Zanini, mwanamke anayefanya kazi za ndani miaka 20 kwa Bosi mmoja

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
1691391007626.png


Mara kadhaa kumeripotiwa matukio ya kikatili yanayodaiwa kufanywa na wafanyakazi wa ndani, ikiwamo kuwaua au kuwapiga watoto wa mabosi zao wakati wazazi husika wakiwa hawapo nyumbani,

Hali hiyo imesababisha kujenga uadui kati ya wafanyakazi wa ndani na waajiri.

Hatua hiyo, imesababisha wenye uwezo kufunga kamera maalumu za kufuatilia matukio yanayoendelea ndani ya nyumba, lengo likiwa kuwalinda watoto wao wasifanyiwe vitendo vibaya na wafanyakazi hao.

Hata hivyo, hali hiyo ni tofauti na mfanyakazi wa ndani, Zanini Othuman kwa kile alichoeleza kuwa upendo uliopo kati yake na watoto wa mwajiri wake ni mkubwa kiasi cha kumsaidia asipoteza kazi yake.

Zanini, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti Chama cha Wafanyakazi za Majumbani Mkoa wa Dar es Salaam anasema mwaka 2003 baada ya kufiwa na baba yake alianza kufanya kazi za nyumbani na ilipofika mwaka 2006 alipata ujauzito.

"Pamoja na mwajiri wangu kunifanyisha kazi kipindi chote cha miezi tisa ya mimba, ilipofika muda wa kwenda kujifungua, aliniambia nisirudi tena na angetafuta mfanyakazi mwingine, ikizingatiwa msichana wake mwingine aliyeondoka kabla yake alipatwa na changamoto kama hiyo, hivyo akaona yatakuwa yale yale,” alisema Zanini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi za Majumbani, cheo alichokipata mwaka 2018.

"Maamuzi haya ya bosi wangu kuwa nisirudi kazini yaliniumiza sana, ukizingatia ni kazi niliyokuwa naitegemea inisaidie kumlea na mtoto wangu, nilimwitikia tu, lakini kiukweli nilikuwa nimeshapoteza mwelekeo na kutojua nini hasa nitafanya."

Hata hivyo, wakati siku zikiwa zinaelekea ukingoni, Zanini ambaye anafanya kazi ya kwenda kazini na kulala nyumbani kwake, anasema aliwaaga watoto wa bosi wake kuwa hatarudi tena akishakwenda kujifungua kwa kuwa mama yao kakataa asifanye kazi tena.

Kwa kuwa watoto wa bosi wake walikuwa wanampenda kwa jinsi alivyoishi nao kwa upendo, walimwambia wataongea na mama yao asimwachishe kazi na kumshauri kipindi ambacho yupo kwenye uzazi ni vema akamtafuta mtu mbadala wa kumshikia.

"Waliniambia nimtafute mtu ninayemjua ili itakapofika wakati wa kurejea kazini iwe rahisi kumuondoa, pindi nitakapokuwa tayari kurudi,” anasema mfanyakazi huyo.

Zanini anasema hilo alilitelekeza, na baada ya kumaliza siku 40 za uzazi alirejea kazini kuendelea na shughuli zake, kazi anayoifanya hadi leo.

Mama huyo wa watoto wawili kwa sasa anasema, "nina imani haya yote yalifanyika kwa kuwa nilikuwa nikiishi vizuri na watoto wa bosi wangu, kama watoto wameridhika mfanyakazi ni nadra sana kufukuzwa, labda uwe na matatizo yako mengine na bosi."

Nini kajifunza?

Kutokana na yaliyomkuta katika ajira yake, Zanini anasema anatamani mkataba wa kimataifa namba 189 wa wafanyakazi majumbani, uridhiwe na Serikali haraka kwa kuwa pamoja na kuzungumzia haki mbalimbali wanazopaswa kupewa wafanyakazi, limo suala la likizo.

"Pia naiomba jamii ielewe kwamba mfanyakazi wa ndani ana haki ya kuanzisha familia yake, na sio inapofika katika hatua hiyo anaonekana kama mkosaji na kupoteza kibarua chake, kwa ni moja ya kesi nyingi anazozipokea kutoka kwa wanachama na waajiri wao," anasema Zanini ambaye baada ya kujifungua mtoto wake alikuwa akimuacha kwa mama yake kisha yeye anakwenda kazini.

Zanini anaiomba jamii kuwathamini wafanyakazi wa majumbani kwa kile alichosema ukiwatenda vibaya ni rahisi kudhuru familia, “hawa ndio walinzi wa nyumba na wapishi.”

Anasema kutowathamini wafanyakazi wa ndani ni chanzo cha kufanya ukatili dhidi ya mabosi au watoto wa mabosi wao.

Changamoto kama hizo, anasema huwa anakutana nazo kwa wanachama wake, lakini yeye aliponea kwa watoto wa bosi wake kwa kuwa walikuwa wanampenda.

“Wito wangu kwa jamii kuwaona wafanyakazi wa ndani nao wana mahitaji yao, na huwa wana haki ya kuwa na familia pia, hivyo inapotokea mfanyakazi kapata ujauzito apewe likizo ya uzazi kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine.”

Anafanyaje kazi za chama


Zanini anasema yeye akiwa mwenyekiti wa wafanyakazi wa ndani anashukuru anapata muda pia wa kufanya kazi za chama kwa kuwa bosi wake amekuwa akimuunga mkono katika hilo.

"Nashukuru bosi anajua mimi ni mwenyekiti katika chama changu, ananipa muda wa kufanya kazi za kichama, kikubwa tu niwe nimemaliza kutekeleza majukumu yangu na hata ikitokea napaswa kusafiri huwa nikimpa taarifa mapema," anasema Zanini.

