Mwasisi wa Mageuzi avunjiwa nyumba mbili
Thursday, 14 October 2010
MWANASIASA Mkongwe na mwasisi wa mfumo wa vyama vingi nchini James Mapalala anaishi katika mazingira magumu, kando ya zizi la ng'ombe baada ya nyumba zake mbili kupigwa mnada na kubomolewa.
Habari zimeeleza kuwa nyumba hizo zilizoko kwenye kitalu namba 403 mtaa wa Usino North, barabara ya Moroco, zilibomolewa juzi na dalali wa mahakama kutokana na mtu aliyemdhamini kuchukua mkopo wa dola 12, 000 benki, kushindwa kulipa.
Mapalala ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Haki na Ustawi (CHAUSTA ), alilieleza gazeti hili jana kuwa nyumba hizo, zina thamani ya Sh80 milioni na kwamba eneo husika lina thamani ya Sh 1.5 bilioni, lakini zimeuzwa kwa Sh100milioni.
Alisema nyumba hizo, zilivunjwa Oktoba 11, mwaka huu majira ya mchana wakati yeye akiwa mahakamani kukata rufaa kwa ajili ya kupinga hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama kuu.
"Mahakama Kuu iliamua nyumba hiyo iuzwe ili kulipa deni hilo,Oktoba 5, mwaka huu na ilivunwa Oktoba 11, mwaka huu.
"Tangu siku hiyo nimelazimika kuishi kwenye chumba cha mfanyakazi wangu wa ng'ombe ambacho kipo zizini," alisema Mapalala.
Alikisimulia mkasa huo, alisema mwaka 2003, alimdhamini rafiki yake ambaye sasa ni marehemu, Mozes Maira kukopa kwa ajili ya kukopa Dola 12,000 kutoka benki ya Savings Finances ya jijini Dar es Salaam.
"Mkataba huo, ulionyesha kuwa mkopaji (Maira) anatakiwa alipe ndani ya miezi miwili, lakini alishindwa kuzilipa.
"Ilipofika mwaka 2004, benki ilifungua kesi namba 79/2004 katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, lakini baadaye kesi hiyo ilikuwa ikizungumzwa nje ya mahakama kwa makubaliano ya benki na mkopaji, lakini mwaka 2008 mahakama hiyo, ilitoa hati ya kuvunjwa kwa nyumba hiyo baada ya mkopaji kushindwa kulipa deni hilo," alisema Mapalala.
Alisema kutokana na hali hiyo, alifungua kesi Mahakama ya Ardhi kuomba deni hilo adaiwe mkopaji mwenyewe kwa sababu udhamini wake kwa Maira, haukuhusisha mali.
"Kesi nilifungua, lakini haikuweza kusikilizwa mapema. Baadaye nikaamua kukata rufaa mahakama Kuu,lakini sikufanikiwa baada ya mahakama hiyo, kunieleza nimechelewa kukata rufaa.
"Nilipoiomba mahakama inisikilize na mimi upande wangu, ilisisitiza kuwa madai yangu yamepitwa na wakati na uamuzi ulikuwa tayari umetolewa," alisema Mapalala.
Mapalala alisema Maira alifariki dunia mwaka 2009, na deni alilokuwa akidaiwa rafiki yake, liliamishiwa kwake .