Waziri Kangi Lugola Umewahi Kuisoma Makala ya RaiaMwema? Inakuhusu

Bazazi

JF-Expert Member
Aug 18, 2008
2,806
3,476
*IGP Mgaya: Bila kujitegemea tutauza mpaka Ikulu*

DEC 04, 2014
by RAIA MWEMA in HABARI

HIVI karibuni, LIVINGSTONE RUHERE, alifanya mahojiano na aliyepata kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Philemon Mgaya, ambaye pia alipata kuwa msaidizi (ADC) wa Mwalimu Julius Nyerere. Yafuatayo ndiyo yaliyojitokeza kwenye mahojiano hayo. Endelea

Raia Mwema: Huyu Philemon Nathaniel Mgaya, Mkuu wa zamani wa Jeshi la Polisi (IGP) ametoka wapi?

Mgaya: Nilizaliwa Novemba mosi, mwaka 1929, katika kijiji cha Usangi, sasa Wilaya ya Mwanga. Nilianza Shule ya Msingi mwaka 1939. Ni Shule ya Msingi Usangi. Nilisoma pale darasa la kwanza hadi la nne, baadaye nikachukuliwa na kaka yangu ambaye alikuwa Mwalimu Shule ya Msingi Ilembula, Mbeya, anaitwa Philip Nathaniel Mgaya.

Nikasoma Ilembula lakini ikaonekana kwamba pale nitapoteza muda kwa sababu ilikuwa ni village school (shule ya kijiji) kwa hiyo nikaenda kusoma Iringa, darasa la tano na la sita, baada ya hapo nikaingia Malangali Sekondari mwaka 1947 hadi mwaka 1951. Baadaye nikaenda Tabora School darasa la 11 na 12, niliondoka pale mwaka 1953.

Nikaenda kuchukua kozi ya Survey, Nakawa Technical College Kampala – Uganda. Niliporudi mwaka 1955 nikaajiriwa na Wizara ya Ujenzi kama Surveyer. Nilifanya kazi hiyo Ikwiriri – Rufiji, halafu Morogoro – barabara ya Morogoro Iringa, nilipokuwa kule ndipo nikashawishika kuingia Jeshi la Polisi.

Nilikwenda kozi ya polisi mwaka 1956 Chuo cha Mafunzo ya Polisi (CCP) Moshi mpaka nadhani ilikuwa Aprili, mwaka 1957 nilipomaliza kozi ya Sub Inspector nikapangiwa kazi Railway Police Dar es Salaam (Polisi Kitengo cha Reli) kutoka pale nikapelekwa Oysterbay (Dar es Salaam) kuwa OCS (ambaye ni OCD) nilichukua nafasi ya mzungu, namkumbuka kwa jina moja la Mr. Mofat.

Baada ya hapo nilipelekwa kuwa Deputy Regional Police Commander chini ya Bundugu aliyekuwa RPC, kwa takriban mwaka mmoja.

Nilipotoka hapo nikapelekwa kuwa RPC Tabora, kutoka Tabora nikapelekwa Morogoro halafu Dodoma. Nakumbuka Dodoma nilikaa mwaka 1966 na baada ya hapo nikateuliwa kwenda kuwa ADC wa Mwalimu Julius Nyerere.

Raia Mwema: Hii kazi ya ADC nini majukumu yake?

Mgaya: Kazi ya ADC watu wengi wanaichanganya wanadhani ni mlinzi wa Rais, lakini kazi ya ADC kimsingi ni ceremonial. Mnapokwenda mahali unavaa sare, kwa kawaida kama Rais anatoa hotuba unasimama nyuma yake. Rais anao walinzi wake lakini si kwamba kama jambo lolote litatokea wewe utakaa tu, kuna namna ya kudhibiti mambo vile vile.

Raia Mwema: Hao walinzi wanakuwa chini ya mamlaka yako kama ADC?

Mgaya: Walinzi wa Rais wanatoka Idara ya Usalama wa Taifa, ADC anatoka jeshini. Walinzi wanakuwa na mkubwa wao.

Raia Mwema: Kama ADC wajibu wako mkuu ni nini?

Mgaya: Nilipofanya mimi wakati ule, kama Mwalimu anasafiri unahakikisha kwamba unajua mnaenda kwa mfano, Ulaya ujue kwamba kule atavaa nini. Kwa mfano, Ulaya kuna baridi ni wajibu wako kuhakikisha Rais mavazi yake yaandaliwe vizuri yatakayokidhi hali ya hewa na unajua kwamba kule ataalikwa sehemu nyingi, kwa hiyo lazima uhakikishe unachukua nguo nyingi atakazozivaa kwa nyakati tofauti.

Ni wajibu wako ujue ratiba yake ili kumkumbusha. Kabla ya muda unamueleza, kwa mfano, saa tano tunatakiwa kwenda mahali fulani. Kwa hiyo ni kusimamia ratiba yake. ndiyo jukumu kubwa.

Raia Mwema: Ulikaa muda gani ukiwa ADC wa Mwalmu Nyerere?

Mgaya: Niliingia Ikulu mwaka 1966 hadi mwaka 1971 ndiyo Mwalimu akaniteua kuwa RC Tabora.

Raia Mwema: Tueleza zaidi kuhusu uteuzi wako katika nafasi ya ADC.

Mgaya: Mpaka nilipopewa huo wadhifa wa ADC wa Rais, ma-ADC wote walionitangulia walikuwa wanatoka Polisi. Mimi nilichukua kutoka kwa Francis lakini ADC wa kwanza baada ya uhuru alikuwa Melkzedeck naye kutoka Jeshi la Polisi.

Raia Mwema: Kazi ya ADC haina mafunzo maalumu?

Mgaya: Haina mafunzo maalumu, ni uzoefu wa kijeshi tu. Kabla ya kwenda kuwa ADC nilikuwa nimekwishafanya kozi Ulaya mara mbili. Safari ya kwanza nilipelekwa Uingereza kwenye kozi ya ofisa wakati huo nilikuwa inspekta. Safari ya pili nilipekwa Ulaya huko huko kwa kozi ya uafisa mwandamizi.

Baada ya mimi kutoka ADC waliofutia walichukuliwa kutoka jeshini na mpaka sasa ma-ADC wote wanatoka Jeshi la Ulinzi. Sijui kwa nini wamebadilisha. Hata kwenye nchi nyingine naona iko hivyo.

Raia Mwema: Ulikuwa na misa ya shukrani kutimiza miaka 85 hivi karibuni. Unazungumziaje hilo?

Mgaya: Hii ni mara ya kwanza nafanya misa kanisani kumshukuru Mungu kutimiza miaka 85. Sikuwahi kufanya kabla. Nimeona ni jambo la busara kumshukuru Mungu.

Raia Mwema: Ulijisikiaje?

Mgaya: Kwa kweli pale kanisani siku hiyo nilijisikia furaha sana, nilifarijika sana kwa maombi yaliyofanywa kwangu na kuimbiwa wimbo wa happy-birthday.

Raia Mwema: Unajua wewe ndiye shuhuda namba moja katika matembezi ya Musoma – Mwanza kuunga mkono Azimio la Arusha. Ilikuwaje?

Mgaya: Kwa kweli hakuna aliyejua kwamba tutafanya hiyo safari. Tuliondoka hapa (Dar es Salaam) na Mwalimu Nyerere tukaenda Butiama. Ilikuwa kawaida kwa Mwalimu kwenda Butiama kwa ajili ya mapumziko.

Basi siku moja usiku akaniambia kesho nataka tuanze safari ya kutembea kwa miguu kwenda Mwanza kama tukiweza na kama tukishindwa tutapumzika. Usiku huo huo nikaanza kupiga simu kwa viongozi mbalimbali, watu wa usalama na wengine kwamba kesho Mwalimu anataka kufanya matembezi. Kesho yake tukaanza safari.

