Yajue majukumu ya viongozi wa Serikali za Vijiji, Kata, Tarafa, Wilaya na Mkoa kwa mujibu wa sheria

YALIYOMO.
1. Majukumu ya afisa mtendaji wa kijiji
2. Majukumu ya afisa mtendaji wa kata
3. Majukumu ya afisa tarafa
4. Majukumu ya diwani
5. Majukumu ya meya/mwenyekiti wa halmashauri
6. Majukumu ya mwenyekiti wa kijiji
7. Majukumu ya mwenyekiti wa mtaa
8. Majukumu ya mwenyekiti wa kitongoji
9. Majukumu ya katibu tawala wa wilaya
10. Majukumu ya mkuu wa wilaya
11. Majukumu ya katibu tawala wa mkoa
12. Majukumu ya mkuu wa mkoa
____________________________________

I. MAJUKUMU YA AFISA MTENDAJI WA KIJIJI
(i) Atakuwa Mtendaji na Mshauri Mkuu wa Serikali ya Kijiji na Kamati zake katika Mipango ya Maendeleo ya kijamii na Utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo.

(ii) Atakuwa Afisa Mhasibu wa Serikali ya Kijiji na atasimamia mapato na matumizi ya Serikali ya kijiji.

(iii)Atakuwa Mlinzi wa Amani na Msimamizi wa Utawala Bora katika Kijiji.

(iv) Ataratibu na kusimamia upangaji wa utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo ya kijiji.

(v) Atakuwa Katibu wa Kamati ya Halmashauri ya Kijiji.

(vi) Atatafsiri Sera, ataratibu na kusimamia utekelezaji wa Sheria ndogondogo za Halmashauri ya Kijiji.

(vii) Ataratibu na kuandaa taarifa ya utekelezaji wa kazi katika eneo lake na kuziwasilisha kwenye Halimashauri ya Kijiji na baadae kwenye kata.

(viii) Ataongoza vikao vya maendeleo ya Kijiji vitavyowahusisha wananchi na wataalamu waliopo kwenye eneo lake.

(ix) Atahamasisha wananchi katika kampeni za kuondoa njaa, umasikini, na kuongeza uzalishaji mali.

(x) Atasimamia matumizi bora ya Nguvu kazi.

(xi) Atakuwa Kiongozi wa Wakuu wa Vitengo vya Kitaalamu Katika Kijiji.

(xii) Atasimamia ukusanyaji wa kumbukumbu za walipa kodi, wataalamu mbalimbali na NGO waliopo katika kijiji.


II. MAJUKUMU YA AFISA MTENDAJI WA KATA
(i) Atakuwa Mtendaji Mkuu wa Kata na kiungo cha Uongozi kwa Idara zote katika kata na atashughulikia masuala yote ya kata.

(ii) Atakuwa Mhamasishaji mkuu wa Umma katika mikakati mbalimbali ya uzalishaji, mali, kuondoa njaa na Umasikini.

(iii)Atakuwa ni Katibu wa kamati ya maendeleo ya kata.

(iv) Ataratibu na kusimamia upangaji wa shughuli za maendeleo ya kata, vijiji na vitongoji.

(v) Atatafsiri sera na kusimamia utekelezaji wa sheria ndogondogo katika Kata yake.Atamsaidia Mkurugenzi Kuratibuna kusimamia shughuli za Uchaguzi katika Kata.

(vi) Kumsaidia na kumwakilisha Mkurugenzi katika kusimamia maendeleo ya eneo lake.

(vii) Kusimamia utendaji kazi wa wataalamu na watendaji wengine katika ngazi ya Kata.

(viii) Kuratibu na kuandaa taarifa za utekelezaji na kuziwasilisha kwa mkurugenzi na nakala kwa Katibu Tarafa.

(ix) Atakuwa mwenyekiti katika vikao vya vinavyowahusisha wataalamu na watendaji wa vjiji, na NGO’S katika kata yake.

(x) Atakuwa Msimamizi na mratibu wa takwimu zote zinazokusanywa katika vijiji, vitongoji, na kata yake.


III. MAJUKUMU YA AFISA TARAFA
(a) Majukumu ya Afisa Tarafa Kwenye Mamlaka ya Serikali Kuu.

(i) Kumwakilisha na kumsaidia Mkuu wa Wilaya katika utekelezaji wa shughuli za Serikali Kuu katika Tarafa.

(ii) Kuandaa na kuratibu taarifa na ripoti zinazohusu masuala ya ulinzi na usalama ya kata kwenye tarafa yake na kuiwasilisha kwa Mkuu wa Wilaya.

