Calender
Senior Member
- Dec 28, 2015
- 112
- 84
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
Yamenikuta jana baada ya kunyofolewa ndani ya begi walinyakuwa iPad moja, Camera Nikon na Laptop!!
IMEBAINIKA kuwapo kwa wizi wa kutisha katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, huku magari ya Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji yakitajwa kwamba yamekuwa yakivusha vifaa vya wizi kutoka ndani ya uwanja huo. Wizi huo ambao umewasababishia hasara kubwa baadhi ya wasafiri wakiwamo wafanyabiashara, abiria wa kawaida na watalii wanaoingia nchini, unadaiwa kufanywa na baadhi ya wafanyakazi wa Wakala wa Mizigo wa Kampuni ya Swissport.
Wafanyakazi hao wamekuwa wakiiba vifaa na bidhaa kwa kuchana mabegi ya abiria kisha kuviweka kwenye makoti yao ya kazi lakini kwa mizigo mikubwa, wamekuwa wakiificha kwenye magari ya zimamoto ambayo huingia na kutoka ndani ya uwanja wa ndege bila kufanyiwa ukaguzi. Chanzo kingine cha habari katika uwanja huo kinasema magari ya zimamoto yanayofanya kazi katika uwanja huo hayakaguliwi yanapopita kwenye lango kuu, hivyo kutoa mwanya wa kuvushwa kwa mali za wizi. Mali zinazowekwa katika magari hayo ni zile kubwa ambazo hutakiwa kuuzwa nje ya uwanja wa ndege kama kontena la simu au mabegi makubwa ya nguo, kilisema chanzo hicho.
Baadhi ya waathirika wa wizi huo waliliambia gazeti hili kwamba wamepoteza mizigo mingi kwa nyakati tofauti na kupata hasara kubwa na kwamba uwanja huo si salama kwa wafanyabiashara hasa wanaoingiza bidhaa zao kutoka nje ya nchi. Chanzo chetu katika uwanja huo kilidokeza kuwa mara nyingi wizi hufanyika wakati mizigo inaposhushwa kutoka kwenye ndege kupelekwa eneo la kusubiri kuchukuliwa na abiria pia wakati mizigo mingine inapohifadhiwa kwenye stoo uwanjani hapo ikisubiri wahusika kuichukua. Wakati wanashusha mizigo kutoka kwenye ndege wanaikata kwa visu au viwembe vikali na kuchomoa chochote kilichomo kisha wanaweka katika makoti ya kazi ambayo yana mifuko mikubwa, kilieleza chanzo hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Swissport Tanzania, Gaudence Temu alikiri kuwapo kwa tatizo hilo lakini akasema kampuni yake kwa kushirikiana na wadau wengine uwanjani hapo wamekuwa wakichukua hatua za kudhibiti wizi huo. Huu wizi unaharibu sifa ya uwanja wa ndege wa kimataifa, ndiyo maana tukasema hatutakuwa na uvumilivu hata kidogo kwa wale ambao tunabaini kwamba wanafanya vitendo hivyo, alisema Temu.
Kamishna Msaidizi wa Zimamoto na Uokoaji, Sikiri Sala alisema amekwishazungumza na Kikosi cha Zimamoto Uwanja wa Ndege kuhusu suala hilo ambalo hata hivyo, alisema ni zito na linahitaji ushirikishwaji wa viongozi wote kwa kuwa uwanja huo una mashirika mengi. Wadau wengi wanapaswa kuzungumzia suala hili. Kuna polisi wa usalama uwanja wa ndege, kuna watu wa usalama, TAA (Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania) na kampuni za mizigo kama Swissport. Hawa wote wanatakiwa kufahamu suala hili kwa sababu lina uzito, alisema Sala. Alisema ni vigumu kwa wafanyakazi wa ngazi za chini kuzungumzia habari za wizi huo kwa kuwa hawatatoa ushirikiano na badala yake alisema viongozi wakuu wa mashirika yanayofanya kazi uwanja wa ndege watatakiwa kuzungumza. Alisema atafanya nao kazi kwa karibu ili kujua undani wa tuhuma hizo.
Mkurugenzi wa moja ya kampuni za ndege zinazotumia uwanja wa huo alisema yake imepata hasara kubwa kutokana na wizi huo. Kila siku ilikuwa ni lazima tuibiwe, wateja wetu walilalamika kuibiwa, mizigo mingi ilikuwa inapotea, yaani nina maana kila ndege inapotua lazima malalamiko yawepo, alisema. Mfanyabiashara wa simu katika eneo la Kariakoo, Aloyce Lyimo alisema aliwahi kuibiwa idadi kubwa ya simu za mkononi katika uwanja huo, Juni mwaka jana. Alisema alileta kontena mbili za simu mchanganyiko kutoka Japan na baada ya kutua uwanjani hapo, nyingi ziliibwa katika mazingira ya kutatanisha. Mzigo ulifika lakini tulipokwenda kuuchukua ulikuwa umepungua zaidi ya nusu, kuna wizi mkubwa sana hapo uwanjani na ni jambo linalotukera, aliongeza Lyimo.
Alisema hiyo si mara ya kwanza kuibiwa na kwamba wizi ni kilio cha wafanyabiashara wengi wanaopitisha mizigo yao kwenye uwanja huo. Pia imefahamika kuwa raia wengi wa kigeni hupoteza mizigo yao katika uwanja huo na wanapohoji huambiwa kuwa huenda imebaki Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro au Jomo Kenyatta, Nairobi, hadithi ambazo hudumu kwa miezi au mwaka bila mizigo husika kupatikana.
Raia wa Ufaransa, anayefanya biashara nchini, Tom Dyancov alisema mara nyingi anapotoka Ufaransa kuja nchini amekuwa akipoteza mabegi yake au kukuta yamevunjwa makufuli au yamechanwa. Karibu kila ninaposafiri kutoka Ufaransa kuja hapa, lazima niibiwe au begi zima lipotee. Wakati mwingine begi linachanwa kwa viwembe au wanavunja kufuli, alisema na kuongeza: Hakuna siku niliyoshuka bila kuwa na malalamiko.
Zinakouzwa bidhaa
Imebainika kuwa baadhi ya maduka yaliyomo ndani ya uwanja huo hutumika kwa kiasi kikubwa kununua mali zinazoibiwa. Maduka hayo yanadaiwa kusuka mipango na baadhi ya wafanyakazi wa Swissport ambao huwapelekea mizigo yote wanayoiba na ambao huuza mali hizo wakizinadi kuwa zimetumika kutoka Marekani, Dubai na Uingereza. Wakishaiba tu, wanachukua kama ni simu, kamera, saa, kompyuta na nguo na hata majarida halafu wanayapeleka kwenye maduka, kilisema chanzo chetu cha habari.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa moja ya duka linalouzwa bidhaa za vyakula katika uwanja huo, limekuwa likinunua bidhaa zinazoibwa. Mwandishi wetu alikwenda katika duka hilo na kuuliza iwapo kuna uwezekano wa kununua kompyuta ndogo (laptop) na kamera na mazungumzo na muuzaji yalikuwa hivi:
Mwandishi: Nahitaji laptop used (laptop iliyotumika) na kamera, naweza kuvipata hapa uwanjani mimi ni mgeni natokea Kenya.
Muuzaji:Hapa zipo laptop, kamera na simu lakini inategemea siku vikipatikana.
Mwandishi: Kwa nini mpaka vikipatikana? Kwani wewe si mfanyabiashara au na wewe unanunua?
Muuzaji: Kuna watu wanatuletea ndiyo maana nakuambia mpaka vikipatikana.
Mwandishi: Lini vitapatikana nije kununua?
Muuzaji: Sasa zimekuwa adimu kidogo lakini jaribu wiki ijayo, nitakuuzia kwa bei nafuu.
Mwandishi: Lakini hili duka linaonekana kama ni la vyakula pekee.
Muuzaji: Kama nilivyokuambia kuna watu wanaotoka nchi za nje ndiyo wanaotuletea.
Meneja Ulinzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Clemence Jingu alisema mamlaka hayo inahusika na usalama wa uwanja wa ndege na si mizigo. Alisema TAA inasimamia ulinzi wa uwanja, watu wanaoingia ndani ya uwanja, wanaokamatwa na dawa za kulevya au silaha na si vinginevyo na kwamba suala la mizigo linazihusu mamlaka nyingine ambazo hata hivyo, hakuzitaja.
Lakini Temu, alisema: Tumehakikisha tunaudhibiti wizi kwa njia zote, tumeshirikiana na wadau wote, TAA, Polisi na tunatumia teknolojia ya hali ya juu. Temu aliitaja mikakati mingine ya kumaliza wizi uwanjani hapo kuwa ni kuwafukuza kazi wafanyakazi wanaobainika kuhusika na wizi huo. Hata katika kuajiri hivi sasa tunaajiri wafanyakazi wenye sifa. Hizo ni pamoja na historia zao, hatuwezi kuajiri wafanyakazi ambao hawana maadili au wenye historia chafu, alisema. Alisema Swissport imeshirikiana na TAA kufunga kamera za CCTV katika kila idara ya mizigo ili kuangalia kila kinachoendelea ingawa alisema ni vigumu kusema kuwa wizi umekwisha kwa kuwa mizigo inapita kwenye mikono mingi. Hata hivyo, alisema changamoto wanayoipata ni pale abiria wanaposingizia kwamba wameibiwa mizigo ili walipwe fidia.