitavutana na hata kupigana, na kusukuma uhusiano mzima wa China na Marekani katika hali hatari sana. Kauli hii inadhihirisha tena kwamba suala la Taiwan ni mstari mwekundu ambao China haiwezi kuuvuka, na haitaki kuona suala la Taiwan likiwa kichocheo cha mzozo kati ya China na Marekani.
Zaidi ya hayo, wakuu hao wawili wa nchi pia walibadilishana mawazo kuhusu Mashariki ya Kati, Ukraine, na Peninsula ya Korea—maeneo yenye misukosuko zaidi duniani.
Jambo la tatu ni kwamba ziara hii si kuhusu China na Marekani pekee.
Kwa muda mrefu, Marekani imekuwa ikitafuta "ushindani kati ya nchi zenye nguvu" kote duniani, ikilazimisha nchi nyingine kuchagua upande. Sasa kwa kuwa China na Marekani zinaweza kukaa chini na kuzungumza, nchi hizi zinaweza kupumua kidogo—zinaweza kufuata "diplomasia yenye usawa," kufanya biashara na China, na pia kushirikiana katika usalama na Marekani, mambo ambayo hayakinzani.
Kwa undani zaidi, zikiwa ni nchi zenye uchumi mkubwa zaidi duniani zinaweza kufuata njia mpya ya "kutopigana, kuzungumza zaidi, na kuweka bayana misingi," zitavunja mtego maarufu wa "nguvu kubwa bila shaka husababisha vita". Mchango huu kwa mazingira ya kimataifa unaweza kuwa muhimu zaidi kuliko ni kiasi gani cha mikataba imesainiwa.
Hata hivyo, bado ni mapema kuridhika.
Ziara moja haiwezi kutatua matatizo yote. Tofauti za kimuundo kati ya China na Marekani hazitatoweka kwa sababu tu Trump amefanya ziara nchini China , na haitarajiwi kwamba watu wanaopinga China nchini Marekani watanyamaza. Zaidi ya hayo, sifa kubwa ya Trump ni kutotabirika kwake. Kwa hivyo, matokeo ya ziara hii yatakuwa ya kimfumo na kimwelekeo; bado kuna safari ndefu kabla ya mafanikio haya kutekelezwa kweli.
Kwa kumalizia: Kukaa chini kuzungumza ni bora kuliko kupindua meza.
Ziara ya Trump nchini China si mwisho, bali ni mwanzo.
Kwa sasa Trump yupo China. Je, uhusiano kati ya China na Marekani utaendeleaje? Tusubiri tuone.