Tulihangaika sana usiku huo kutafuta nguo za Mwalimu za kuvaa safarini kwenye matembezi na hata viatu. Siku ya kwanza tulitoka Butiama mpaka Kyabakari. Tulianza safari saa 12 asubuhi, lakini tulilala hapo Kyabakari na tulitembea barabara kuu.

Raia Mwema: Iliwachukua muda gani?

Mgaya: Ilichukua kama siku saba kufika Mwanza, ni umbali wa zaidi ya kilomita 100. Ilikuwa safari ngumu, wote tulipata madhara, michubuko miguuni, wengine walishindwa ikabidi waingie kwenye magari. Namkumbuka kama Bhoke Munanka, alijitahidi lakini aliishia katikati ikabidi apande gari.

Kila mtu alichoka. Mimi na hata Mwalimu, mfano mmoja ni kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa amebeba kisu kidogo hivi alikuwa amekiweka mfukoni lakini alikiona kizito.

Raia Mwema: Najua ulikuwa unasikia mazungumzo mengi ya Mwalimu na viongozi mbalimbali kuhusu harakati za ukombozi. Mfano, mazungumzo ya Mwalimu na Uingereza kuhusu Rhodesia. Unaweza kueleza nini kuhusu hili?

Mgaya: Mimi sikuhusika kwenye mazungumzo lakini wakati fulani Mwalimu aliwahi kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu mmoja anaitwa Edward, walitofautiana sana.

Nadhani Mwalimu alitaka Waingereza wasaidie kushinikiza Ian Smith atoke Rhodesia. Walikuwa wanafanya kiburi, walikuwa hawaoni umuhimu wa kumshauri Smith atoke. Walikuwa na maslahi Rhodesia, kutawala kuna raha yake.

Sisi kama Taifa tulitambua madhara kuendelea kwa ukoloni katika nchi nyingine, tulipeleka majeshi yetu Rhodesia kusaidia wapigania uhuru na kwa kweli wapigania uhuru wengi makao makuu yao yalikuwa Dar es Salaam.

Wapiganaji walikuwa wanavuka mipaka kupitia sehemu za kusini hadi Rhodesia. Serikali yetu ilikuwa ikitoa ruksa. Tulipambana kimkakati na kwa mafanikio.

Raia Mwema: Unadhanai ingekuwa leo tungefanya hivyo?

Mgaya: Nadhani tungefanya, hata juzi juzi hapa tulipeleka askari Comoro kusaidia.

Raia Mwema: Unakumbuka nini kikubwa ukiwa Ikulu nyakati za ukombozi?

Mgaya: Sikumbuki tukio kubwa. Ni kwamba ukombozi ulimhusu kila mtu, Watanzania wengi walijua tuko katika hali ya kupigana. Japo vita haikupiganwa Tanzania lakini ni kama nchi ilikuwa vitani.

Raia Mwema: Uingereza walikuwa na askari lakini pia baadhi ya askari wetu walipata mafunzo huko. Je, hawakuwa wakitumika kufanya hujuma?

Mgaya: Hapana, hiyo haikuwapo. Hapakuwa na kibaraka yeyote. Kiwango cha uzalendo kilikuwa kikubwa sana.

Raia Mwema: Mwaka 1971 walikupeka Tabora kuwa RC kutoka Ikulu. Changamoto gani ulizipata?

Mgaya: Kwa miaka niliyokuwa na Mwalimu kama ADC wake nilipata uzoefu wa kufanya kazi za kisiasa na wakati huo ndiyo ilikuwa Operesheni Vijiji.

Changamoto iliyokuwapo ni kuwaweka watu katika vijiji, ndiyo ilikuwa kazi kubwa wakati huo. Operesheni Vijiji haikuwa tu kukusanya watu bali kufanya watu hao wafanye kazi kwa pamoja. Msisitizo uliokuwa watu walime kwa pamoja, washirikiane kwenye shughuli zao za kila siku.

Raia Mwema: Unadhani Operesheni Vijiji lilikuwa wazo zuri?

Mgaya: Kwamba ni wazo zuri zaidi sijui, lakini iliwafanya watu kufanya kazi zaidi kwa sababu usingeweza kuacha kulima na wenzako halafu ukavuna. Kwa hiyo kila mmoja alikuwa akifanya kazi.

Raia Mwema: Lakini utekeleaji kwa ujumla wake haukufanikiwa. Kwa nini?

Mgaya: Kuna mambo ambayo kama yangesimamiwa vizuri tungekuwa mbali sana. Hata Azimio la Arusha lilikuwa bora. Kwa mfano, tulichukua benki, viwanda lakini kwa uzembe wetu tukaacha na vitu vingine vimekufa, uzembe wa kutosimamia vizuri. Kwa hiyo Azimio la Arusha lilikuwa na uzuri wake.

Mameneja walizembea katika usimamizi wa rasilimali hizo, viwanda vingi vikafa. Leo tunazo sera nyingine za uchumi.

Raia Mwema: Katika uongozi wako Tabora ukiwa Mkuu wa Mkoa, umeacha kumbukumbu gani?

Mgaya: Mimi na wenzangu, kama marehemu Fulgence Kazaura alikuwa RDD tulifanya kazi sana. Nakumbuka tulisimamia kilimo, Mwalimu Nyerere siku moja alikuja kututembelea tukampeleka sehemu moja, inaitwa Igagala, kulikuwa na kilimo cha mahindi, alipofika hapo akapanda juu ya Landrover hakuweza kuona mwisho (wa shamba).

Mwalimu akasema hivi; “…ningekuwa na ma-regional kamishna watano namna hii ningekwenda Ufaransa kupumzika. Igagala ni kijji tulichoanzisha tukakisimamia wananchi walilima mashamba mazuri na makubwa.

Raia Mwema: Kutoka Tabora ukawa IGP, hali ilikuwaje?

Mgaya: *Tabora nilikaa miaka mitano kuanzia 1971 hadi 1975 nikiwa RC. Katikati ya 1975 nilikuwa IGP. Baada ya kuteuliwa IGP Mwalimu aliniagiza kwamba Jeshi la Polisi lazima lisafishwe. Kusafishwa maana yake kutoa maofisa au maaskari kwa ujumla ambao hawafai. Hawafanyi kazi sawa sawa.*

*Kwa hiyo aliniambia nisaidiane na Joseph Butiku, Private Secretary wa Mwalimu pamoja na Hassy Kitine huyu alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa. Kwa hiyo tukatazama mafaili yote ya jeshi zima, watu tulioridhika hawafai kubaki jeshini tukawatoa na kazi hiyo ilihusisha askari wa kawaida mpaka maofisa.*

Raia Mwema: Unadhani hata sasa Jeshi la Polisi linahitaji kusafishwa?

Mgaya: Kwa maoni yangu nadhani hilo lingefanyika kwa sasa. Niseme tu wakati wangu kama rushwa ilikuwapo kwenye Jeshi la Polisi ilikuwa ni ya watu wa kuhesabu, mmoja …wawili…watatu, sitaki kuliponda Jeshi la Polisi lakini sasa hivi wapo wengi wanachukua rushwa.

Raia Mwema: Umekuwa kiongozi kwa ngazi mbalimbali. Nadhani utakuwa na mali nyingi sana. Maana leo watu wa aina yako ni matajiri. Unajilinganishaje na hawa?

Mgaya: Sina. Hili banda (nyumba) niliijenga kwa nguvu zangu bila mkopo kwa sababu nilikuwa nimepewa kiwanja eneo la Pugu Road ambalo ni eneo maalumu kwa ajili ya viwanda. Mimi nikaona sitaweza kujenga kiwanda nikauza kiwanja kisha pesa nikawekeza na baadaye kujenga nyumba hii.

Raia Mwema: Unazungumziaje mwelekeo wa nchi kwa sasa ukilinganisha na huko tulikotoka?

Mgaya: Ninachokiona sasa hivi, tumejitawala miaka 50 na bado tunategemea kuendesha nchi kwa fedha za kukopa. Nadhani kwa hiyo miaka 50 tungekuwa tumekwishajitayarisha kuendesha nchi kwa hela zetu wenyewe.

Sasa hivi mataifa yale yanayotusaidia kwa fedha za uendeshaji nchi yetu yametishia kukataa kutoa fedha na kila mtu anahangaika. Tumepuuza wazo la kujitegemea na Mwalimu alisema mkiendelea namna hii mtauza hata Ikulu, nadhani alikuwa sahihi.

Raia Mwema: Unawazungumziaje marais waliomfuatia Nyerere?

Mgaya: Mimi niseme kwa ujumla, ni vigumu kusema Mwinyi alikuwa hivi, Mkapa alikuwa hivi au Kikwete yuko hivi. Wananchi wenyewe wanaona. Siwezi kusema sijui huyu anafaa au yule hafai.

Upungufu upo na wananchi wanajua nami naona. Labda niseme katika elimu kwamba ni jambo la kushangaza mpaka sasa hatujaweza kujenga madarasa ya watoto wetu kusoma kwenye darasa ambamo wanakaa kwenye madawati, ni aibu kusikia bado kuna watoto wanasoma chini ya miti, ni aibu.

Raia Mwema: Vipi kuhusu uendeshaji wa serikali?

Mgaya: Unajua si kwamba nchi hii haina hela, angalia mashangingi haya na misururu inayokwenda na marais. Wakati wetu hapakuwa na misururu mirefu inayomsindikiza rais.

Kuna wakati Mwalimu aliniandikia minute mimi, akasema nikiwa Dar es Salaam nataka magari matatu tu. Gari la polisi mbele, gari la kwangu (Nyerere) na gari linalofuata nyuma.

Misururu hii ina athari kiuchumi. Mashangingi 12 katika msafara wa rais yanatafuta nini?

Raia Mwema: Huoni hiyo inatokana na changamoto za kiusalama za wakati huu?

Mgaya: Kwani wote wanaokuwapo wanamlinda Rais? Una mpa DC shangingi Lindi huko, huyo anatakiwa awe sana sana Landcruiser (hard top).

Raia Mwema: Ukiwa IGP wewe na Nassoro Moyo akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, hamkuwa mnaelewana, ni kweli?

Mgaya: *Nassoro Moyo alikuwa anataka aliendeshe Jeshi la Polisi, nikakataa. Kwa mfano, nakumbuka moja ambalo tulitofautiana mimi nilikwenda kumwomba Rais Nyerere kuchukua maofisa, vijana waliotoka chuo kikuu wenye digrii niwachukue moja kwa moja wawe maofisa wa jeshi, hilo Moyo hakulitaka.*

Raia Mwema: Nasikia miaka yote mitano mliyokaa kama Waziri na IGP, Moyo hakuwahi kufika ofisini kwako.

Mgaya: *Sikumbuki, lakini yeye mwenyewe alikuja kuomba radhi, kwamba nimsamehe mambo mengine aliyofanya hayakuwa mazuri.*

Raia Mwema: Mwalimu Nyerere alisikia kuhusu ugomvi wenu huo?

Mgaya: *Mwalimu alisikia akatuita akatuambia; nasikia wewe Mgaya una jeshi lako…. Moyo una jeshi lako, la kwangu liko wapi? Akatuonya kwamba msigawane jeshi, hili ni jeshi la nchi.*

Raia Mwema: Kulikuwa na Ubara au Uzanzibari jeshini?

