Watesi wa Chongolo wameshinda: Mengi yaja

Jaji Mfawidhi

JF-Expert Member
Feb 20, 2016
14,047
20,411
Novemba 28, 2023 nilianza kuona fununu za aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo kujiuzulu. Nikiri ilikuwa nimetokea msibani Bukoba ambako nilikaa siku nne, hivyo sikuwa na taarifa za kinachoendelea mtandaoni. Novemba 29, 2023 nilisafiri kwenda Nairobi, na hatimaye kuja hapa Mombasa.

Kimsingi nilianza kufatilia na kudodosa kinachoendelea. Nikiwa hapa Mombasa, nikaona taarifa mtandaoni zenye kusema kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amekubali taarifa ya aliyekuwa Katibu Mkuu Chongolo kujiuzulu. Nikamsilikiza Katibu wa Uenezi na Itikadi, Paul Makonda naye akatoa taarifa iliyoishia kusema kuwa Rais Samia amekubali ombi la Chongolo kujiuzulu.

Sitanii, ikabidi kwanza niingie kwenye mtandao. Nikasoma hiyo iliyotajwa kuwa ni barua ya Chongolo kwenda kwa Rais Samia. Barua hiyo ilikuwa imetumwa siku moja kabla mitandaoni. Kwanza kitendo cha barua ya Chongolo kuvuja kwenye mitandao kabla ya kufika kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM) kilinipa shida kidogo.

Nilijiuliza nani aliyeisambaza kwenye mitandao ya kijamii? Ni Chongolo mwenywe aliyeiandika? Ni walioipokea? Hilo nikaona niliweke kando. Maudhui ya barua hiyo nayo yakaniongezea kiu ya kujiuliza maswali. Nikajiuliza ni uchafuzi gani huo uliofanywa kwenye mtandao dhidi ya Chongolo?

Sitanii, baada ya nusu saa nilitumiwa dozia mbili. Moja inaonyesha kuwa Chongolo alipata ajali na gari lake binafsi likawa halina bima, hivyo baada ya ajali akaenda kwenye kampuni ya Bima akalipa Sh mil. 9 akarejesha nyuma taarifa (akafoji) kwa nia ya kutaka alipwe fidia Sh milioni 196. Upatikanaji wa ajali ukaunganishwa na jambo jingine.

Taarifa hiyo iliyokuwa inasambaa kama moto wa pori, ikaongeza kuwa Chongolo alipata ajali hiyo akiwa amelewa chakali na ndani ya gari alikukwa na wanawake. Hapa moyo wangu ukakataa. Nikasema binafsi nimemfahamu Chongolo tangu mwaka 1999 kwa maana ya miaka 24 sasa. Kwamba Chongolo alikuwa amelewa pombe akapata ajali, hili kwangu haliingii akilini.

Kwa miaka yote 24 niliyomfahamu akiwa Mwandishi wa Habari mwenzangu pale Majira, baadaye akiwa Katibu Msaidizi katika Idara ya Uenezi na Itikadi CCM na Mkuu wa Vyombo vya Habari vya Chama, akiwa DC wa Longido na baadaye Kinondoni, kisha akawa Katibu Mkuu wa CCM, nimekaa naye mara nyingi ila sikupata kumwona anakunywa pombe.

Mimi nakunywa pombe na kinywaji ninachokunywa siyo siri kwa walio marafiki zangu. Hata akiwa Katibu Mkuu nikikaa naye, ilikuwa nakunywa kinywaji changu, yeye anaagiza kahawa. Nikajiuliza alikuwa ananikwepa mimi au anakwepa nini kunywa pombe kwa miaka yote hiyo 24? Hili kichwa changu kinaendelea kulikataa. Mbaya zaidi hata huyo mwanamke wanayesema alikuwanaye, hajatajwa hadi leo.

Sitanii, kama hiyo haitoshi likamwagwa baya kuliko. Kikasambazwa kipeperushi kinachotajwa kuwa ni mawasiliano kati ya Chongolo na mwanamke ampendaye. Katika kipeperushi hicho, kitu kinachoonekana kuwa ni jina la mtumaji kimeandikwa “D C”. Katika lisilofikirika kwa maadili ya Kitanzania, mtumaji akaonyesha Chongolo alituma kiungo chake cha uzazi kwa mwanamke (asiyetajwa).

Kikaendelea kuonyesha kuwa Chongolo anaomba huyo mwanamke asiyetajwa katika kipeperushi amtumie naye kiungo chake cha uzazi… Hii ikaongezewa na maelezo yaliyojitenga ikisema ni mawasiliano kati ya Chongolo na mwanamke ambaye hatutajiwi ni nani na hajajitokeza hadharani hadi leo kueleza kuwa alitumiwa picha hizo za kudhalilisha.