(iii) Kuhamasisha na kuhimiza wananchi iliwashiriki kwenye shughuli za maendeleo kwenye Tarafa.

(iv) Kuwa kiungo kati ya Serikali kuu na Wananchi Katika Tarafa.

(v) Kuwa mlinzi wa amani katika eneo lake.

(vi) Kufuatilia na kuhimiza utekelezaji wa sera za Serikali katika eneo lake na kuhakikisha kuwa zinatekelezwa ipasavyo.

(vii) Kuratibu shughuli zote za maafa na dharura mbalimbali katika eneo lake.

(viii) Kuandaa taarifa zote zinazohusu masuala ya Serikali Kuu kuhusu utendaji wa kazi za maafisa Watendaji wa kata wa eneo lake na kuziwasilisha kwa Mkuu wa Wilaya.

(ix) Kuwa kiungo kati ya Serikali kuu na Serikali za Mitaa. katika eneo lake.

(x) Kufanya kazi zingine atakazopangiwa na Katibu Tawala wa Wilaya.

(b) Majukumu ya Afisa Tarafa Kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa;

(i) Kuwasaidia Wakurugenzi wa Serikali za Mitaa katika shughuli za Maendeleo katika eneo lake.

(ii) Kusimamia utendaji wa shughuli za Maafisa Watendaji wa Vijiji, Kata na Mitaa.

(iii)Kushiriki na kutoa ushauri katika upangaji wa mipango ya Maendeleo katika eneo lake.

(iv) Kuhudhuria vikao vya kamati za Halmashauri na Baraza la madiwani na kutoa ushauri.

(v) Kuandaa taarifa za utekelezaji wa kazi katika eneo lake kama zitakavyopokelewa kutoka kwa Watendaji wa Kata.

(vi) Kusimamia utekelezaji wa Sheria ndogondogo za Halmashauri ya Wilaya, Miji, Manispaa au Jiji.


IV. MAJUKUMU NA KAZI ZA DIWANI
(i) Kuwakilisha wananchi katika Halmashauri. Diwani huwakilisha wakazi wote wa Kata yake hivyo anatakiwa kuwa karibu na wapiga kura wake na kufikisha mbele ya Halmashauri na Kamati zake vipaumbele vya wananchi ili vijadiliwe na kutolewa maamuzi.

(ii) Kuhamasisha wananchi katika kulipa kodi na ushuru wa Halmashauri.

(iii) Kusimamia matumizi ya Fedha za Halmashauri. Diwani anatakiwa kuhakikisha Fedha za Halmashauri zinatumiwa kwa madhumuni yaliyokusudiwa na sio vinginevyo.

(iv) Kuwa kiungo kati ya Halmashauri na ngazi za msingi za Serikali za Mitaa. Diwani ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata. Atumie mamlaka hayo kuwasilisha kwenye Halmashauri maamuzi ya Kata yake na vile vile kuwasilisha kwenye Kata maamuzi ya Halmashauri.

(v) Kuhamasisha wananchi kuhusu vita dhidi ya umaskini. Katika kulitekeleza hili ni lazima ajue kwa ufasaha hali ya kiuchumi na kijamii inayowakabili wananchi wake na kushirikiana nao ili kupanga mipango endelevu ya kujikwamua.

(vi) Kufuatilia utekelezaji wa mipango yote ya wananchi na ya Halmashauri. Ili kutimiza jukumu hili ipasavyo, Diwani anatakiwa kufuatilia utekelezaji wa miradi yote ndani ya Kata yake ambalo ni jimbo lake la uchaguzi bila kudai malipo yoyote toka kwenye Halmashauri au wadau wengine. Kimsingi hii ndiyo kazi ambayo Diwani aliahidi kuitekeleza wakati wa kampeni.

(vii) Kutetea Maamuzi ya Halmashauri. Wakati wa majadiliano ndani ya Halmashauri, Diwani ataelekeza na kutetea maoni yake au ya wakazi wa eneo lake. Hata hivyo, iwapo uamuzi utakaofikiwa na wengi utakuwa kinyume na matarajio yake atalazimika kuunga mkono maamuzi ya wengi yaliyofikiwa kidemokrasia.
(viii) Kuzingatia misingi yote ya Utawala Bora wakati wa kutekeleza majukumu yote ya Udiwani.


V. MAJUKUMU NA KAZI ZA MEYA/MWENYEKITI WA HALMASHAURI
(i) Meya/Mwenyekiti wa Halmashauri ni Kiongozi Mkuu wa Halmashauri mwenye dhamana ya kisiasa. Dhamana hii humfanya kuwa kioo ndani na nje ya Halmashaui yake.

