Uchungu ni kitu kinachoua mahusiano mengi iwe ni kifamilia, kihuduma na hata kindoa. Uchungu unaondoa ukaribu baina ya watu na kujenga ukuta wa uhasama. Kamwe uchungu usiachwe ukakua katika maisha yetu.
Uchungu unakuja na hasira, ghadhabu na kelele na matukano. Utakapoacha uchungu ukue ndani yako utaleta na yote hayo. Kwa wale wanaoamini katika Bibilia "Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya - Efeso 4:31.
Uchungu unakuja pale mtu anapokukosea na wewe ukaweka kinyongo ndani ya moyo wako. Uchungu unakuwa shina ndani yako kwa kukuonyesha kuwa uko sahihi kuwa na kinyongo kwa kosa ulilotendewa. Unapingana na dhamira yako inayokuambia sio sawa kuwa na kinyongo na mtu. Unajikuta unawaza jinsi mtu huyo alivyokukosea na kutokuona kosa ambalo unalifanya la kuweka kinyongo na kutokusamehe.
Again kwa wale wanaoamini katika Bibilia, "Mkiangalia sana mtu asiipunguke neema ya Mungu, shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo" - Ebrania 12:15. Katika mistari hii tunaona kuwa shina la uchungu linachupuka pale ambapo mtu anakuwa ameipungukia neema ya Mungu.
Mtu unapoacha kusamehe hapo ndipo unapoanzisha mizizi ya uchungu na kutokusamehe kutapelekea wewe kupungukiwa na neema ya Mungu. Unaposhindwa kusamehe wengine unakuwa unamwambia Mungu kuwa asikusamehe na ndipo unapopungukiwa na neema ya Mungu.
Unapokuwa na uchungu na mtu, sio nyie wawili tu mnao athirika bali na watu wote wanaowazunguka. Ndio maana kwa wale wanaoamini katika biblia inasema kuwa muangalie sana maana uchungu utasababisha watu wengi kutiwa unajisi sababu yenu. Shina la uchungu linachipuka kwenye mizizi ya kutosamehe, lazima ujifunze kusamehe hata kama mtu amekukosea kwa kukusudia.