Waziri Lukuvi afuta waraka unaokataza madiwani kuidhinisha mipango ya uendelezaji miji

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,011
9,879
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amefuta waraka namba moja unaowaondoa madiwani kushiriki katika shughuli za uidhinishaji mipango ya uendelezaji miji katika halmashauri zao uliotolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi nchini.

Kabla ya kutolewa waraka huo mpya Madiwani kupitia kamati zao za mipango miji walikuwa ndiyo wenye mamlaka ya kubariki mipango ya uendelezaji miji kwenye halmashauri kupitia vikao vyao vya robo mwaka na waraka mpya unataka shughuli hizo sasa kufanywa na wataalamu wa mipango miji kwa kushirikisha sekta mbalimbali kama vile sekta za maji, barabara na umeme.

Lukuvi alifanya maamuzi hayo tarehe 1 Juni 2021 katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Meru wakati akizingumza na madiwani wa halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kusikiliza na kuitafutia ufumbuzi kero za ardhi katika mkoa wa Arusha.

Alisema, kwa sasa waraka huo ameufuta mpaka utakapotolewa mwingine wenye maelekezo yatakayokuwa na tija na kusisitiza kuwa, haiwezekani kuwaondoa madiwani kupitisha mipango ya uendelezaji miji kwenyea halmashauri zake kwa kuwa mamlaka ya upangaji bado ziko chini halmashauri.

"Nimeamua kuufuta waraka namba moja unaokataza madiwani kupanga mipango ya uendelezaji miji katika halmashauri zenu, huwezi kuwa na halmashauri inayoshindwa kupitisha au kubariki mipango ya wilaya katika matumizi ya ardhi" alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, wataalam wa mipango miji katika ofisi za ardhi za mikoa waendelee kuwa washauri kwa kamati za mipango miji katika mabaraza ya madiwani.

"kama vibali vya ujenzi tuliwaondolea na kupanga pia tuwaondoe, mtafanya kazi gani ? hiyo haiwezekani, kwa sasa muongozo unaokuja kamati za madiwani zitapatiwa ufafanuzi wa namna bora ya matumizi ya ardhi na baadaye kupelekwa kwa maafisa mipango miji.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ametangaza kufutwa kwa shamba la Valeska lenye ukubwa wa ekari 4,087 katika halmashauri ya wilaya ya Meru mkoani Arusha.

Lukuvi alitangaza uamuzi huo baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kufuta shamba hilo kufuatia kuombwa kufanya hivyo na Waziri wa Ardhi kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema halmashauri ya wilaya ya Meru itawajibika kulipa fidia katika maeneo yanayohitaji fidia ambapo kwa mara ya mwisho fidia ya shamba katika eneo hilo ilikuwa milioni 394.10.

Waziri Lukuvi alianisha matumizi ya shamba lililofutwa kuwa ni ekari 1500 kugawiwa kwa vijiji vitatu vya Kwaugoro, Valeska na Maloloni na kuongeza kuwa ekari 1028 zitatumika kwa shughuli za kilimo huku ekari 1559 ikibaki kwa matumizi mbalimbali kama vile makazi na biashara.
 
Back
Top Bottom