Akieleza changamoto anazozipata katika kuongoza chama hicho, anasema kuna ugumu wa kuwapata wanachama, hasa wanaoishi kwa mwajiri, hivyo anachofanya ni kuwavizia wakiwa wanaenda dukani au kuwasindikiza watoto kupanda gari la shule, njia zinazotumiwa pia na viongozi wa mikoani.

Alipoulizwa anawatambuaje, Zanini anasema wanajuana kwa kuwaangalia hasa maeneo ya Upanga, wengi wanavalishwa sare siku hizi.

Mpaka sasa chama hicho kwa Mkoa wa Dar es Salaam kuna wanachama 30, huku Taifa wakiwa 5,000, lakini malengo kufikia 10,000 mwaka 2025.

“Ili kuongeza wanachama kirahisi, naomba maofisa kazi wanisaidie kuwafikia wafanyakazi wengine wa ndani kwa kuwa anaamini asilimia kubwa nyumba zina wafanyakazi hao,” anasema Zanini.

Mikataba ya wafanyakazi wa ndani

Mwanasheria wa Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani Hifadhi, Hotelini, Huduma za Jamii na Ushauri (Chodawu), Wagala Shungu, anaungana na Zanini na kueleza alichofanyiwa mfanyakazi huyo ndio wengi hufanyiwa na kuwataka waajiri kuzingatia mikataba ya kazi.

Wagala anasema hayo yote ni matokea ya waajiri na wafanyakazi kuingia mikataba ya mdomo licha ya Serikali katika sheria za kazi inataka waingie mikataba ya kimaandishi.

Anasema haki hizo za likizo ya uzazi zipo, lakini hakuna ufuatiliaji na wafanyakazi wenyewe hawajui kama wana haki hizo.

Kutokana na hilo, mwanasheria huyo anasema kwa sasa wamekuwa wakiupambania mkataba namba 189 wa wafanyakazi kazi za ndani.

Wagala anasema mkataba huo unasisitiza umuhimu wa kuingia mkataba wa kimaandishi, kupewa haki zote kama wafanyakazi ikiwamo likizo ya uzazi, mapumziko kwa saa 24, kujiunga na mifuko ya hifadhi za jamii na haki ya faragha kwa mfanyakazi kuwa na chumba chake mwenyewe cha kuishi.

"Juhudi nyingine tunazozifanya ni kuhakikisha kazi hii inaheshimiwa, ikiwamo kuja na mtalaa maalumu kwa ajili ya kazi hizo utakaokuwa ukifundishwa katika vyuo vya ufundi Veta, kazi ambayo tumeifanya kwa kushirikiana na jumuiya ya watu wanaojitolea ulimwenguni (CVM) Tanzania,” anasema Wagala.

Anasema programu hiyo ya kuwasomesha wafanyakazi wa majumbani ina lengo la kuwasaidia kuongeza ujuzi katika kazi zao na kuuzika kitaifa na kimataifa.

Mratibu wa mradi huo, Ibrahim Mtoni, anasema mradi uliopewa jina la mradi wa kukuza kazi zenye heshima, haki na utu kwa wafanyakazi wa majumbani, umekuja wakiamini kutawaongezea uelewa na ufanisi wafanyakazi hao na kuweza kuuzika kitaifa na kimataifa.

Katika kuteleza hilo, Mtoni anasema wametenga Sh87 milioni kwa ajili ya kuwasomesha wafanyakazi hao na Sh98 milioni kwa ajili ya kununulia vifaa mbalimbali kwenye Vyuo vya Ufundi Stadi (Veta).

“Mradi huu utakuwa na msaada kwa wafanyakazi hawa, kwani tumekuwa tukishuhudia baadhi yao wakiwa wanafika maeneo yao ya kazi hawana wanalolijua na mwisho wa siku kuishia kufukuzwa, huku kwa wale wa nje wakiishia kupewa kazi ambazo sizo walizokwenda kuzifuata,” anasema Mtoni.

Mkuu wa Idara ya Sheria Chodawu, Asteria Mathias, anasema ili mfanyakazi kuweza kupata mafunzo haya, ni lazima awe mwanachama wa Chodawu na ada italipwa na chama hicho, baadaye atakatwa kidogokidogo kwenye mshahara wake, kiasi kisichozidi Sh5,000 kwa mwezi.

Asteria anasema ni lazima mwajiri wake awe ameridhia kwa maandishi kwa kuwa lazima itamchukulia muda, hasa anapokuwa darasani na kuacha kazi, “lakini lazima akubali kutoa fedha iliyotumika kumsomesha mfanyakazi wake katika mshahara atakaomlipa.”

Katika kusoma huko, anasema kuna machaguo mawili, ikiwamo kusoma kutwa au kulala huko huko, mafunzo yatakayochukua mwezi mmoja na kuvitaja vyuo vitakavyohusika katika utoaji mafunzo hayo kwa sasa kuwa ni Veta ya Dodoma, Mikumi Morogoro, Tanga, Dar es Salaam na VTA Zanzibar.

Veta wanasemaje?

Kwa mujibu wa Veta, wataanza mafunzo hayo Oktoba mwaka huu, licha ya kuwa walishaanza kwa majaribio, huku wanachama 44 wa Chodawu wakifaidika.

Ofisa Ukuzaji Mitalaa Veta, Anna Nyoni anasema wameandaa mitalaa miwili tofauti kati ya hiyo, ipo ya wafanyakazi wa majumbani hapa nchini na upo wa wafanyakazi wa majumbani wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi. Ndani ya mitalaa hiyo, Anna anasema watajifunza mambo mbalimbali, ikiwamo mikataba, namna ya kutunza nyumba, kulea watoto na kulea Wazee.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom