Waziri Mwigulu awaagiza TRA kuweka mabango mipakani

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ameiagiza Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) kuweka mabango hasa katika maeneo ya mipakani mwa nchi jirani kuelezea bidhaa ambazo zinapaswa kutozwa ushuru na zisizotakiwa kutozwa.

Mwigulu ametoa agizo hilo leo Septemba 11, 2022 katika mji wa Sirari baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa viongozi mbalimbali wa kisiasa kuhusu hali ya biashara katika mji huo uliopo mpakani mwa Tanzania na Kenya.

"Nawaagiza TRA muweke mabango mipakani mara moja kuelezea bidhaa zinazopaswa kulipiwa na zile ambazo hazitakiwi kulipiwa ili kuondoa mkanganyiko uliopo sasa kwani malalamiko yamekuwa mengi, yawezekana kuna upande hautimizi wajibu wake" amesema.

Amesema kuwa ni lazima wananchi wajue utaratibu unaotakiwa kufuatwa wakati wanaponunua vitu kutoka nchi jirani kwani wapo wengine ambao wamekuwa wakijikuta katika wakati mgumu huku wakiwa wamebeba bidhaa ambazo hazipaswi kulipiwa ushuru.

"Utakuta mtu anakimbizwa na askari kumbe kile alichokibeba hata hakitakiwi kulipiwa chochote sasa mkiweka hayo mabango itasadia kuondokana na huu usumbufu"amesema.

Pia, ameitwaka mamlaka hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kiwango cha bidhaa ambacho kinatakiwa kutozwa ushuru ili kuondoa usumbufu hasa kwa wale wanaonunua hidhaa chache kutoka nchi jirani kwaajili ya matumizi binafsi na sio biashara.

"Mtu anajenga nyumba yake halafu anaona kuna bati hapo nchi jirani ambazo zina bei nafuu na anaamua kwenda kununua huko hili sio kosa na huyu ni tofauati na yule anayeagiza mzigo mkubwa kwaajili ya biashara " amesema.

Amesema kuwa yapo malalamiko ambayo ameyapokea yanayohitaji utekelezaji kwa misingi ya kisheria na utaratibu na kuahidi kuwa atakutana na wataalamu kwenye wizara yake ili kuona namna ya kufanya.

Dk Mwigulu pia amewaonya watu ambao wamekuwa wakifanya magendo na kubuni mbinu za kukwepa kodi kila mara na kwamba watu wa aina hiyo lazima sheria itachukua mkondo wake dhidi yao.

Pia amezitaka mamlaka zinazohusika kuheshimu watu ambao wamejiajiri akisema kuwa watu hao wanatakiwa kusaidiwa ili wafike mbali.

"Kuna watu wangu ambao hawajawahi hata kuuza nyanya kwahiyo hawajui magumu wanayopitia watu wengine na wao kazi yao ni kuwasumbua tu ndio maana unakuta wanafikia hatua hata ya kupiga teke bidhaa za hawa watu sasa sitaki kusikia hicho kitu nataka muwape ushirikiano ili waweze kuwa wafanyabishara wakubwa watakaoongeza nafasi za ajira kupitia sekta binafsi" amesema.

Awali, mbunge wa viti maalum mkoa wa Mara, Ghati Chomete alidai kuwa mazingira ya ufanyaji biashara hasa kwa wafanyabishara wadogo katika mji huo wa Sirari ni magumu kutokana na kamata kamata inayofanywa na askari polisi kwa kushirikiana na TRA.

Amesema kuwa vijana wa bodaboda nao wamekuwa wakisumbuliwa na TRA na askari polisi pale wanapokuwa wamapatikana wakiwa wamebeba mifuko hata miwili ya saruji jambo ambalo amedai kuwa sio utaraibu.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom