Ziara ya Kilango yaibua mengi yaliojificha CCM Kilimanjaro | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ziara ya Kilango yaibua mengi yaliojificha CCM Kilimanjaro

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Josh Michael, Dec 6, 2009.

 1. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #1
  Dec 6, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Na Daniel Mjema,Moshi

  ZIARA ya siku tisa ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), Anne Kilango Malecela katika Mkoa wa Kilimanjaro, imeibua mambo mengi yaliyokuwa yamejificha na kukitafuna chama hicho.

  Sasa ni dhahiri hali ya kisiasa katika chama hicho katika majimbo ya Moshi Mjini,Mwanga na Vunjo sio nzuri kutokana na kuibuka kwa makundi yanayopingana kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010.

  Kitendo cha wananchi wa mji mdogo wa Himo 'waliobatizwa' kwamba ni wafuasi wa Tanzania Labour Party (TLP), kumzomea Mbunge wa Jimbo la Vunjo,Aloyce Kimaro mbele ya Mama Kilango kinakitia doa chama hicho.

  Utafiti uliofanywa na gazeti hili, umebainisha kuwa mpasuko mkubwa uko ndani ya CCM yenyewe na baadhi ya waliomzomea Kimaro wanadaiwa kwamba ni wananchi wa kawaida na wengine ni wafuasi wa CCM.

  Mpasuko huo, mkubwa ndani ya CCM Jimbo la Vunjo ulioanzia uchaguzi wa 2005,umeongezwa nguvu na kundi kubwa la wapambe wa mwanasiasa kijana(jina tunalo) anayedaiwa kuwa katika harakati za kumng'oa Kimaro 2010.

  Mahudhurio hafifu ya wananchi na wana-CCM katika mikutano ya Mbunge huyo, yanadhihirisha kuwa lipo kundi linalomwaga sumu mbaya na propaganda dhidi ya utendaji wa Kimaro ili kumkosanisha na wapiga kura wake.

  Kimaro mwenyewe ambaye ni maarufu kama Simba wa Yuda, amekaririwa akitamba kuwa ataibuka mshindi kuanzia kura za maoni ndani ya CCM na kwenye sanduku la kura la wananchi, akisema atafanya kampeni kisayansi.

  Kauli ya Mama Kilango aliyoitoa katika mkutano wa hadhara Moshi mjini akiwapasha wanaCCM kuwa wao ndio chanzo cha chama hicho, kupoteza jimbo hilo mara tatu mfululizo ni ushahidi tosha kuwa lipo tatizo.

  "Kwanini tupate madiwani 12 na CHADEMA watatu halafu tushindwe Ubunge? Nitataka nimfahamu mchawi ili nimshike mkono nimwambie Rais Kikwete huyu ndiye anayetufanya tushindwe kulichukua jimbo hili," alisema Kilango.

  Ndesamburo ni Mbunge wa Jimbo la Moshi mjini kwa tiketi ya CHADEMA (2000-2005 na 2005-2010) na inadaiwa kuwa mgawanyiko,fitina na CCM kuhujumiana wenyewe kwa wenyewe ndivyo vinavyompa ushindi Ndesamburo.

  Lakini Mbunge huyo amekaririwa akipinga dhana kuwa ushindi wake unatokana na wanaCCM akijenga hoja kuwa yeye huchaguliwa na idadi kubwa ya wananchi wasio na itikadi na kama wapo ni kwa idadi ndogo sana.

  "Mimi sitishiki yeye (Kilango) afanye kampeni anavyotaka na mimi sijawahi kumwambia wanaonifanya nishinde ni wanaCCM hata kidogo, wanaCCM hawazidi 5,000 mimi nilipigiwa kura na wananchi 30,000," alisema.

  Katika uchaguzi wa 2005, Ndesamburo aliibuka mshindi baada ya kunyakua kura 32,035 sawa na asilimia 56.5 dhidi ya kura 23,773 sawa na asilimia 41.9 alizopata mgombea wa CCM ambaye ni wakili,Elizabeth Minde.

  Miongoni mwa yaliyojiri katika ziara ya Mama Kilango ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, ni kitendo cha baadhi ya wanawake katika Jimbo la Mwanga kuleta tafrani wakitaka Mbunge huyo awarejeshee nauli na posho.

  Mwanasiasa mkongwe nchini,Peter Kisumo aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa mazoea ya watu kutaka kulipwa yasipokemewa na yatasababisha kuporomoka kwa maadili.

  "Hatuwezi kukubali hii hali kuwa mwanaCCM au kiongozi akitaka kusema na wanachama aandae pesa hapana! Tunaelekea wapi?" Alihoji Kisumo akisema maandalizi yote ya vikao yanapaswa kuwa chini ya chama na si mtu.

  Tukiangalia hali ya kisiasa katika jimbo hilo ambalo linaoongozwa na Profesa Jumanne Maghembe,hali ya kisiasa inatikiswa,lakini sura halisi za siasa za Mwanga sasa imefika katika kiwango kibaya cha wanaCCM wenyewe wanafanyiana fitina.

  Mathalani, wiki iliyopita, Profesa Maghembe alikaririwa akisema limeibuka kundi la mahasimu wake wa kisiasa linaloeneza fitina ya kumchonganisha na Kisumo na waziri Mkuu mstaafu,Cleopa Msuya.

  Kwa tafsiri rahisi ni kwamba Jimbo la Mwanga sasa ndani ya CCM yapo makundi mawili yanayohasimiana, lakini yote yakitaka kuungwa mkono na wanasiasa hao wawili wenye nguvu na ushawishi mkubwa wa kisiasa jimboni humo.
   
Loading...