Ndugu zangu Watanzania. Nimeandika ujumbe wa kumshukuru Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan aliyeagiza ufanyike uchunguzi juu ya suala hili. Ingawa Msemaji wa CCM Makonda hakusema kama upo uchunguzi, lakini kutokana na vyanzo vyangu uchunguzi upo na ndiyo maana Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Anamringa Macha amepewa nafasi ya kukaimu wadhifa huo.

Sitanii, hatua hii ya kuagiza ufanyike uchuguzi imenipa imani kuwa Rais Samia amechukizwa na mchezo huu mchafu. Rais Samia amekuwa wazi katika uongozi wake muda wote. Hakurupuki anataka kuona haki ikitendeka kwa kila awaye. Kitendo kilichofanyika ni kibaya haijapata kutokea. Kimemdhalilisha Chongolo si tu mbele ya jamii, bali hata mbele ya familia yake; mke na watoto.

Yapo mambo kadhaa kupitia makala hii leo nayaandika. Kwanza nisema nafahamu kuwa uchuguzi unafanyika, ila angalau la Chongolo kunywa pombe, nafahamu asilimia 99.99 kuwa ni uongo. Hanywi pombe. Sasa nimeangalia hicho kipeperushi kinachodaiwa kuwa ni mawasiliano kati ya Chongolo na mwanamke. Jambo moja tu niwakumbushe wanaofanya uchunguzi kuwa kwa sasa kuna teknolojia ya “Akili Tarakirishi (Artificial Intelligence – AI).

Kwa wiki nzima nimekuwa hapa Mombasa tunajadili matumizi ya AI. Teknolojia hii ni ya ajabu kweli. Leo niko Mombasa, lakini mtu akitaka kuitumia naweza kuonekana ‘live’ napita kwenye mitaa ya Sumbawanga - Rukwa mchana au usiku! Hivyo kipeperushi kubandikwa “D C” ni jambo rahisi kuliko kunywa uji uliopozwa.

Sitanii, sisemi ndicho kilichotokea kwa Chongolo maana uchunguzi unaendelea, ila kwa wiki yote tumejadili hatari ya AI ikitumiwa vibaya, maadili katika matumizi ya AI, uwepo wa sera, sheria, kanuni na miongozo. Tanzania kati ya vyote hivyo hatuna hata kimoja. Tunaitegemea Sheria ya Makosa Mtandaoni, ambayo ilivyoandikwa Mwendesha Mashitaka hawezi kushinda kesi ya AI mahakamani hapo nchini.

Siyo Tanzania tu, hata wenzetu Kenya hapa tulipo hawana sheria, sera au kanuni, japo Waziri wao wa Mawasiliano, Habari na Teknolojia ya Kidigiti ameelekeza mchakato wa kutunga sheria uanze mara moja. Uganda wao angalau wa rasimu ya sera, Misri ndiyo sera inaelekea Bungeni. Bara la Ulaya lilianza mchakato wa kutunga sheria ya AI mwaka 2021 na mwezi Juni mwaka huu, ndipo wamepitisha rasmi rasimu ya utunzi wa sheria hii sasa inajadiliwa na nchi wanachama.

Lakini, hata kama sheria haipo hivi nchi hii maadili yetu yameshuka kwa kiwango cha kusambaza picha za viungo vya uzazi vya viongozi wetu kwenye mitandao ya kijamii? Ni jambo gani limemsukuma aliyetenda haya ayatende? Je, tusipoufahamu ukweli na mhusika akachukuliwa hatua za kisheria leo Chongolo akiishamalizwa kisiasa na kijamii kwa kuua heshima yake kabisa, nani atafuta?

Sitanii, nimejiuliza sana. Nimejiuliza tatizo ni nini hadi watu wanasambaza taarifa za hivi? Ni upendo wa taifa lao? Ni husda? Ni fitina? Ni ‘kamunobele?’ Ni vita ya madaraka? Ni siasa zimekua katika nchi yetu? Nimepata majibu mengi, ambayo nadhani uchunguzi unapaswa kupanuliwa mawanda yake. Suala hili liko kama kokolo ndani yake ila makubwa mawili kila nilipozungumza na vyanzo vyangu yamejitokeza mara nyingi.

