Kwenye Kipindi changu chote kwenye Tasnia hii ya habari sikumbuki siku nyingine zaidi ya siku ya Jana ambapo ndipo nilipoona Taifa likisimama pamoja kwa lugha moja na kwa kupaza sauti moja. Sauti iliyokuwa ikisika kutokea pande zote za Nchi ilikuwa, "Haki itendeke kwa Bw. Mohamed Ali Kibao". Mzee Ali alikuwa kiongozi wa CHADEMA, Bahati mbaya kurasa zake za uhai zimefungwa kikatili baada ya Uhai wake kufisadiwa na kuporwa na wale "wasiofahamika", katika hali isiyoweza kusimulika kirahisi.
Leo Jumatatu Mzee Kibao atapumzishwa kwenye makazi yake ya Milele, nyuma akituachia Maswali mengi, hofu, wasiwasi na uoga unaofunikwa na fukuto la kutaka kuona hatua zikichukuliwa kwa wote wanaohusika na tukio hilo la kinyama.
Kauli ya Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa jana jioni kupitia mitandao yake ya kijamii akiagiza mamlaka hususan vyombo vya uchunguzi kumpatia taarifa ya kina kuhusu mauaji ya Mzee Kibao imeamsha hisia nyingine mpya ya kutaka uwajibikaji zaidi miongoni mwa wale wanaoonekana kushindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu.
"Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi, serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vua kikatili vya namna hii.", Ujumbe wa Rais ulisomeka.
Wengi wa watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaamini kuwa kauli ya Rais Samia haitoshi, ilihali bado Waziri wa mambo ya ndani Hamad Masauni, Mkuu wa Polisi ya Tanzania IGP Camillus Wambura na Kamishna wa operesheni na mafunzo Awadh Jumbe, wote wapo Maofisini. "Wote wajiuzulu kutokana na wimbi la utekaji na mauaji ya raia nchini", wamesema watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii.
Ismail Jussa Mwanachama wa ACT Wazalendo amenukuliwa akisema "Uchunguzi huru wa kimahakama (Independent Judicial Inquiry) tu tena uwe HURU hasa ndiyo unaweza kutupa ukweli kuhusu matukio haya ya utekaji na mauaji yanayoendelea nchini. Na wakati tunasubiri hatua hiyo, hawa wawili (Masauni na Wambura) wanapaswa kuondolewa bila ya kuchelewa kwa kushindwa kazi!"
Mtumiaji wa mtandao wa X aliyejitambulisha kama Luhaga Mpina amechapisha andiko lake akisema, "Tweet hii ( Ya Rais Samia) ingependeza zaidi kama ingeambatana na utenguzi wa mara moja wa Waziri wa Mambo ya Ndani Masauni na IGP Wambura. Watu hawa wanatia doa baya kwenye uongozi wako. Vitendo vya kutekana na kutishana vimetamalaki mno hali inayoleta hofu kwa Watanzania."
Martin Masese naye kupitia ukurasa wake wa X amesema "Kama kweli RAIS @SuluhuSamia angelikuwa ameumizwa na kukereka na tukio la Mzee #AllyMohammedKibao kutekwa, kuteswa, kuuuwawa na kutupwa UNUNIO, tungeona hadi muda huu kuna watu wamewajibishwa akiwepo MASAUNI. Huwezi kuwa WAZIRI wa mambo ya ndani watu wanatekwa na kuuwawa. NO.
Aidha katika hatua nyingine, baadhi ya wananchi wametaka uboreshaji wa mfumo wa utendaji wa Jeshi la Polisi, wakiamini kuwa hatua hiyo ndiyo itakayoiweka Tanzania na Raia wake kuwa salama kwa kuondokana na vitendo vya mateso, udhalilishaji, ukandamiza, mauaji na utekaji unaoonekana kushamiri kwa siku za hivi karibuni.
Bw. Onesmo Mushi, mtumiaji wa Mtandao wa X anasema "Kuwa na independent oversight body mwenendo wa jeshi la polisi nayo ni kupoteza muda tu. Unaoversee nini ili ureport kwa nani afanye nini? As long as tutaendelea kuwa na jeshi linaloapa kutii amri za watawala, haya matukio hayawezi kuisha.
..... So long as tutaendelea kuwa na katiba inayomfanya Rais kuwa Mungu mtu, polisi wataendelea kutumika kulinda dola tu. Hata ukifanya overhaul ya jeshi zima la polisi leo na kuintroduce structure mpya, bila kugusa madaraka ya kimungu aliyopewa Rais ni kazi bure.
Bw. Onesmo amepingana na Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo Bw. Zitto Kabwe ambaye awali alichapisha taarifa yake akisema "Tume huru ya uchunguzi, Presidential Commission of Inquiry, kwa mujibu wa Sheria ndiyo njia sahihi, bora na ya kuaminika kupata ukweli wa tukio hili na mengine kama hili."