(ii) Meya/Mwenyekiti wa Halmashauri ni Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani na Kamati ya Kudumu ya Fedha na Mipango/Utawala.

(iii) Kwa mujibu wa Kifungu Na. 193 (2) cha Sheria Na. 7 ya 1982 na Kifungu Na. 108 (2) cha Sheria Na. 8 ya 1982, Meya/Mwenyekiti wa Halmashauri ni mtia lakiri/mhuri katika nyaraka zote rasmi za Halmashauri.

(iv) Meya/Mwenyekiti wa Halmashauri analo jukumu maalum la kudhibiti na kuongoza mikutano ya Baraza la Madiwani ili liweze kufanya maamuzi yenye maslahi kwa wananchi wote wa Halmashauri. Katika kutimiza jukumu hili Meya/Mwenyekiti wa Halmashauri anatakiwa kutenda haki kwa Madiwani wote bila kujali itikadi za Kisiasa, Jinsia, Dini, Rangi au Kabila na wakati wote awe mtulivu, imara na asiyeonyesha udhaifu wakati wa kuendesha vikao.

(v) Ili kutimiza wajibu wake wa Uongozi ipasavyo, Meya/Mwenyekiti wa Halmashauri anatakiwa kupewa Ofisi na Halmashauri ambayo ataitumia kukutana na wananchi wote wenye shida, kero na maoni ya kuboresha utendaji wa Halmashauri mara mbili kwa wiki. Ratiba ya siku hizi mbili lazima iwe wazi na ifahamike kwa wananchi wote. Aidha, Meya/Mwenyekiti wa Halmashauri kama atataka kutembelea Halmashauri yake katika harakati za kuhimiza maendeleo, atalazimika kufanya kazi hiyo katika siku hizo mbili tu zilizoruhusiwa na sio vinginevyo.

VI. MAJUKUMU NA KAZI ZA MWENYEKITI WA KIJIJI
(i) Atakuwa ndiye Mkuu wa Serikali ya Kijiji;

(ii) Atakuwa na wajibu wa kuitisha na kuongoza mikutano yote ya Halmashauri ya kijiji, pamoja na Mikutano Mikuu ya Kijiji. Lakini endapo Mwenyekiti hayupo katika mkutano wowote, wajumbe wa mkutano unaohusika wanaweza kuchagua Mwenyekiti wa muda wa mkutano huo;

(iii)Atakuwa mwakilishi wa kijiji kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata;

(iv) Atawahudumia kwa usawa wanakijiji wote, bila kujali tofauti za Kisiasa, Kijinsia au za Kidini;

(v) Atakuwa mfano wa uongozi bora na utendaji bora wa kazi, kwa kuwa na shughuli zake mwenyewe za kujitegemea, ambazo zaweza kuigwa na wanakijiji wenzake.

VII. MAJUKUMU NA KAZI ZA MWENYEKITI WA MTAA
(i) Kuwa Mwenyekiti wa Mikutano yote ya Kamati ya Mtaa na Mkutano wa Mtaa;

(ii) Kusuluhisha migogoro midogo midogo ambayo haistahili kuitisha mkutano wa Kamati ya Mtaa au kupelekwa kwenye Baraza la Kata au Mahakama;

(iii)Kuwa msemaji wa Mtaa;

(iv) Kuwaongoza na kuwahimiza Wakazi wa Mtaa washiriki shughuli za maendeleo, sherehe za Taifa, Mikutano ya hadhara itakayoandaliwa na Mtaa, Halmashauri ya Mji Manispaa au Jiji na Serikali;

(v) Kuwakilisha Mtaa kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata;

(vi) Kutekeleza kazi atakazopewa na Kamati ya Mtaa na Mkutano wa Mtaa na Kamati ya Maendeleo ya Kata;

(vii) Kusimamia utekelezaji wa kazi na Majukumu ya Kamati ya Mtaa;

(viii) Kusimamia utunzaji wa rejesta ya wakazi wote wa Mtaa.