La kwanza ni “UKATIBU MKUU”. Baada ya vipeperushi vya kashfa dhidi ya Chongolo kusambazwa na barua yake ya kujiuzulu kuvujishwa, tulianza kutajiwa majina ya “wateule” wa nafasi ya UKATIBU MKUU. Majina kama manne yametajwa mara nyingi. Sasa nikajiuliza hawa kuna mmoja wao ameshiriki mchezo huu wa uchafuzi au nao wametajwa kushirikishwa kwa nia ya kupoteza maboya?

La pili ni “URAIS MWAKA 2030”. Hili kwa kadri nilivyoelezwa lina mawanda mawili au matatu hivi. Kwanza wapo viongozi wazito ndani ya chama ambao wana matamanio ya kupata urais mwaka 2030 (kwa hesabu wanazopiga) Rais Samia atakapomaliza muda wake. Hawa nimeambiwa wanalalamika. Wanalalamika kuwa katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanya uchaguzi wa NEC Desemba, 2022, Chongolo aliwaumiza!

Wanasema aliwaumiza ama kwa kutochaguliwa kabisa au kuchaguliwa kwa kura chache hali inayopeleka sura kwenye jamii kuwa wamepoteza mvuto. Kwa maana hiyo, wamepiga hesabu na kuona kuwa Chongolo akikivusha Chama Cha Mapinduzi kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, Rais Samia ataona anamfaa kuendelea naye hadi 2030.

Ikitokea hiyo, ina maana mwaka 2027 katika uchaguzi wa NEC ndani ya CCM, Chongolo atadhibiti makundi haya ya urais yasiingize watu wao katika safu za uongozi kwa ajili ya kujipanga kuelekea mwaka 2030. Kundi hili linakwenda sambamba na wagombea ubunge watarajiwa waliokosa nafasi siku za nyuma wanaona Chongolo haangukii kwenye makundi yao, kwa hiyo bora wamalizane naye mapema!

Sitanii, masuala ya kuchafuana kisiasa hapa nchini hayajaanza leo. Sitarudi miaka ya nyuma sana, ila nigusie kati ya mwaka 2000 na sasa. Tutakumbuka Rais (hayati) John Magufuli alipoonekana anaweza kupata urais kilichomkuta miaka ya kuelekea 2005. Taifa letu liliambiwa amemgawia nyumba ya serikali kimada kwa jina la Angelina, akiwa si mtumishi wa umma katika ule mpango wa kuuza nyumba za serikali. Hadi leo, hatukuelezwa mwisho wa tuhuma hizi.

Alipoonyesha nia ya kugombea urais mwaka 2005, Dk. Salim Ahmed Salim tunakumbuka picha yake ilivyounganishwa na Sulutani wa Oman na kuchapishwa na gazeti moja ikamkosesha urais. Sitazungumza watoto wa marais wanavyopopolewa kila kukicha hapa nchini.

Kuchafuana kisiasa kulielekea kuvuka mipaka hapa nchini mwaka 2007. Tunakumbuka mitume 12 walivyoshirikiana na Spika wa “Kasi na Viwango” kumdhalilisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kwa kufanya uchunguzi hadi Marekani, lakini katika taarifa yao ya Richmond hawakupata kumpa nafasi Lowassa kueleza anachokifahamu juu ya Richmond, ila lengo lao wao la kumdhibiti asigobee urais lilifanikiwa.

Wakati mitandao ya kijamii inaanza kushika kasi nchini, mwaka 2008 tunakumbuka mtandao wa “The Utamu” ulivyounganisha picha ya Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete kinyume kabisa na maadili ya jamii yetu, hadi mtandao huo ukafungiwa.

Sitanii, kwa uchafuzi ule ule kuelekea 2020 tulishuhudia gazeti moja lisilo na maadii likitumika kuwachafua Hayati Maalim Seif Sharif Hamad na Zitto Kabwe wakiwahusisha na vitendo vya ushoga. Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Dk. Festo John Dunduge, Aprili 2023, akiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, alipata ajaili Dodoma.

Baada ya ajali hiyo, nchi ilishuhudia washinidani wake kisiasa walivyosambaza taarifa sawa na wanazomsambazia Chongolo wakidai alikuwa amelewa, eti alikuwa na mwanafunzi kutoka UDOM na mengine mengi. Tena wakasema mwanafunzi huyo wa kike amefariki, ila bahati mbaya wakakosea ikaonekana binti huyo huyo amefika Moshi, kisha akafia Dodoma kwa wakati huo huo.

Sitanii, nchi yetu ina watu ambao ni wajumbe wa kudumu wa “Kamati ya Roho Mbaya.” Wanaunga maelezo kuhalalisha uhalifu wao. Leo kwa mafano wanahoji wakisema Chongolo alipata wapi fedha. Wanasahau kabla ya Chongolo kuingia kwenye siasa, pia alikuwa anafanya biashara. Nimetangulia kusema nimemfahamu kitambo.

