singidadodoma
JF-Expert Member
- Nov 11, 2013
- 4,394
- 1,536
Waziri wa Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako
WIZARA ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi imeeleza baadhi ya vigezo vitakavyotumika kupanga ada elekezi katika shule binafsi, kuwa ni pamoja na aina ya huduma zinazotolewa kwa wanafunzi, mishahara ya walimu.
Akizungumza jana bungeni wakati akijibu maswali ya wabunge waliojadili Hotuba ya Rais John Magufuli aliyotoa wakati kuzindua Bunge, Waziri wa Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema kutokana na vigezo hivyo, ada elekezi hizo haziwezi kufanana.
Profesa Ndalichako aliwaambia wabunge kwamba tayari wanaye mtaalamu mshauri anayefanya kazi hiyo, ambaye baada ya kukamilisha kazi, watakubaliana kwa ajili ya kutoa ada elekezi zitakazotofautiana kulingana na viwango vya shule.
Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, mambo mengine yanayoangaliwa katika huduma zinazotolewa shuleni ni pamoja na chakula, aina ya miundombinu, viburudisho na mishahara ya walimu. Profesa Ndalichako aliwahakikishia wabunge kwamba wizara inafanyia kazi suala hilo.
Alisema suala hilo linahitaji kufanyiwa kazi kwa kina, kwa kuangalia vizuri makundi ya shule. “Unaweza kukuta huduma ambazo zinapatikana shuleni zinatofautiana sana. Kuna shule nyingine mpaka zina swimming pool (maeneo ya kuogelea), zimejengwa kwa terazo na nyingine zimejengwa kwa marumaru.
Sasa unapotoa ada elekezi lazima uzingatie kwamba mwanafunzi anasoma katika aina gani ya shule. “Zipo shule nyingine za binafsi ambazo hazina hata sakafu, kwa hiyo huwezi kuja na ada elekezi, ukasema tu kwamba ni shilingi kadhaa, lazima mambo haya yote uyaangalie.
“Hata chakula wanachokula wanafunzi kinatofautiana, baadhi ya shule wanapewa mpaka soseji, wanakula pilau na wengine wanakula ugali na maharage kila siku,” alisema. Profesa Ndalichako alisisitiza kwamba haiwezekani kuja na ada elekezi zinazofanana, kwa hiyo wizara yake lazima iangalie jambo hilo kwa umakini mkubwa.
“Kuna baadhi ya shule zinawaonea sana walimu, zinawalipa kidogo na nyingine zinawalipa vizuri. Nawaomba Watanzania tuwe na subira, wizara yangu inalifanyia kazi, lakini si jambo linalohitaji kufanyiwa kazi kwa haraka, tutakapokuwa tayari tutakuja kuwapa majibu,” alisema.