Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,741
- 40,871
Ugomvi wa Kifikra: Mojawapo ya upotoshaji mkubwa uliotokea ni kuwaaminisha watu kuwa ipo haki fulani inaitwa "ya kupata habari live". Kwamba, usipopata habari "live" basi haki yako hiyo imevunjwa. Haki hii haipo mahali popote duniani, na haijawahi kutambuliwa na serikali yoyote duniani! Hakuna haki ya kupata habari "live"!
Ipo haki ya kupata na kutoa habari. Haki hii ni miongoni mwa haki za msingi za binadamu. Haki hii imeanishwa katika Azimio la Wote la Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Binadamu la 1948 (Kifungu cha 19) ambalo nchi nyingi duniani nazo zimeikubali.
Tanzania nayo inatambua haki hii na tumeiweka Katika Katiba yetu Ibara ya 18. Haki ya kupata habari ni haki ya msingi ya binadamu, kwamba huwezi kumnyima mtu habari. Ningekuwa miongoni mwa watu ambao wamekasirika na kuja kuu kama Serikali ya Magufuli ingedai au hata kupendekeza kuwa Watanzania wasiambiwe au wasisikie kinachotokea Bungeni. Ningeungana na wengine kupinga vikali endapo angesema kuwa Serikali imeamua kuwa kuanzia sasa habari za Bunge hazitawekwa wazi kwa wananchi. HIlo lingekuwa ni kuvunja Ibara ya 18 ya Katiba na kwenda kinyume na Azimio la Umoja wa Taifa la Haki za Binadamu ambayo Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoliridhia.
Kama Magufuli na Serikali yake wangekuja na pendekezo kama hilo nina uhakika kesi rahisi kabisa ya Kikatiba ingeweza kufunguliwa dhidi ya uamuzi huo na kwa asilimia 100 Serikali ingeshindwa.
Binafsi naamini ipo haki kubwa zaidi ambayo inatishia Watanzania kupata habari sahihi kutoka kwa wawakilishi wao Bungeni. Wabunge wamechaguliwa na wananchi kuwawakilisha Bungeni; nii ni pamoja na kushiriki mijadala, kutoa maoni, kusimamia serikali, lakini kubwa zaidi kutunga sheria na kubadilisha sheria mbalimbali. Mbunge ambaye haendi Bungeni, au ambaye anatoka Bungeni kwa sababu tu hajapenda uamuzi fulani wa Kiti cha Spika au kupinga maamuzi fulani ya kisiasa anawanyima wananchi waliomwakilisha kupata habari sahihi - kwani akija na kuulizwa kuhusu jambo ambalo yeye hakuwepo Bungeni hawezi kutoa habari sahihi na hivyo atakuwa anawanyima wananchi haki yao chini ya Ibara ya 18 ya Katiba na chini ya Azimio la UM la Haki za Binadamu.
Ndugu zangu, kama kuna sababu ya wabunge kulumbana na kucharuka ni kuhusiana na wao kutokuwepo “live” Bungeni wakati mijadala mbalimbali inafanyika na wao kutoa mawazo au kutoa hoja na kupendekeza Sheria au Mabadiliko ya Sheria mbalimbali Bungeni. Kuna faida gani kwa wananchi kuona kinachotokea Bungeni “live” kama wale waliowatuma huko Bungeni hawapo “Live”. Mwananchi wa jimbo fulani atafurahia nini kuona Bungeni kinachofanyika “live” wakati Mbunge wa jimbo lake hayupo “live” Bungeni?
Mwananchi ambaye anamuuliza Mbunge wake kuhusu suala fulani ambalo alitakiwa awe ametolea maoni nay eye hakuwepo “live” Bungeni atafaidika nini kuambiwa kuwa ameona jinsi watu walivyozungumza kwa ukali mambo ambayo yeye hayamgusi na mbunge wake hakuwepo Bungeni? Hili ndilo jambo hasa la kulizungumzia.
Binafsi, ningekuwa na uwezo nisingejali sana hili la kuona au kutoona “live”; ningejali zaidi kile kinachofanyika “live” Bungeni hata kama mimi mwenyewe sioni kwa macho! Kwa sababu macho siyo chombo cha kuaminiwa sana kwa kukupa taarifa sahihi; vinginevyo, mazingaombwe yangekuwa yanaamini ni ukweli. Kuona tu haitoshi; tunataka tujue nini kinafanywa na wabunge wetu Bungeni.
Lakini ningeenda mbali zaidi; na ninatumaini Serikali ya Mabadiliko ya J.P. Magufuli itakuja na mabadiliko ya sheria ambayo wabunge wote watafurahia ambayo yataweka adhabu kwa wabunge watoro Bungeni. Kama wafanyakazi wengine kwenye makampuni wanapewa kiasi tu (limited) cha siku ambazo anaweza kusema alikuwa mgonjwa wabunge nao wapewe siku (na zisizidi siku saba) kwa mwaka (ambapo kikao cha Bunge kinafanyika) ambapo ataweza kutoa udhuru kuwa hawezi kuwepo Bungeni. Isipokuwa kwa Mbunge ambaye yuko mahututi amelazwa au amepewa leave na Daktari kwa muda fulani. Wengine wote watatakiwa wawepo Bungeni au kwa kila siku, saa ambayo hawapo wakati vikao vya Bunge vinafanyika “live” watakatwa kwenye mishahara yao shilingi 50,000 kwa kila saa ambayo hawapo Bungeni au kwenye vikao ambavyo wanatakiwa wawepo. Hatutaki tuone Bunge “live” tunataka tujue wabunge wako “live” bungeni – mbele ya Luninga au hata nje ya luninga!
Nje ya hapo, ni lazima tukatae sanaa za maigizo ambazo zinajaribu kuwashikisha Watanzania wanasesere na kuwaambia waimbe “mtoto, mtoto!” na wengine kweli wanadakia “ni mtoto mtoto!” ati kwa vile mdoli huyo unafumba na kufumbua macho na unacheka kwa sauti zinazotokana na spika zinazoendeshwa na betri tumboni! Wakati wa kuwalazimisha Watanzania washike vipepeo na kuimba “uyoga uyoga” umepita! Tusiwafanye watu wetu waamini haki ambazo hazipo zipo na zile haki zenyewe za msingi wasijue kuwa zipo na wanatakiwa kuzidai!
Lakini kuna kubwa zaidi; kama kweli Wabunge wanataka kulazimisha kitu fulani kifanywe na chombo cha serikali ni wao wenye jukumu la kutunga sheria na kutenga fedha kwa chombo chochote cha serikali. Kama Nape ameona kuwa ni gharama kubwa kurusha vipindi “Live” badala ya kususa na kukasirika wabunge wanaweza hata kutoa hoja ya dharura ikajadiliwa Bungeni na kuamuliwa ili Serikali ipeleke fedha za ziada kwa TBC ili irushe Bunge live. Na hata Bunge likirushwa “live” masaa 24 – wabunge wawemo au viti tu vinavyozunguka zunguka – bado Watanzania watakuwa wanadai haki yao ya kuona wabunge wao wapo Bungeni “live” na wanashiriki ipasavyo kwenye mijadala muhimu na inayogusa maisha yao.
Mengine haya ni vipepeo na uyoga tu! Sidandii hata.
MMM