Waziri Mkuu awataka madereva wa Serikali wazingatie sheria

Ojuolegbha

JF-Expert Member
Sep 6, 2020
738
478
- Asisitiza kuwa ukiwa dereva wa Serikali haimaanishi uko juu ya sheria

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka madereva wa Serikali kuwa mfano wa kuzingatia sheria zote kwa sababu kuendesha gari ya Serikali haimaanishi wamepewa rungu la kuvunja sheria bali wanapaswa kuwa mfano wa kuzizingatia hasa zile za usalama barabarani.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa, “ukiwa dereva wa Serikali haimaanishi kuwa uko juu ya sheria bali kila dereva anatakiwa kuwa mfano wa kuzingatia sheria zote. Aidha, madereva wa vyombo visivyo vya Serikali wanapaswa kujifunza kutoka kwenu madereva wa Serikali.”

Pia, Waziri Mkuu amesema madereva hao wanapaswa kufanya kazi kwa kufuata maadili ya taaluma ya madereva wa Serikali ambayo yanawataka madereva hao kuzingatia na kutii sheria za usalama barabarani. “Madereva wa Serikali hakikisheni mnakuwa kioo cha jamii.”

Ameyasema hayo Jumanne, Oktoba 24, 2023 alipofungua Kongamano la Chama cha Madereva wa Serikali, katika Ukumbi wa Hoteli ya Morena mkoani Morogoro. Kongamano hilo limebeba kauli mbiu isemayo; “Dereva wa Serikali bila ajali inawezekana. Kazi iendelee”

Akizungumzia kauli mbiu hiyo, Waziri Mkuu amesema ni kweli inawezekana kuendesha magari ya Serikali bila kusababisha ajali iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake kwa kuzingatia sheria zilizopo, hivyo amewasisitiza madereva hao wahakikishe wanafuata sheria.

“Ninawapongeza sana kwa kuwa kaulimbiu hii pia ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020/2025, Ibara ya 105 (K) ambayo inailekeza Serikali kuliwezesha Jeshi la Polisi pamoja na mambo mengine kuendelea na jukumu la kudhibiti ajali za barabarani.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeshafanya jitihada kubwa katika kutatua kero za watumishi wa kada hiyo ya udereva na bado inaendelea kuzitatua changamoto zinazojitokeza kwa kushirikiana na Chama chao.

Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara zenye dhamana husika bila kuathiri shughuli na majukumu yake ya kila siku ya kiutumishi, imebadilisha muundo wa ajira na kuondoa kigezo cha cheti cha ufundi (trade test) katika kuwapandisha madaraja na ngazi za mshahara kwa mwaka wa fedha uliopita.

Waziri Mkuu amewahakikishia madereva hao kuwa, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya awamu ya tisa inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi zinaendelea kutekeleza azma yake ya kulinda maslahi ya madereva wa Serikali pamoja na kuyafanyia kazi maombi na ushauri utakaotolewa.

Naye, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewahakikishia madereva hao kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kupitia Chama Cha Madereva wa Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuongeza tija katika utendaji kazi Serikalini.

Pia, Waziri Bashungwa amesema suala la stahiki za madereva linapewa msisitizo mkubwa na Serikali. Kama ilivyoelekezwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, waajiri wote wahahakikishe kuwa madereva wote wanapatiwa barua za kuthibitishwa hususan kwa wale ambao bado hawajapewa barua hizo.
IMG-20231024-WA0018.jpg
IMG-20231024-WA0017.jpg
IMG-20231024-WA0014.jpg
IMG-20231024-WA0012.jpg
IMG-20231024-WA0010.jpg
 
Back
Top Bottom