Yajue maficho ya Simu za Wizi

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Wakati wezi wa simu za mkononi wakiendelea kuwatesa wananchi, mafundi wa vifaa hivyo wametajwa kuwa kivuli cha kuwaficha wahalifu hao.

Mbinu kuu inayotumiwa na mafundi ni kuzibomoa simu hizo na kutumia sehemu zake kama vifaa vya kutengenezea zingine zilizo mbovu.

Kutokana na matumizi hayo, inaelezwa ndicho chanzo cha wizi, ambao awali ulidhibitiwa na polisi hivyo matukio kupungua.

Awali, kulikuwa na wimbi la wizi wa simu lililoanzia kwa wauzaji, mafundi na vibaka mitaani lakini usajili wa simu kwa alama za vidole ulipunguza kwa kiasi tatizo hilo.

Pia, kulikuwa na taarifa kutoka mikoa ya Kilimajaro, Arusha, Manyara na Tanga ikielezwa kugeuka lango la kuingiza bidhaa hizo kutoka nchi jirani na kuziuza kwa bei ndogo.

Inavyokuwa

Uchunguzi uliofanyika na gazeti hili umebaini wezi wa simu kwa sasa hawaziuzi kwa watumiaji moja kwa moja kama ilivyokuwa awali, ikiwa ni njia ya kukwepa mtego wa polisi.

Simu zinazoibwa hupelekwa kwa mafundi ambako hufunguliwa na kutolewa baadhi ya vifaa ambavyo hutumika kutengeneza nyingine na baadaye huuzwa kwa wateja.

“Polisi watalaumiwa bure lakini wizi unafanywa kitaalamu zaidi, vifaa vya simu moja vinagawanywa kwa simu zaidi ya tano sasa unawezaje kuikamata,” alisema Agnes Hamisi mmoja wa watu walioibiwa simu.

Anasema ndugu yake alimsaidia kutambua mfuniko wa simu yake baada ya kufungwa kwenye simu aliyopeleka kwa ajili ya matengenezo.

Anasema walinunua simu za aina moja na ndugu yake na ili kuzitofautisha kila mmoja aliweka alama. Siku chache baadaye yake iliibwa.

Anaeleza nduguye simu yake ilianguka kwenye kiti ikaharibika. “Akapeleka kwa fundi, alipofika kule alitengenezewa na alipoiangalia akaona mfuniko ni wa ile simu yangu. Akambana fundi ikabidi amuombe yaishe tu na alilazimika kulipa ili asimtaje aliyepeleka,” alisema.

Mkazi wa Mailimbili jijini Dodoma, Shuffah Idd anasema hivi karibuni aliibiwa simu na kutoa taarifa kituo cha polisi lakini hakufanikiwa kuipata licha ya kuambiwa alipie fedha kituoni.

Shuffah alisema askari walimwahidi simu ingeweza kupatikana kwa haraka lakini ilimchukua muda mrefu kufuatilia asipate majibu ya polisi licha ya juhudi walizofanya.

Alisema mifumo inayotumiwa na polisi si mibaya lakini wamezidiwa na wajanja wachache wa masuala ya ufundi ndiyo maana hali imekuwa tofauti.

“Lazima polisi wajiongeze kwa kwenda mbele ya hapa walipofikia, tunashindwa kupata vitu vyetu halafu lawama tunazielekeza kwao lakini kumbe wahusika wanakuwa na mbinu nyingi,” alisema Shuffah.

Mpango wa awali

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliwahi kutangaza mkakati wa kuwapatia elimu na kuwasajili mafundi simu wote ili wawe mabalozi wa kuzuia uhalifu.

Katika mpango huo, ilielezwa fundi ambaye angeweza kuchukua simu ya wizi na kuanza kuitengeneza, mfumo ungesoma moja kwa moja ikiwa mwenye simu alishatoa taarifa za kuibiwa, hivyo kusaidia kukamatwa kwa haraka.

Fundi simu

Jackson Lucian ambaye ni fundi simu katika Soko la Machinga jijini Dodoma anasema lawama wanazoelekezewa wakati mwingine zinaweza kuwa na ukweli ingawa si wote wanafanya hivyo.

Jackson anasema baadhi ya mafundi hawajiamini katika kazi yao, badala yake wanaishi kwa kutegemea vijana wanaokwapua simu za watu na kuwauzia kwa bei ndogo kama sehemu ya spea.

Alisema ujanja ambao unatumiwa na mafundi hao ni kuchukua aina moja ya simu kwa idadi ya zaidi ya tatu kisha hubadilisha vifaa na kuvichanganya jambo linalowapa ugumu polisi kuzitambua.

“Ndiyo maana tulisema mafundi tusajiliwe, hawa wachache wanatuharibia biashara, vijana wanafahamu maduka ya kupeleka vifaa hivyo. Mtu anaiba simu anaipeleka na wakati huo haiwezi kufunguliwa hadi ipatikane nyingine au zingine za aina ile ndipo inafumuliwa na kubadilishwa kisha zinauzwa kwa bei nzuri,” anasema Jackson.

Kwa upande wake, Joshua Otalu ambaye pia ni fundi katika Mji wa Babati alikiri kuwapo kwa mtindo huo akisema wakati mwingine hutumika bila kujua.

Joshua alisema baadhi ya watu wanafika kwao kwa ajili ya kutengeneza simu lakini huwa wamezikwapua, hivyo ikitokea kifaa kimojawapo kimeharibika upande mmoja huwa ni lazima wabadilishe.

Alikiri kukutana na tatizo hilo alipotengeneza simu mbili za wateja, alifuatwa na polisi na kuhojiwa baada ya mmoja kukiri aliwahi kubadilisha simu kwa mtindo huo.

Kuhusu polisi kutambua mbinu hiyo alisema itawachukua muda kwa kuwa kazi hufanywa kwa umakini.

Polisi wasema

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime alisema polisi hawana taarifa sahihi kuhusu mbinu hiyo na wataendelea kufuatilia kwa wataalamu wao ili waweze kung’amua.

Misime alisema kwa sasa hawezi kutoa majibu ya moja kwa moja kuhusu nini kinatakiwa kufanyika isipokuwa anachoweza ni kufuatilia kwa wataalamu wa mitandao ndani ya Jeshi la Polisi ili awe na uhakika wa atakachokieleza.

Walichosema TCRA

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hakupatikana kuzungumzia jambo hilo, lakini Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano wa mamlaka hiyo, Rolf Kibaja alisema walishatoa elimu kwa mafundi ili kuzuia wizi huo.

Kibaja alisema hana mamlaka zaidi ya kulisemea hilo huku akiomba mwandishi kuwasiliana na mamlaka kwa njia ya barua pepe (e-mail) ili aweze kujibiwa lakini akakiri walishaanza siku nyingi kutoa elimu.

“Naomba uandike e-mail kwa mkurugenzi na kueleza hilo swali lako, lakini kwa sasa ambacho natambua ni kuwa tulishaanza siku nyingi kutoa elimu kwa mafundi simu ili wawe mabalozi wa kukomesha hilo,” alisema Kibaja.

Mtaalamu wa masuala ya mawasiliano na teknolojia, anayefanya kazi Wizara ya Fedha aliyeomba hifadhi ya jina lake alisema kazi hiyo itakuwa ngumu kama TCRA hawatatumia mbinu mbadala kuwasaidia polisi.

Mtaalamu huyo alisema lawama katika mipango hiyo zinapaswa kuelekezwa kwa mamlaka hiyo na si polisi kwa madai hawawezi kutambua ikiwa hawana ujuzi na utaalamu zaidi.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom