Elections 2010 Watawala wetu wamepoteza Hekima?

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,475
39,988
M. M. Mwanakijiji (Tanzania Daima)

amka2.gif
WATAWALA wetu wanahitaji hekima. Yaani, ile tunu na kipaji ambacho Mwenyezi Mungu amewajalia watu kuweza kupambanua na kuamua kati ya mema na maovu, yanayofaa na yasiyofaa, yenye kusaidia na yale yasiyosaidia.
Ni kipaji ambacho mtu hawezi kufundishwa kwa kwenda shule na huwezi kumpa mtu cheti cha kuhitimu kama vile mtu anavyomaliza elimu fulani. Haiwezekani kuwachukua watu na kuwapa semina au warsha juu ya hekima ukitarajia kuwa baada ya kumaliza basi wote wataondoka wakiwa na hekima.
Hekima ni kipaji cha Mungu kwa watu na kila mmoja anapewa kwa kiasi fulani. Lakini kati yetu wapo wanaopewa kipaji hicho zaidi na wapo ambao kama hawana wanahitaji kuomba kipaji hicho zaidi.
Miongoni mwa watu wenye kuhitaji kipaji cha hekima ni watawala. Nimefikia hitimisho hili baada ya kutafakari miaka mitano iliyopita na kuangalia kwa mbali miaka mitano ijayo. Matukio ya siku chache zilizopita wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi na mipango ya baadhi ya watu kutaka kugombea Uspika wa Jamhuri ya Muungano kumenifanya nijiulize “viongozi wetu wana matatizo gani”? Nilipojitahidi kutafuta jawabu nilijikuta narudishwa kwenye simulizi la Mfalme Suleiman (Mfalme Solomoni).
Tunaambiwa katika vitabu vya dini kuwa Solomon alikuwa ni mtu mwenye hekima sana. Na hadi leo katika misemo na maisha ya viongozi mbalimbali tunaambiwa hajawahi kutokea mtu mwenye hekima kama Suleiman.
Ndipo nikajikuta najiuliza ni kitu gani kilimfanya Suleiman awe na hekima hivyo hadi leo kukumbukwa kwa hekima yake?
Katika simulizi la Mfalme Solomon kwenye 1 Wafalme 3 mfalme Suleiman anaambiwa katika ndoto aombe kitu chochote kwa Mwenyezi Mungu naye atapewa. Tunaambiwa Solomon akasema “nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?”
Tunaambiwa Mungu alimkubalia kumpa huo “moyo wa adili” yaani uwezo wa hekima kwani katika sura kadhaa chini tunadokezwa kuwa “basi mfalme Sulemani akawapita wafalme wote wa dunia kwa mali na kwa hekima na pia ulimwengu wote ukamtafuta uso wake Sulemani, ili waisikie hekima yake, Mungu aliyomtia moyoni.”
Nilipopitia maandishi haya na pia kusoma katika Kurani juu ya Sulemani nikagundua kuwa Mfalme Sulemani anatajwa katika vitabu vyote kwa uwezo wake mkubwa wa kufikiria na akili ya kufanya maamuzi magumu. Lakini katika yote ni hekima ndiyo iliyomtofautisha Suleiman na watawala wengine wa zama zake.
Ndugu zangu, tunapoanza ujenzi wa Jamhuri yetu ya tano (The fifth Republic) hitaji kubwa ya watawala wetu ni hii hekima.
Hekima ambayo ni uwezo wa kujua nini kifanyike wapi, kwanini, lini na nani? Lakini siyo hivyo tu bali uwezo wa kujipatia jibu kuwa kwanini kilichofanyika kimefanyia au kwanini kinachotakiwa kufanyika kifanyike.
Kama ambavyo nimedokeza hekima haiwezi kufundishwa shuleni kwani huja kutokana ma mang’amuzi ujuzi wa mambo mbalimbali ni hekima ambayo inawafanya baadhi ya wazee mijini na vijijini kuheshimika sana.
Kwetu Waafrika na hata sehemu nyingine duniani hekima hii ilikuja kutokana na ujio wa uzee. Tunapomwona mtu mzima tunaamini kuwa mtu huyo ana hekima ya aina fulani.
Lakini hekima ninayoizungumzia leo siyo ya wazee au ile ya kidini; bali ni hekima ya kiuongozi. Katika taifa kama la kwetu hatuwezi kuongozwa au kutawaliwa pasipo hekima.
Tunaweza kutawaliwa kwa vitisho, tunaweza kutawaliwa kwa kejeli, tunaweza kutawaliwa kwa kuburuzwa na hata kuchakachuliwa kura zetu, naam tunaweza kutawaliwa kwa jinsi watawala wapendavyo; hatuwezi kutawaliwa pasipo hekima.
Ndugu zangu tunapoanza mchakato wa kuunda serikali mpya, na kujiandaa kuapisha Spika, na wabunge wapya, hatuna budi kujiuliza kwanza kama kwa kuwachagua tulitumie hekima na kama wao waliochaguliwa wanayo hekima ya kuwa viongozi wetu. Kwani hakuna ufisadi mkubwa zaidi kama wa mtu kukosa hekima halafu akatawala kana kwamba anayo.
Tukumbuke kuwa hekima haisimami peke yake, hekima mara zote huendana na ujasiri. Huwezi kuwa na kiongozi mwenye hekima ambaye siyo Jasiri. Na ukimkuta kiongozi jasiri asiye na hekima basi umemkuta mtawala wa mabavu. Tunahitaji viongozi majasiri; yaani majasiri katika misimamo, majasiri katika maamuzi, na majasiri katika vitendo. Tusipokuwa na viongozi wenye ujasiri katika hekima basi tunakuwa katika mazingira ya kudumu ya majuto.
Lakini jambo la kwanza kabisa ni kwa watawala wetu kutambua kama alivyofanya Suleiman kuwa wanahitaji hekima. Hadi hivi sasa bado binafsi sijaona hekima ikinyanyuliwa juu kama tunu ya msingi. Tunahitaji Rais mwenye hekima, tunahitaji Mawaziri wenye hekima na tunahitaji wananchi wanaofuatilia mambo yanayofanywa na viongozi wao huku wakitumia mwanga wa Hekima.
Uchaguzi wa mwaka huu umetuletea watu wenye viwango mbalimbali vya elimu, tuna watu mbalimbali kutoka vyama tofauti na wote hawa wana mitizamo tofauti katika mambo mengi, na tunao watu wengi wanaoingia Bungeni wakiwa na kila aina ya ujiko. Binafsi katika uchaguzi huu wote swali ambalo ninajiuliza na nitaendeleaa kujiuliza ninaposikia maamukzi yao, ninapofuatilia mipango yao au ninapowaona wao wenyewe ni “je, wamejariwa hekima”?
Tuwaangalie na kuwapima tuone hekima waliyonayo. Lakini zaidi tuwaombee ili hatimaye watambue kuwa wao nao kama Suleiman wanahitaji zaidi hekima. Suleiman alijua anahitaji nini zaidi ili aweze kuwaongoza watu wengi wa Mungu je taifa letu leo hii lenye watu zaidi ya milioni 40 linahitaji viongozi wenye hekima au ndiyo tumekubali iwe “kanyaga twende”?
 
Nimerudi kusoma makala hii niliyoandika mwishoni mwa mwaka jana na imenifanya niamini kweli Watawala wetu wanahitaji kati ya vitu vingi - hii hekima kama ya Suleiman.
 
Nimerudi kusoma makala hii niliyoandika mwishoni mwa mwaka jana na imenifanya niamini kweli Watawala wetu wanahitaji kati ya vitu vingi - hii hekima kama ya Suleiman.


Mwanakijiji watawala wetu inaonekana wao huwa wanaomba wawe matajiri na waweze kuwafurahisha marafiki zao tu. Kwao wananchi ni mzigo
 
Nani aombe Hekima? Fisadi Kikwete? au Lowassa, Mwanakijiji umenea lakini hawa Jamaa wa Magmba wako tayari kuua wananchi wao ili wao wawe Madarakani. Simpendi Kabisa Kikwete kwani hasira nilizokuwa nazo juu ya Fisadi huyo Kikwete siya kusimulia hapa
 
Back
Top Bottom