VIII. MAJUKUMU NA KAZI ZA MWENYEKITI WA KITONGOJI
(i) Kutunza rejista ya wakazi wa kitongoji na nyaraka nyingine muhimu zinazohusu maendeleo ya kitongoji kwa jumla ikiwa ni pamoja na kumbukumbu za vizazi na vifo;

(ii) Kusimamia shughuli za ulinzi na usalama wa watu na mali zao waishio katika eneo lote la kitongoji;

(iii)Kuhamasisha ulipaji wa kodi na ushuru mbalimbali, kama utakavyoamuliwa na kuwekwa mara kwa mara na Halmashauri ya Kijiji, Wilaya, Mji, Manispaa au Jiji;

(iv) Kusimamia katika eneo lake suala zima la Hifadhi ya mazingira hususan vyanzo vya maji n.k.;

(v) Kusimamia suala la afya katika eneo lake ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa kampeni za afya za Kitaifa, Kimkoa au Kiwilaya dhidi ya magonjwa ya kuambukiza, na hasa, Vita dhidi ya UKIMWI;

(vi) Kusimamia utekelezaji wa kanuni za kilimo na ufugaji bora ili kuinua hali ya lishe na uchumi wa wakazi wa kitongoji;

(vii) Kufuatilia na kuhakikisha kuwa kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anapatiwa nafasi na kushirikiana na viongozi wa shule katika udhbiti utoro shuleni;

(viii) Kuhamasisha elimu ya watu wazima;

(ix) Kusimamia na kuwahamasisha wakazi wa kitongoji katika kutekeleza shughuli za kujitegemea;

(x) Kusuluhisha migogoro midogo midogo isiyostahili kushughulikiwa na Mabaraza ya Kata au Mahakama;

(xi) Kuwakilisha kitongoji katika Serikali ya Kijiji;

(xii) Kuwaongoza na kuwahamasisha wakazi wa kitongoji washiriki katika sherehe za Taifa na mikutano ya hadhara itakayoandaliwa na kuitwa na Serikali au Halmashauri;

(xiii) Kutekeleza kazi nyingine atakazopangiwa na Halmashauri ya Kijiji, Wilaya, Mji, Manispaa au Jiji.

IX. MAJUKUMU YA KATIBU TAWALA WA WILAYA.
(i) Kumshauri Mkuu wa Wilaya katika masuala yanayohusu ulinzi na usalama.

(ii) Kumshauri Mkuu wa Wilaya katika masuala yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya sherehe na dhifa za kitaifa.

(iii) Kumshauri Mkuu wa Wilaya katika masuala yanayohusu malalamiko ya wananchi.

(iv) Kumshauri Mkuu wa Wilaya katika masuala yanayohusu uwekaji wa mazingira bora ya kuziwezesha Halmashauri za Wilaya kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sera za serikali.

(v) Kuwa Kiongozi Mkuu wa Utawala katika ngazi ya Wilaya.

(vi) Kuwa Msajili wa Vizazi na Vifo.

(vii) Kuwa msajili wa ndoa.

(viii) Kuandaa makadirio ya matumizi ya Wilaya.

(ix) Ushughulikia masuala ya itifaki Wilayani.

(x) Kuratibu harakati za kupambanana dharura za maafa Wilayani.

(xi) Kutekeleza majukumu mengine kama atakavyoagizwa na Mkuu wa Wilaya na Katibu Tawala wa Mkoa.

X. MAJUKUMU YA MKUU WA WILAYA
(i) Kumweka mtu kizuizini kwa muda wa saa 48 mfululizo iwapo atashukiwa kuwa ni mhalifu au anayehatarisha hali ya utulivu na Amani (Sheria ya tawala za mikoa Na 19/1997).

(ii) Kufungisha ndoa za serikali (Law of Marriage Act No 5/1971).

(iii) Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, kuwa mwenyekiti wa Kamati yaMkoa inayochambua maombi ya watu wanaotaka kuuza madawa ya sumu (Pharmaceuticals and Poisons Act No 9/1978).

(iv) Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, kuongoza Kamati ya kusikiliza rufani za leseni za biashara mkoani (Business Licensing Authority Act No 25/1972, ib. 1).

(v) Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa ya leseni za vileo (Intoxicating Liquours Act No 28/1968)
(vi) Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, kuteua wakaguzi wa magereza (Prisons Act No 34/1967, ib. 100).

(vii) Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, kuwashughulikia watu wanaodhaniwa kuwa ni wachawi (Witchcraft Ordinance Cap 18).

(viii) Kuwa mhimili msaidizi wa Halmashauri za Wilaya (Sheria Na 7/1982).

(ix) Kuwa mwenyekiti wa Kamati mbalimbali zitakazoundwa Wilayani.

(x) Kuhudhuria vikao vya Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kamamjumbe.

(xi) Kushughulikia malalamiko ya wananchi na kuyapatia ufumbuzi.

(xii) Kumsaidia Mkuu wa Mkoa katika kuzisimamia Halmashauri za Wilaya na kuhakikisha kuwa zinatoa huduma nzuri kwa wananchi na kwa ufanisi

(xiii) Kuziwekea Halmashauri za Wilaya mazingira mazuri na kuhakikisha kuwa zinatekeleza majukumu yake kulingana na sera za serikali.

