Waziri Kamwelwe afanya ukaguzi wa njia ya reli Moshi- Arusha

Tanzania Railways Corp

JF-Expert Member
Mar 23, 2018
251
595
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe afanya ukaguzi wa njia katika mradi wa ukarabati wa reli Moshi - Arusha Februari 27, 2020.

Lengo la ukaguzi huo ni kuona maendeleo ya Mradi wa ufufuaji wa njia ya reli Moshi - Arusha ambao umefikia zaidi ya 90% kwa ajili ya kupanga mikakati ya kurejesha huduma za usafiri wa abiria na usafirishaji mizigo kwa kujenga bandari kavu katika eneo la Marula mkoani Arusha na Stesheni za Moshi na Arusha.

Waziri Kamwelwe amefanya ukaguzi huo kwa kutumia Kiberenge kutoka Stesheni ya Moshi hadi Arusha akiongozana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania - TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania - TPA Mhandisi Deusdedith Kakoko.

Waziri Kamwelwe amesema kuwa amesafiri na kiberenge kutoka Moshi hadi Arusha ameona kazi kubwa inayoendelea ambapo ukarabati wa madaraja, tuta na reli unakwenda vizuri na matumaini ya kuanza safari za treni za mizigo na abiria kati ya Moshi na Arusha ni makubwa.

“nimepita nimeona njia yote ya reli imekarabatiwa, madaraja yote yamekarabatiwa lakini pia kuna maeneo ambayo tuta lote lilichukuliwa lakini wamerudisha na wametandika reli, kwahiyo nimepita na Kiberenge kutoka Moshi hadi Arusha na majaribio mbalimbali yanafanyika ili kuhakikisha tunaweza kusafirisha treni ya abiria na mizigo mpaka hapa Arusha” alisema Waziri Kamwelwe.

Waziri Kamwelwe aliongeza kuwa Serikali inaendelea na mchakato wa kuhakikisha vibarua wote waliofanya kazi ya ufufuaji wa reli hiyo wanapatiwa ajira ili kuhakikisha reli hiyo haifi tena kwakuwa watakuwa mafundi na walinzi wa miundombinu hiyo, malengo ni kuhakikisha Saruji kutoka Tanga isafirishwe kutoka Tanga hadi Arusha ili wananchi wapate unafuu wa bei za bidhaa hususani za ujenzi lakini pia wafanyabiashara na wawekezaji wa viwanda waweze kusairisha bidhaa na malighafi kwa urahisi na unafuu.

Aidha,Mkurugenzi Mkuu wa TRC amemshukuru Waziri Kamwelwe kwa kutembele mradi huo na kushukuru jitihada zinazofanywa na wafanyakazi wa Shirika kurejesha utendaji wa miundombinu ya reli ya Kaskazini, pia ameongeza kuwa treni ya mwisho kufika mkoani Arusha ilikuwa mwaka 1986 hivyo ni zaidi ya miaka 30 na ndio maana mwitiko ni mkubwa zaidi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Mhandisi Deusdedith Kakoko ameeleza kuwa “Nilikuwa meneja wa TANROADS hapa Arusha kwa zaidi ya miaka 7 sikuwahi kuona treni ikiingia Arusha, mimi wa Bandari nikiwa kama mdau mkubwa wa TRC nimefurahi sana kwa sababu niliwahi kukaa hapa palikuwa kimya, tumefanya mazungumzo na wafanyabiashara mkoani Tanga, tutajenga Bandari kavu ndogo hapa Arusha na tutakuwa tukishirikiana na Mamlaka ya Mapato na Mamlaka ya Usimamizi wa Viwango ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo, hivyo itapunguza gharama za usafiri na bidhaa” alisema Kakoko.

Shadrack Masawe ambaye ni Mhandisi wa Ujenzi anayesimamia Mradi wa ufufuaji wa Reli Moshi – Arusha amesema mradi unandelea vizuri ambapo tayari mpaka sasa treni ya abiria kwa ajili ya majaribio imefanikiwa kufika Arusha ikitoka Moshi, halikadhika wamejenga tuta jipya katika maeneo ambayo tuta liliondolewa na mvua na kuweka reli, wamejenga madaraja makubwa 7 na madogo 30, hivi sasa wameanza kukarabati njia ya reli inayokwenda Uwanja wa ndege wa Kilimanjaro - KIA.
IMG_1582832234447.jpeg


Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom