Pinda awageukia viongozi wa dini
Imeandikwa na Mwandishi Maalumu (HabariLeo), Bunda; Tarehe: 21st February 2011
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema viongozi wa dini wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhimiza uadilifu miongoni mwa waumini wao, kwa sababu wengi wao ndiyo waajiriwa katika sehemu mbalimbali ikiwemo Serikali.
Amesema katika kundi kubwa la waumini, wamo watumishi wasiotimiza wajibu wao na hata wengine kudiriki kuiba au kupokea rushwa, lakini wote ni waumini wao na wanahitaji
kuchungwa kiroho.
Alitoa rai hiyo katika Kanisa la Mtakatifu Paulo wilayani Bunda, mkoani Mara wakati wa sherehe za kumsimika Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki la Bunda, Mhashamu Renatus Nkwenda.
Waziri Mkuu aliyefika Bunda kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko safarini Mauritania, alisema: "Baba Askofu umeteuliwa kushika jimbo hili jipya katika kipindi ambacho kuna changamoto nyingi za umasikini, za waumini waadilifu na wasio waadilifu, kondoo wanaotuongoza sisi, hao hao ndiyo wezi na wengine wala rushwa ambao tuko Serikalini…lakini ni kondoo wako."
Alisema viongozi wote wawe wa dini au wa Serikali hawana budi kulivalia njuga suala la uadilifu ndani ya nchi kwani hali imefikia pabaya.
"Ninyi mnayo nafasi kubwa ya kiroho na kimwili, lakini ni lazima sote tulivalie njuga… lazima tupige kelele, tukipukutisha maadili ya nchi, sote twafa," alisema Waziri Mkuu.
Akiwahutubia maelfu ya waumini walioshiriki ibada hiyo, Waziri Mkuu alisema kila mmoja ana jukumu la kulinda amani na utulivu wa nchi ambavyo vimedumu kwa miaka 50.
"Sisi tumepokea wakimbizi kutoka kila kona, leo hii tukivurugana tutakwenda wapi? Rwanda au Burundi ambako hawana ardhi ya kutosha?" Alihoji.
Alitumia fursa hiyo kuwakumbusha Watanzania kwa wasibaguane kwa misingi ya dini, kabila au jinsi kwani kwa kufanya hivyo, Taifa litasambaratika.
Mapema, akitoa nasaha katika ibada hiyo kabla ya kuweka wakfu Askofu Mteule Renatus Nkwande, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo alisema Askofu Nkwande amepata uongozi katika kipindi ambacho kuna changamoto ya mgawanyiko baina ya viongozi wa dini mbalimbali, viongozi wa Serikali ambayo matokeo yake yanawaumiza wananchi walio wengi.
Alisema changamoto zilizopo, hana budi kukabiliana nazo, lakini akamtaka awe tayari kuubaini uovu na kuusimamia ukweli hata kama itagharimu maisha yake.
"Si vizuri kuunyamazia uovu na kushindwa kuutambua kuwa ni uovu. Ni vema kuwa na ujasiri wa kulitamka na kulisema hili ovu… Huu ndiyo msimamo unaotakiwa katika Tanzania ya sasa," alisema Pengo.
"Uwe na ujasiri wa kusimama nyuma ya ukweli na kufa kwa ajili ya hilo… ukiogopa kufa leo utakufa kesho.
Ukiogopa kusema ukweli leo, kesho au kesho kutwa utakufa, kikubwa ni kuhakiksha unakufa katika mikono ya Kristu na si vinginevyo."
Naye Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Mhashamu Askofu Juda Thadeus Ruwa'ichi wa Jimbo Katoliki la Mwanza akizungumza kwa niaba ya maaskofu wote wa TEC, alisema wao kama viongozi wataendelea kuhimiza mshikamano wa Kitaifa licha ya kudaiwa kuwa wao ni wa dini.
Alisema wanaodai hivyo wana lao na kuongeza: "Sisi siyo wadini, bali ni wakweli, wenye uwezo wa kukemea na kusahihisha mambo yanapokwenda ndivyo sivyo.
Kama hatukuwahi kuwagawa raia huko nyuma kamwe hatutafanya hivyo kesho wala kesho kutwa," alieleza Ruwa'ichi.
Mhashamu Askofu Nkwande aliyesimikwa jana, alizaliwa Novemba 12, 1965 katika Kijiji cha Mantare, Sumve, wilayani Kwimba mkoani Mwanza. Ni mtoto wa kwanza kati ya watoto 10 wa Mzee Alphonce Masalu na Mama Mamertha Masabula.
Mtoto mmoja alifariki na sasa wamebaki watoto tisa. Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Tamisemi, Aggrey Mwanri, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Enos
Mfuru, wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Mara, maaskofu 30 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania na mapadri na watawa kadhaa.
Source: Habari leo (Pinda awageukia viongozi wa dini)