(xiv) Kutekeleza majukumu yote atakayopewa kisheria au kukasimiwa na Mkuu waMkoa.

XI. MAJUKUMU YA KATIBU TAWALA WA MKOA

(i) Kuratibu shughuli zote za utawala kwenye sekretariati ya mkoa

(ii) Kuwa mshauri mkuu wa mkuu wa mkoa katika masuala ya sharia,kanuni na taratibu za uendeshaji wa shughuli za serikali za mitaa.

(iii) Kuwa katibu wa Kamati ya ushauri ya mkoa (RCC)

(iv) Kuwa mkuu wa watumishi waserikali kuu katika mkoa

(v) Kushauri na kuratibu upangaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya serikali za mitaa

(vi) Kuwajibika kwa fedha zote zitakazopelekwa mkoani kwa ajili ya matumizi ya kawaida na mipango ya sekretariati ya mkoa na ofisi za wakuu wa wilaya

(vii) Kuwa afisa mhasibu wa fedha za serikali kuu mkoani

(viii) Kuwa mwenyekiti wa bodi za zabuni ya mkoa

(ix) Kuwa mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Utumishi serikalini (KAMUS)

(x) Kuwa mwenyekiti wa kamati ndogo ya wataalamu katika sekretariati ya mkoa na kamati nyingine zitakazotokea kwa dharura

(xi) Kupokea na kuchambua takwimu na taarifa za utekelezaji zinazotoka kwenye halmashauri na mashirika mbalimbali

(xii) Kufuatilia upatikanaji na usambazaji wa pembejeo na zana muhimu za kazi ikiwa ni pamoja na mahitaji mengine kama vile wataalamu na fedha

XII. MAJUKUMU YA MKUU WA MKOA

(i) Kusimamia utekelezaji wa kazi na shughuli zote za serikali ya Jamhuri ya Muungano katika mkoa aliokabidhiwa (Katiba 1977, ib. 61(4))

(ii) Kuwa mwenyekiti wa RCC inayotoa ushauri kuhusu masuala mbalimbali mkoani mwake (RAA No 19/1997).
(iii) Mhimili wa Halmashauri za wilaya (LG Finance Act No 9/1982)

(iv) Mhimili msaidizi wa Halmashauri za Miji iliyoko katika mkoa wake (LG (Urban Authorities) Act No 8/1982)

(v) Kumweka kizuizini kwa saa 48 mfululizo mtu anayehisiwa kuwa ni mhalifu au anayehatarisha hali ya utulivu naamani (Regional Admin Act No 19/1977)

(vi) Kuongoza Kamati ya Mkoa ya maombi ya leseni za magari (Motor Vehicles, Registrations, Acquisitions and Dispositions Act No 5/1972, ib 24(2))

(vii) Kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Mkoa inayoshughulikia uteuzi wa vijana wanaojiunga na jeshi la kujenga taifa (National Service Act No 16/1964)

(viii) Kuwa mwenyekiti wa Kamati yaMkoa inayochambua maombi ya watu wanaotaka kuuza madawa ya sumu (Pharmaceuticals and Poisons Act No 9/1978)

(ix) Kuongoza Kamati ya kusikiliza rufani za leseni za biashara mkoani (Business Licensing Authority Act No 25/1972, ib. 1)

(x) Kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa ya leseni za vileo (Intoxicating Liquours Act No 28/1968)

(xi) Kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Mkoa ya utoaji wa leseni za magari na uchukuzi (Transport Licensing Act No 1/1973)

(xii) Kuteua wakaguzi wa magereza (Prisons Act No 34/1967, ib. 100)

(xiii) Kuwa mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama mkoani kwake ili kuhakikisha kuwa kuna ulinzi na usalama mkoani wakati wote na kuishauri serikali ipasavyo (National Defence Act No 24 1966)

(xiv) Kuwashughulikia watu wanaodhaniwa kuwa ni wachawi (Witchcraft Ordinance Cap 18)

Hasta la victoria siempre
Kukata majina ya wapinzani ili vilaza was ccm wapite bila kupingwa in nani mhusika kama ilivyokua uchanguzi was serikali za mitaaawaka huu!??
 
Useme na mishahara wanalipwa sh. Ngapi, na pia kuna ambao hawalipwi mishahara na ho ndio wamehallishwa kuwa wezi na kusubiri elfu mbili za mihuri

Kumkoma nyani geradi
 
Waingezewe majukumu....
Wapokee Kadi za wananchi Wanaorudisha Kadi za Uanachama wa CCM
 
Back
Top Bottom