Waziri Ngeleja aomba muda kuhusu kauli ya Dk Rashid

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,015
Date::3/9/2009
Waziri Ngeleja aomba muda kuhusu kauli ya Dk Rashid

Na Jackson Odoyo
Mwananchi

WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja amesema kuwa ni mapema mno kuzungumzia hatua ya mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco), Dk Idriss Rashid kujitoa kwa shirika hilo katika mpango wa kununua mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura ya Dowans, huku akionya kuwa asihukumiwe wakati nchi itakapoingia gizani.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini jana, Waziri Ngeleja alisema: "Jamani ni mapema mno kuzungumzia suala hilo.

"Mimi nilikuwa nje ya nchi ndiyo nimerudi hata ofisini sijakaa na kuangalia mambo hayo yanakwendaje... hivyo ninawaomba wananchi wanivumilie kidogo nipitie pitie kwanza baadhi ya nyaraka kisha nitawajulisha."


Alisema kuwa anafahamu namna ambavyo suala hilo lilivyopokelewa na kwamba kila mtu ana hamu ya kusikia kauli ya serikali, lakini akaongeza kuwa hawezi kulizungumzia kabla ya kujiandaa kwani hivi sasa haelewi pa kuanzia.

"Hili suala ni nyeti mno na linawagusa watu wote hivyo siwezi kutoa kauli yoyote kabla sijakutana na wataalamu wangu pamoja na watu wengine wanaohusika. Naomba nirudie tena kuwaomba wanahabari na wananchi kwa ujumla mnipe muda niweke mambo sawa na baadaye nitawaita," aliongeza Waziri Ngeleja.

Hata hivyo alipoulizwa kama alimruhusu Dk Rashid atangaze kuwa nchi itaingia gizani baada ya Tanesco kujitoa katika ununuzi wa mitambo hiyo, Ngeleja alisema: "Jamani nimeshasema kwamba yote nitazungumzia siku hiyo.

"Ninafahamu kwamba mna maswali mengi ya kuniuliza kuhusu suala hilo, lakini leo sitaweza kuzungumza chochote kwa sababu ninahitaji muda wa kuandaa taarifa ya kwenda kwa wananchi."

Waziri huyo wa nishati na madini alisema ingawa suala hilo ni nyeti, uamuzi ama kauli ya wizara yake ndiyo itakuwa kauli ya serikali, hivyo wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi mpaka atakapozungumzia suala hilo katika taarifa yake, akisisitiza kuwa ili aweze kutoa taarifa nzuri kwa wananchi anahitaji kujiandaa.

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iliishauri serikali isinunue mitambo hiyo kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma, inayokataza kununuliwa kwa vitu vilivyokwishatumika, lakini baadaye serikali ikawasilisha azma hiyo ya kuinunua kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, ambayo hata hivyo ilishindwa kufanya maamuzi.

Baada ya kukwama kwa mpango huo na majibizano makali baina ya watendaji wakuu wa Tanesco na wizara na wabunge, Dk Rashid alitangaza uamuzi huo wa kujitoa kwenye mpango wa kununua mitambo hiyo, kitu ambacho kimetafsiriwa kuwa cha kuingilia madaraka ya waziri mwenye dhamana na nishati na madini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, William Shelukindo alikaririwa jana akisema kuwa kitendo cha Dk Rashid ni utovu wa nidhamu na anastahili kuchukuliwa hatua kwa kutangaza uamuzi wa serikali. Shellukindo alisema Waziri Ngeleja ataitwa ili ahojiwe na kamati yake kujua kama alimpa Dk Rashid ridhaa ya kutangaza uamuzi huo.
 
Back
Top Bottom