Chongolo alikuwa ananunua nyanya makambako kwa wastani wa Sh 3,000 kwa tenga miaka ya 2007, anasafirisha matenga ya kutosha hadi soko la Big Brother Dar (kwa sasa Mahakama ya Ndizi) anauza tenga moja Sh 70,000. Alikuwa anakodi magari yanaleta nyanya na bidhaa nyingine, na kwa kufanya hivyo amepata kujenga nyumba kadhaa katika Jiji la Dar es Salaam.

Si hilo tu, nafahamu Chongolo ana magenge ya kuuza nyanya, vitunguu, ndizi za kukoboa na bidhaa zote unazozifahamu za genge yasiyopungua 10 hapo Dar es Salaam. Mara kadhaa asubuhi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, tumekutana pale Mahakama ya Ndizi akipakia bidhaa za genge kwenye gari lake na kusambaza. Anaamka saa 11 alfajiri ananunua bidhaa anasambaza kwenye magenge yaliyoishiwa, anaoga anakwenda kazini kama Mkuu wa Wilaya. Wangapi wanaiweza hiyo?

Narudia, huyu mtu anayeitwa “Kigogo” ni sawa na bunduki ya kuazima. Utashuhudia atakavyoniporomoshea matusi baada ya makala hii. Tumemshuhudia anavyowaandama wateule kadhaa wa Rais kwa sasa akiwamo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko kwa kumzushia kila liwalo siku hadi siku.

Jambo moja ikiwa hii bunduki ya kuazima inayoitiwa “Kigogo” itaendelea kupelekewa matango pori ikayasukuma kwenye jamii, uamuzi ukafanyika wa kuwatosa aliowasema, tutalea jini kwenye chupa. Ipo siku ataibuka na kutoa tuhuma zitakazobomoa taifa letu. Kwa kuwa jamii itakuwa imeaminishwa kuwa kila anachosema “Kigogo” ni kweli, ipo siku atamwaga bomo chafu kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya viongozi wakuu wa nchi tutatfutana. Si kila anachokisema “Kigogo” ni cha kweli.

Narudia, Sitanii, Chongolo hanywi pombe. Sijawahi kumwona akiranda na wanawake mitaani. Si tabia yake. Nisema kama yuko anayemtuma “Kigogo” kufanya haya, afahamu kuwa “Kigogo” amefika dau kwake. “Kigogo” akipata mtumaji mwenye dau kubwa zaidi, atamgeukia mtumaji kama mbwa aliyeshindishwa njaa asivyomtambua mwenye nyumba. Anguko la mtumaji, kishindo chake kitakuwa kikuwa zaidi.

Kama ni vyeo, naomba tuvitafute kwa njia halali. Dhana ya kuchafuana kupata madaraka, inaweza kuanza kubomoa umoja wetu wa kitaifa, na mwisho wa siku tukatengeneza makundi ambayo mbele ya safari yanaweza kugeuka kuwa gharama kubwa kwa nchi yetu. Naomba uchunguzi ufanyike, Chongolo atendewe haki. Kama ameyatenda anayotuhumiwa nayo, aadhibiwe. Kama hakuyatenda, asafishwe. Mungu ibariki Tanzania.


credit: D Balile.
 
Hebu acha upuuzi na ww nani anasema kunywa pombe ni shida .chongolo hanywi hilo tunalijua fika ila kataa haya

1. Kufoji alipwe 196m na akalipwa je anafaa kuwa kiongozi mkuu wa chama kukemea rushwa na ufisadi bado?
2. Tuhuma za kulala na wakurugenzi na kuwaomba hela kuwatishia kuwatumbua.
3. Kutongoza ovyo wanawske kwa kutumia cheo chake. Hilo ni kero toka yuko longido.wanawake wanamjua anatuma chat anafuta huyo wa boro alimuweza.

Na huo uchunguzi kuna moja nzito itatajwa utabaki mdomo wazi
 
"Rais Samia amekuwa wazi katika uongozi wake muda wote. Hakurupuki anataka kuona haki ikitendeka kwa kila awaye"

Niliona andiko lako ni zuri na lina objective, nilipofika hapa kwenye kusifu, kuabudu na kama kuomba huruma nikaishia hapa.

Umetumwa na Chogolo, inawezekana kabis kaonewa, maana sina ushahidi, ila nachukia sana uchawa, na kujipendekezala.

Na Chogolo kajiuzulu kwa hiyari yake, huko si kukubali makosa? Hivi mnajua maana ya kujiuzulu? Kwamba mimi ningesingiziwa kitu cha uongo ninge resign?
 
Hebu acha upuuzi na ww nani anasema kunywa pombe ni shida .chongolo hanywi hilo tunalijua fika ila kataa haya
1.kufoji alipwe 196m na akalipwa je anafaa kuwa kiongozi mkuu wa chama kukemea rushwa na ufisadi bado?
2.Tuhuma za kulala na wakurugenzi na kuwaomba hela kuwatishia kuwatumbua .
3.Kutongoza ovyo wanawske kwa kutumia cheo chake .hilo ni kero toka yuko longido.wanawake wanamjua anatuma chat anafuta huyo wa boro alimuweza.
Na huo uchunguzi kuna moja nzito itatajwa utabaki mdomo wazi
Unaweza ukawa na ushahidi wowote katika haya? Hivi kwa unri kama wake amebakiza nini hadi atumie mwanamke picha ya Boro? Acha hizo we February Makamba.
 
Hili la Samia kumaliza muda wake 2030 naona ni propaganda ya sasa!!

Demokrasia ifuate mkondo wake, hajawahi kuchaguliwa na wajumbe wa CCM- Ameokota dodo chini ya mbuyu,aache wanaoweza kuangua madodo wakalisha familia nzima waangue!
Tume inayolipwa na Bibie inaweza kumtangaza mtu mwengine!

Labda sala na maombi mungu afanye jambo.
 
Hebu acha upuuzi na ww nani anasema kunywa pombe ni shida .chongolo hanywi hilo tunalijua fika ila kataa haya
1.kufoji alipwe 196m na akalipwa je anafaa kuwa kiongozi mkuu wa chama kukemea rushwa na ufisadi bado?
2.Tuhuma za kulala na wakurugenzi na kuwaomba hela kuwatishia kuwatumbua .
3.Kutongoza ovyo wanawske kwa kutumia cheo chake .hilo ni kero toka yuko longido.wanawake wanamjua anatuma chat anafuta huyo wa boro alimuweza.
Na huo uchunguzi kuna moja nzito itatajwa utabaki mdomo wazi
BALILE BHANA!
 
K
Novemba 28, 2023 nilianza kuona fununu za aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo kujiuzulu. Nikiri ilikuwa nimetokea msibani Bukoba ambako nilikaa siku nne, hivyo sikuwa na taarifa za kinachoendelea mtandaoni. Novemba 29, 2023 nilisafiri kwenda Nairobi, na hatimaye kuja hapa Mombasa.
Kwani kuna ulazima wa kutwambia Ukikuwa Bukoba to Nairobi to Mombasa??
🤣🤣
 
Unaweza ukawa na ushahidi wowote katika haya? Hivi kwa unri kama wake amebakiza nini hadi atumie mwanamke picha ya Boro? Acha hizo we February Makamba.


We kenge kweli, kuna wazee wa miaka 68, wama wajukuu, na PhD wanatuma picha za utupu, umri "for some" sio busara, Chogolo is not an exception.

Inawezekan hii ni timing mbaya na ina nia ovu ya kumchafua, ila kafanya hayo mambo yote kama ilivyo kawaida.

Na usiwe kama mtoto wa Kimasai anayesoma olgalai, Kujiuzulu ni kukubali makosa na kuona haufai, unawajibika kwa yote yanayoendelea.
 
We kenge kweli, kuna wazee wa miaka 68, wama wajukuu, na PhD wanatuma picha za utupu, umri "for some" sio busara, Chogolo is not an exception ...

Inawezekan hii ni timing mbaya na ina nia ovu ya kumchafua, ila kafanya hayo mambo yote kama ilivyo kawaida.

Na usiwe kama mtoto wa Kimasai anayesoma olgalai, Kujiuzulu ni kukubali makosa na kuona haufai, unawajibika kwa yote yanayoendelea.
Chongolo amekuwa kafara tu na mpango umesukwa na sukuma Gang! We all know lakini shetani atashindwa mwishoni.
 
Kikaendelea kuonyesha kuwa Chongolo anaomba huyo mwanamke asiyetajwa katika kipeperushi amtumie naye kiungo chake cha uzazi… Hii ikaongezewa na maelezo yaliyojitenga ikisema ni mawasiliano kati ya Chongolo na mwanamke ambaye hatutajiwi ni nani na hajajitokeza hadharani hadi leo kueleza kuwa alitumiwa picha hizo za kudhalilisha.
Ndio michezo yenu huko ccm.

Hapo mnavuna mlichopanda
 
Back
Top Bottom