Tunalaani matukio ya Jeshi la Polisi kuvamia wananchi Mkoani Kigoma

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
617
1,542
ACT Wazalendo tunalaani matukio ya Jeshi la Polisi kuvamia wananchi Mkoani Kigoma.

Chama cha ACT Wazalendo kupitia Sekta ya Mambo ya ndani ya nchi inalaani kwa nguvu zote kitendo cha Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma kuvamia wananchi, kusababisha majeruhi, kupora mali na kutishia amani Mkoani humo. Mnamo tarehe 8 April, 2024 tulipokea taarifa ya Jeshi la Polisi kufanya uvamizi kwa kutumia silaha, mabomu ya machozi na kuwapiga wananchi, wafanyabiashara wadogo katika soko la Kijiji cha Kajana, Wilayani Buhigwe na kusababisha kifo cha mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Athumani Ndongo na wawili kujeruhi akiwemo Damian Anthony ambaye alivunjwa miguu yote miwili.

ACT Wazalendo tunafahamu tukio hili ni mwendelezo wa taarifa za Polisi Mkoani humo kutumia nguvu kubwa kudhibiti imani zinazojulikana na kufichua wachawi na uchawi 'Makamchape'. Mwaka jana tulishuhudia matukio haya yakisababisha vifo katika Wilaya za Kigoma Vijijini, Kigoma na Kasulu. Tunaamini kuwa suala hili linaweza kushughulikiwa kwa weledi zaidi bila kuleta athari za mauaji, vurugu na mapigano kati ya wananchi na Jeshi hilo.

Aidha, tunafahamu njama zinazofanywa na jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma kuficha tukio hili kwakuwa sababu zilizotajwa na kuwafanya wapeleke nguvu kubwa kupita kiasi katika eneo hilo kutokuwa za kweli ikiwemo madai ya baadhi ya nyumba za wananchi kuvunjwa.

Matukio ya kuvamia na kupora mali za wananchi yanakithiri siku hadi siku hasa maeneo ya pembezoni mwa nchi. Imekuwa ni kawaida sasa jeshi la Polisi kuvamia masoko, sehemu za biashara na kuchukua mali na mitaji ya wafanyabiashara bila maelezo yoyote kinyume kabisa na sheria za nchi, jambo hili linatia hofu kwa wananchi na kutilia shaka wajibu wa jeshi la Polisi wa kulinda raia na mali zao.

ACT Wazalendo tunamtaka Waziri wa Mambo ya Ndani kuingilia kati na kufuatilia matukio haya ili kuchukua hatua stahiki kwa Jeshi la Polisi Mkoani.

Pili, tunalitaka Jeshi la Polisi kurejesha mali zote walizochukua na wananchi waliojeruhiwa wagharimiwe matibabu na fidia ya siku zote ambazo hawajafanya kazi kutokana na majeraha waliosababishiwa.

Mwisho, tunalitaka Jeshi la Polisi kufanya kazi zake kwa kufuata sheria na taratibu za nchi, kwani jukumu lao ni kulinda usalama wa raia na mali zake na sio kupora mali za wananchi na kutishia uhai na usalama wao.

Ndg. Dahlia Majid Hassan
Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani
14 April, 2024.
 
Hiki chama hakikuwepo pale walipopigwapigwa watu wa Kawe na JW?
Kwanini haikutoa tamko?
 
Back
Top Bottom