RAIS Jakaya Kikwete amemteua Mbunge wa Mpanda Mashariki (CCM), Mizengo Kayanza Peter Pinda kuwa waziri mkuu mpya kuchukua nafasi ya Edward Lowassa aliyejiuzulu nafasi hiyo juzi.
Uteuzi huo ambao ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa, umewaacha watu wengi midomo wazi kwani waziri mkuu huyo mteule hakuwa miongoni mwa orodha ndefu ya watu waliokuwa wakitajwa kumrithi Lowassa, licha ya gazeti hili na gazeti dada la THISDAY kumtaja.
Katika barua yake jana kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Kikwete alisema kwamba amefanya uteuzi huo kwa kufuata Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 51 (2) toleo la mwaka 1977.
Wabunge 282 wa Bunge hilo walimpitisha Pinda kwa kura 279, wakati ambapo kura mbili zilimkataa na moja iliharibika. Ni ushindi wa kiwango cha asilimia 98.9.
Kabla ya uteuzi huo, Pinda alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu akishughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), na utendaji wake ulionekana tangu awali kuwaridhisha wengi.
Akizungumza kabla ya kuthibitishwa, Pinda ambaye alisema kwamba yeye ni mtoto wa mkulima tena mtoto wa kwanza, alisema kwamba nafasi hiyo ni kubwa lakini akamhakikishia kwamba angejitahidi kuitekeleza.
Pinda, ambaye ni mwanasheria kitaaluma aliyehitimu shahada Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974, alisema kwamba amekuwa Katibu Mkuu Msaidizi wa Rais Julius Nyerere kwa miaka saba tangu mwaka 1978 na kisha kuendelea na wadhifa huo katika miaka yote 10 ya awamu ya pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi kabla ya kuendelea tena kwa miaka mitano katika serikali ya awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa.
Mwaka 1995 aliwahi kuwania ubunge katika jimbo la Mpanda Mashariki lakini akashindwa katika kura za maoni. Hata hivyo, aliwania tena nafasi hiyo mwaka 2000 ambapo alifanikiwa kushinda na kutwaa tena jimbo hilo katika uchaguzi wa mwaka 2005.
"Mimi si mwanasiasa, lakini katika kipindi nilichokaa na wanasiasa wakongwe, nimeweza kujifunza mambo mengi, na hasa katika wizara hii kupitia kwa Ngwilizi (Hassan), Rais Kikwete (wakati akiwa waziri) pamoja na Lowassa (Edward) ambapo wizara yangu iko chini yake," alisema.
Alisema kwamba atahakikisha kwamba analinda misingi ya katiba na kujenga mshikamano miongoni mwa wabunge kwa maslahi ya Watanzania wote.
"Nitabadilika kimadaraka, lakini kihalisia nitaendelea kuwa Pinda yule yule
Ninachowaahidi ni kwamba, nitahakikisha nalifanya Bunge hili kuwa moja. Yanapokuja masuala ya maslahi ya taifa, Bunge lote liwe moja kama zilivyo nchi za wenzetu kama Israel na hata Marekani," alisema.
Aidha, baada ya kuapishwa, waziri mkuu mpya alisema, atajitahidi kusimamia na kudhibiti dalili zozote za maovu ndani ya serikali.
Pinda alisema kwamba yale yote yaliyotajwa na kupendekezwa na kamati teule ya Bunge kuhusiana na kashfa ya Richomond yanapaswa kufanyiwa kazi kwa msingi wa kuleta mabadiliko kwa maslahi ya taifa.
"Vyombo vya dola vimetajwa. Takukuru, polisi na kadhalika. Haya yote yanapaswa kushughulikiwa na nina hakika yakifanyiwa kazi kwa makini nina hakika tunaweza kufika kule tulikokusudia," alisema.
Aidha, alisema kwamba umoja ndani ya Bunge na serikali ndivyo vitu vitakavyoweza kujibu yale ambayo wananchi wanataka wafanyiwe.
"Hoja siyo vyama vingi, nadhani Bunge la Jamhuri ya Muungano linajitosheleza kwa sababu lina watu makini. Kwa hiyo hoja hapa ni kutekeleza masuala ya msingi kabisa ambayo wananchi wetu wametutuma kwa maslahi ya taifa," aliongeza.
Aliomba wabunge wote kushirikiana na kuheshimiana ili kuweza kuleta mabadiliko yenye manufaa kwa taifa.
Pinda alihimiza Watanzania wote kushirikiana kufichua maovu ili kujenga taifa lenye maendeleo.
Aliwataka watu kuondoa hisia kwamba kamati teule ilitoa mapendekezo kwa chuki na ubinafsi na kusema kwamba kamati hiyo ilitenda kazi yake kwa ukamilifu, huku akiahidi kwamba hata yeye ataweza kuwajibika ikiwa yatampata kama hayo.
Kuteuliwa kwa Pinda kumekuja kufuatia Rais Kikwete kulivunja Baraza la Mawaziri baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa kujiuzulu nafasi hiyo baada ya kuhusishwa katika ripoti yak amati teule ya Bunge kwamba alihusika katika mkataba wa Richmond na Tanesco.
Waliojiuzulu pamoja na Lowassa ni pamoja na waziri wa zamani wa wizara ya nishati na madini, Dk. Ibrahim Msabaha ambaye kwa sasa alikuwa waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pamoja na waziri wa sasa nishati na madini Nazir Mustafa Karamagi.
Mawaziri hao wote wametajwa kwamba walishiriki kwa kiasi kikubwa kuiingiza Tanzania kwenye mkataba mbovu wa Tanesco na Richmond, kampuni ya Marekani ambayo ilikuwa imepewa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura tangu mwaka 2006.
Hata hivyo, mkataba huo ambao ulihaulishwa kwa kampuni ya Dowans ya kutoka Arabuni, umeleta hasara kubwa kwa taifa ambapo Tanesco sasa imeongeza tarifu za umeme kwa asilimia 21.7 ili kuweza kulipa gharama za milioni 152/- kila siku kwa kampuni hizo za kigeni.
Zitto Kabwe, alipongeza kuteuliwa kwa Mizengo Pinda akisema kwamba ndiye aliyefanikisha mgogoro uliokuwa umejitokeza Kigoma baada ya uchaguzi mkuu kufikia kwenye muafaka wa kuunda halmashauri ya pamoja.
Kwa hali ilivyotokea, ingekuwa kwenye nchi nyingine, hali ingekuwa ya vurugu, lakini kwa misingi ya katiba, hali imeweza kuwa ya utulivu na Rais akafanya uteuzi wa msaidizi wake kwa kipindi muafaka, alisema Zitto.
Pinda ataapishwa leo na Rais Jakaya Kikwete saa 5 asubuhi mjini Dodoma.
Wakati huo huo, Spika Sitta jana alitangaza kuwa baraza jipya la mawaziri litatangazwa Jumatatu.
ends