Mgaya: *Hapana hapakuwa na mpasuko huo jeshini. Moyo alioniomba msamaha nami nikakubali. Aliondoka wizarani mapema kabla yangu.*

Raia Mwema: Unakumbuka nini kingine kuhusu Nyerere? Ulikaa naye miaka mingi kama ADC wake.

Mgaya: Mwalimu alipenda sana Tanzania na aliwapenda sana Watanzania. Nilichojifunza kwake ni uaminifu kwa nchi na kuheshimu madaraka anayopewa mtu. Hayo ndiyo muhimu zaidi.

Raia Mwema: Ukiwa IGP ulipendelea ‘kunywa’?

Mgaya: Nilikuwa nakunywa bia. Siku hizi nimeacha, mara chache sana nakunywa wine lakini mara nyingi nakunywa maji au juice.

Raia Mwema: Kuna tatizo la kiafya linalokukabili?

Mgaya: Sina tatizo la sukari, tatizo langu kubwa nilipata ugonjwa ambao unapata wanaume, enlarged prostate (tezi dume), nilifanyiwa operesheni mara tatu lakini sijambo sasa.
 
Hizi mambo za IGP vs Minister of internal affairs naona mpaka sasa kuna kuingiliana



Msafara mashangingi 12 yanini,DC apewe hard top atumie kufuatilia maendeleo vijijini....hawa wazee ndiyo wakuwafuata kutafuta hekima na ushauri wao
 
Kwenye hii story Mgaya ame miss dataz za miaka, Mgaya alikuwa IGP, mwaka 1976 na sio 1975, baada ya IGP Pundugu kujiuzulu kwa kashfa ya Kesi ya Mauaji Mwanza, ambayo pia ilimtoa Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali Hassan Mwinyi, nafasi yake kuchukuliwa na Hassan Nassor Moyo, pia ilimtoa Director wa TISS, Mzena na nafasi yake kuchukuliwa na Hassy Kitine.
P.
 
Kwenye hii story Mgaya ame miss dataz za miaka, Mgaya alikuwa IGP, mwaka 1976 na sio 1975, baada ya IGP Pundugu kujiuzulu kwa kashfa ya Kesi ya Mauaji Mwanza, ambayo pia ilimtoa Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali Hassan Mwinyi, nafasi yake kuchukuliwa na Hassan Nassor Moyo, pia ilimtoa Director wa TISS, Mzena na nafasi yake kuchukuliwa na Hassy Kitine.
P.
Ni sahihi upon sawa bro..

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Kwenye hii story Mgaya ame miss dataz za miaka, Mgaya alikuwa IGP, mwaka 1976 na sio 1975, baada ya IGP Pundugu kujiuzulu kwa kashfa ya Kesi ya Mauaji Mwanza, ambayo pia ilimtoa Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali Hassan Mwinyi, nafasi yake kuchukuliwa na Hassan Nassor Moyo, pia ilimtoa Director wa TISS, Mzena na nafasi yake kuchukuliwa na Hassy Kitine.
P.
Uko vizuri Kijana

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Kwenye hii story Mgaya ame miss dataz za miaka, Mgaya alikuwa IGP, mwaka 1976 na sio 1975, baada ya IGP Pundugu kujiuzulu kwa kashfa ya Kesi ya Mauaji Mwanza, ambayo pia ilimtoa Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali Hassan Mwinyi, nafasi yake kuchukuliwa na Hassan Nassor Moyo, pia ilimtoa Director wa TISS, Mzena na nafasi yake kuchukuliwa na Hassy Kitine.
P.
Uko vizuri Kijana

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Nimependa swali waliloulizwa na Mwalimu Nyerere kuhusu kugawana jeshi, kwa mtu mzima hapo unajua ulipoboronga!

Najaribu kuwaza kama hiyo hekima bado ipo kwa kiongozi wetu Mkuu.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom