Makala
Lowassa, nionyeshe marafiki zako na mimi nitakuambia wewe ni nani.
Fred MpendazoeToleo la 409
10 Jun 2015
SIKU Edward Lowassa alipotangaza rasmi kugombea urais wa Tanzania nilibahatika kumsikiliza na nilishuhudia umati mkubwa wa watu waliofurika kumsikiliza. Ni kweli yalikuwa ni mafuriko ya watu. Sijui kama walikwenda kwa hiari yao au walilipwa ili waende kwenye mkutano huo.
Hilo sijui wala si ajenda yangu kwenye makala hii. Jambo ambalo ninataka wasomaji wa makala hii walizingatie ni aina ya watu waliokuwepo kwenye mafuriko hayo, kwani ndege wenye manyoa yanayofanana ndiyo wanaoruka pamoja.
Tumeona utawala wa Rais Jakaya Kikwete. Rais aliyeingia kwa hamasa kubwa akibeba matumaini na matamanio ya mamilioni ya Watanzania . Utawala wa Kikwete ulikuja na kila ahadi za kurudisha utukufu wa Taifa. Lakini Kikwete atakapoondoka mwezi wa kumi mwaka huu, Je atakuwa amefanikiwa kurudisha heshima ya taifa letu?
Na wakati wa mchakato wa kugombea urais, Watanzania wengi walimuunga mkono Kikwete hadi baadhi ya viongozi wa dini walifikia kusema alikuwa chaguo la Mungu. Walisema sauti ya wengi ni sauti ya Mungu! Leo ukisema kwamba Kikwete alikuwa chaguo la Mungu, sijui kama Watanzania wengi watakubaliana na wewe. Sijui.
Rais Kikwete alitengeneza mtandao uliomsaidia kuingia Ikulu. Lowassa ametengeneza mtandao unaomsaidia aingie Ikulu. Isipokuwa katika maelezo yake Lowassa, amejitahidi kujitofautisha na Kikwete na hasa aliposema suala la urafiki wao lisihusishwe katika azma yake ya kuomba nafasi ya kuwa rais.
Anawataka Watanzania wampime kama yeye binafsi na wasilihusishe suala la urafiki wao. Sijui kwa nini kwa sasa Lowassa anajitenga na Kikwete. Lakini Watanzania wanakumbuka Lowassa aliwahi kusema urafiki wao si wa kukutana barabarani.
Kwa kuwa Lowassa anaomba nafasi ya nyeti ya urais ni muhimu Watanzania wajiridhishe bila shaka yoyote Lowassa ni nani. Na je anaweza kukabiliana na changamoto zinazolikabili Taifa letu hasa ufisadi, rushwa na kuporomoka kwa maadili.
Mwalimu Nyerere katika kitabu chake, Nyufa, cha mwaka 1995, alisema: Sasa Tanzania inanuka rushwa
tunataka kiongozi anayejua hivyo, ambaye atasema rushwa kwangu mwiko, mwaminifu kabisa kabisa, hawezi kugusa rushwa na
watoa rushwa watamjua hivyo. Lakini hatutaki aishie hapo tu, maana haitoshi wewe mwenyewe uwe mwaminifu
Unaweza ukawa wewe mwaminifu kabisa kabisa, lakini una shinikizo la ndugu zako, jamaa zako na marafiki zako.
Kwa hiyo si inatosha wewe kuwa mwaminifu tu, lakini uwe na uwezo wa kuwaambia jamaa zako kwa kauli ambayo wataiheshimu na hawatarudia tena. Unawaambia jamaa na rafiki zako kwa dhati kabisa
Ikulu ni mahali patakatifu, mimi sikuchaguliwa na wananchi wa Tanzania kuja kupageuza pango la walanguzi na hakuna serikali yoyote duniani inayoongozwa bila miiko.
Zipo taarifa zinazoeleza kwamba fedha nyingi zimetumika katika kufanya maandalizi ya mkutano wa Arusha uliosababisha mafuriko ya watu. Aidha, ndugu Lowassa mara kadhaa amekiri kwamba marafiki zake ndio wanaomchangia kufanikisha safari yake ya matumaini.
Hivyo fedha nyingi anazochangia kwenye harambee kwenye misikiti na makanisani nyingine anatoa yeye na nyingine anachangiwa na hawa marafiki zake ambao wengi wao ni wafanya biashara matajiri na wengi wao ni wale waliotajwa kwenye kashfa za ufisadi na tuhuma mbalimbali.
Hawa marafiki zake Lowassa wamesaidia sana kumjua Lowassa ni nani, kwani wahenga walisema, Nionyeshe marafiki zako na mimi nitakuambia wewe ni nani au wewe una tabia gani.
Hawa marafiki zake na Lowassa wanaweza kuwasababisha Watanzania wamtilie shaka Lowassa kama anaweza kuwa safi na kustahili kupewa dhamana ya kuongoza nchi. Naomba niwakumbushe kauli ya Mwalimu Nyerere kuhusu mmoja wa wagombea urais kwenye NEC Dodoma mwaka 1995, Hapa hatuchagui mtu maarufu, tunachagua mtu safi na huyu si safi.
Kama unapenda sura yake basi nenda kanywe nae chai. Wengine mnasema aaah ni tuhuma tu. Hapa mnasema ni tuhuma tuhuma tu! Lakini mtakumbuka mke wa Kaisari alipotuhumiwa kwa ugoni, Kaisari akaagiza uchunguzi ufanyike.
Uchunguzi ukafanyika na ikabainika kwamba si kweli. Lakini Kaisari bado akamwacha, akasema mke wa Kaisari hapaswi hata kutuhumiwa. Na sisi hapa mgombea wetu hapaswi hata kutuhumiwa wakati wapo wengine wasafi ambao hawana tuhuma.
Kama mtamteua huyu mimi sitapiga kampeni. Siko tayari kumsafisha mtu matope halafu nimwombee kura. Hapana kabisa . Huyu najua si msafi na nchi nzima inajua si msafi. Hafai kuwa mgombea wetu.
Aidha, mtakumbuka pia kuwa mwaka 1995, kundi la Vijana lilimtaka Lowassa ateuliwe kugombea urais wa Tanzania. Hata hivyo, ilitolewa kauli kuwa Lowassa alikuwa na tuhuma za rushwa, kujilimbikizia mali na kupungukiwa na maadili, kinyume na katiba ya CCM na kanuni za chama hicho.
Kamati Kuu ilipopeleka mapendekezo ya kutompendekeza kugombea urais, Lowassa alitetewa kwa makelele, kihuni, bila kufuata taratibu za kikao cha NEC Dodoma. Kundi moja lilikuwa limejiandaa kumpitisha kwa hoja ya nguvu na si kwa nguvu ya hoja.
Waliyatetea maelezo ya Kamati Kuu, lakini waliyakataa yale ya nyongeza aliyoyatoa Mwenyekiti Ali Hassan Mwinyi (Rais wa wakati huo) ambaye alielezea tuhuma hizo zilizokuwa zinamkabili Lowassa. Hivyo, naomba kusisitiza kwamba Lowassa hakuwa chaguo la CCM katika uchaguzi wa mwaka 1995.
Katika kikao hicho cha Kamati Kuu, Mwalimu Nyerere aliamua kusaidia kikao kwa kutoa maelezo ya nyongeza. Aliwauliza wajumbe wa NEC maswali, kwamba wao ni wahuni au ni viongozi wa CCM? Ikiwa wao ni viongozi wa CCM, je, hivyo ndivyo wanavyopaswa kumtafuta mgombea wa urais, kwa makelele?
Kama Watanzania wangewaona walivyokuwa wanafanya katika kikao hicho, je, wangeamini kuwa wao ni viongozi kweli? (Wajumbe walibaki kimya). Kisha Mwalimu aliendelea kusisitiza maelezo aliyoyatoa Mwenyekiti Ali Hassan Mwinyi akisema: Mwinyi amemstahi sana Lowassa.
Hakuwaambia wajumbe wa NEC baadhi ya tuhuma mbaya kabisa kuhusu Lowassa.
Ikiwa NEC inachoombwa ni kuchagua kati ya wenye tuhuma za rushwa kuchaguliwa kwa nafasi ya urais, na wale wasioitaka, basi huu ni wakati muafaka kwao kuipeleka hoja hiyo mbele ya Watanzania waiamue kwa kuwa ndani ya NEC hakuna mwenye uwezo wa kumfukuza mwenzie, wote ni wajumbe sawa kwa mujibu wa katiba ya CCM.
Hatimaye kikao cha NEC kiliondoa jina la Lowassa, kikawateua Benjamin William Mkapa, Cleopa David Msuya na Jakaya Mrisho Kikwete kuwa wagombea. Majina yao yaliwasilishwa kwenye Mkutano Mkuu ambao ndio uliopaswa kumchagua miongoni mwao kuwa mgombea urais wa CCM.
Kwenye Mkutano Mkuu wa CCM, wagombea hao watatu walijinadi kwa wajumbe. Kikwete alipokuwa akijinadi aliwaeleza wajumbe kwamba endapo wangempitisha kugombea na akashinda, angemteua Lowassa kuwa Waziri Mkuu wake.
Lakini hapa pia tujiulize, pamoja na maelezo ya Mwalimu Nyerere na Kamati Kuu kuondoa jina la Lowassa kwa nini bado Kikwete alidiriki kumtaka Lowassa awe Waziri wake Mkuu?
Hapa kwa akili za kawaida inaonekana dhahiri kuwa Kikwete na Lowassa ni marafiki wakubwa. Lowassa Alisha sema urafiki wao si wa kukutana barabarani. Nionyeshe rafiki yako na mimi nitakuambia wewe ni mtu wa aina gani au nitakuambia tabia yako.
Hata hivyo Kikwete hakuchaguliwa kuwa mgombea urais. Historia hii inatoa mfano hai wa jinsi matatizo yanayolikumba taifa letu yalivyoanza.
Ni dhahiri kabisa kuwa watu walewale, wakiongozwa na tamaa zilezile za kuwa matajiri na kutaka urais kwa gharama yoyote hata kuhonga au kutumia fedha, ndio wanaolisumbua taifa letu mpaka sasa.
Ninachotaka kusisitiza hapa ni kwamba, wale wanaoomba nafasi ya urais hawapaswi kutuhumiwa kwa jambo lolote. Hawapaswi kutiliwa mashaka kuhusu uadilifu wao. Wanapaswa kuaminiwa kuhusu dhamira yao ya kupiga vita ufisadi na rushwa.
Na wagombea hawa tunaweza kuwajua kutokana na hulka au tabia za marafiki zao. Katika mafuriko ya Arusha, baadhi ya walioshiriki mkutano huo walitajwa. Hawa walitajwa kuwa ni marafiki wa Lowassa. Wengine walikuwa wamevaa nguo zilizoandikwa Marafiki wa Lowassa.
Baadhi ya marafiki wa Lowassa ni pamoja na Rostam Aziz, Andrew Chenge, Anna Tibaijuka, Cyril Chami, Ezekiel Mayige, David Matayo, Nazir Karamagi na kadhalika.
Baadhi ya marafiki hawa wa Lowassa wengi wao ni wale ambao ama walijiuzuru kwa kupatikana na tuhuma za ufisadi, au wengi wao waliondolewa kwenye nyadhifa zao kwa kashfa za kutokuwa waadilifu.
Na wengi wao ni wafanyabiashara na matajiri. Tunapoliangalia kundi la watu wanaomuunga mkono Lowassa, tunaweza kujua Lowassa ni nani. Tukiliangalia kundi linalomuunga mkono Lowasssa tunaweza kujua kama Lowassa akiingia Ikulu atapambana na rushwa na ufisadi au ataenda kufanya biashara.
Je, marafiki wa Lowassa anaowataja na walioonekana kwenye mafuriko ya Arusha wanakerwa na rushwa na ufisadi kwa dhati?. Ndege wenye manyoya yanayofanana ndio wanaoruka pamoja.
Watanzania tukumbuke kwamba utumishi wa umma ni dhamana na fursa adhimu kwa ajili ya kulinda na kutetea maslahi ya wananchi wote. Haya ni maneno aliyoyasema Rais Barack Obama baada ya kula kiapo cha kuongoza Marekani.
Inawapasa wale wanaopata nafasi za kuchaguliwa wafahamu kwamba wamepewa dhamana ya kuwatumikia wananchi na si nafasi ya kujitajirisha au kumnufaisha ndugu au marafiki. Kutokana na kumomonyoka kwa maadili na moyo wa uzalendo nchini, uongozi umegeuzwa kuwa nafasi ya kujitajirisha. Urais, uimekuwa fursa ya uwekezaji, na wala si fursa ya kuwatumikia wananchi.
Ukweli kwamba kuna matajiri au watu wanaotumia pesa kumiliki siasa na uongozi katika nchi yetu, ni jambo lililo wazi. Zipo taarifa kwamba baadhi ya watu wanaokwenda kwenye mikutano ya watia nia ya urais mfano waliofurika Arusha walinunuliwa waende kwenye mkutano, walilipwa wapige kelele Rais, Rais.
Matumizi makubwa ya fedha yalionekana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Baada ya kutangazwa mshindi wa kiti cha urais katika uchaguzi huo, Kikwete, alizindua Bunge Desemba 30, 2005 alidhibitisha hili alisema: Yameanza mawazo kuwa uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha.
Tusipokuwa waangalifu, nchi yetu inaweza kuwekwa rehani kwa watu wenye fedha za kununua uongozi au wanaoweza kupata fedha za kufanya hivyo, maana unaweza kufadhiliwa na mtu ili ununue uongozi, ni vema sasa tulishughulikie suala hili.
Kuna mawazo kwamba sasa Tanzania inahitaji Rais tajiri. Ninapenda niwakumbushe wosia alilowahi kuutoa Mwalim Nyerere wakati wa uhai wake juu ya hatari ya watu wachache wenye pesa kujaribu kutafuta uongozi kwa manufaa yao.
Alisema: Tanzania halijawa taifa imara sana na adilifu kiasi cha kuruhusu matajiri kuingia kwenye uongozi wa nchi kama ilivyo Marekani na Ulaya. Wakati huo bado uko mbali sana na tukitaka kuuvuta kwa kamba huko ndiko kuliingiza taifa letu changa kwenye kiwango cha ufisadi.
Mgombea mmoja wa urais amesema bado anasaka utajiri na anaomba aende Ikulu. Je Ikulu kuna biashara gani itakayompatia utajiri? Na wale wanaomuunga mkono atawalipaje akienda Ikulu?
Nchi kuwekwa rehani kwa matajiri ni jambo la hatari sana, kwa maana serikali itaongozwa na matajiri na haitawajibika kwa wananchi. Hili limeanza kujitokeza. Demokrasia itakoma na udikteta utatawala.
Jambo linalojitokeza hapa na ambalo ni matokeo ya matumizi makubwa ya fedha na rushwa kwenye chaguzi, ni kupatikana kwa viongozi ambao hawakuchaguliwa na wananchi bali walinunua uongozi au waliotoa rushwa kushawishi wapiga kura wawape uongozi.
Serikali inayopatikana kwa rushwa haiwajibiki kwa wananchi. Hutumikishwa na matajiri walionunua uongozi na waliotoa rushwa. Serikali hiyo huwaabudu matajiri walioiweka madarakani, haiwezi kufanya maamuzi yenye maslahi kwa wananchi.
Serikali hiyo hulinda maslahi ya watu wachache, haiwezi kuchukua hatua dhidi ya ufisadi. Baadhi ya maamuzi ambayo yamekuwa yakitolewa na utawala wa awamu ya nne, ripoti ya hivi karibuni ya Ikulu ya TOKOMEZA na ESCROW ni ushahidi wa ninachokieleza.
Tuwe makini na wagombea wanaotumia fedha nyingi na wanaopewa fedha nyingi na marafiki zao katika mchakato wa kutafuta nafasi za kuchaguliwa urais, ubunge na udiwani. Tumejifunza katika utawala wa awamu ya nne. Tusirudie makosa.
Ningependa kusisitiza, Watanzania tunatakiwa tuichukie rushwa ya aina yoyote. Rushwa ni dhambi na mshahara wa dhambi ni mauti. Rushwa hupofusha macho na moyo. Taifa linaoendekeza rushwa ni taifa ambalo watu wake ni sawa na vipofu na wafu.
Vipofu ambao hawaoni madhara ya rushwa na mioyo yao imekufa. Rushwa inapotolewa na kupokelewa kwa shangwe makanisani na misikitini na wagombea wa vyama vya siasa ni ushahidi wa jambo hili.
Tanzania ina nafasi ya kuwa Taifa linaloheshimika kama tutaichukia rushwa na kukataa kuipokea au kuitoa. Mfalme Suileman aliwahi kusema; haki huinua taifa bali dhambi na uovu ni aibu ya watu wote. Rushwa ni dhambi na ni aibu kwa watanzania wote.
Tanzania imepoteza heshima kwa sababu ya rushwa. Pia napenda kusisistiza, Kwenye nchi ambapo rushwa imetawala sauti ya wengi si sauti ya Mungu. Sauti ya wengi ni sauti ya Mungu kwenye nchi ambapo haki, usawa na upendo vinatamalaki.
Mafuriko ya watu kule Arusha kama walilipwa ili waende kwenye mkutano sauti yao si sauti ya Mungu. Na, Je Lowassa ana dhamira ya kweli ya kuchukia rushwa?
Nionyeshe marafiki zake na mimi nitakuambia kama Lowassa ana dhamira ya kweli ya kupiga vita rushwa na ufisadi. Niliposikiliza akisema atapiga vita ufisadi, rushwa na atahakikisha rasilimali za nchi hii zinawanufaisha Watanzania na nilipowangalia marafiki zake ni nani, nilitambua anachokifanya ni usanii. Hana dhamira ya kweli na anachokisema.
Lowassa hafai kuwa Rais.
Tufuatilie mtandaoni:
Wasiliana na mwandishi
Fred Mpendazoe
fmpendazoe@hotmail.com
Mwandishi aliwahi kuwa mbunge wa chama tawala cha CCM kabla ya kujiondoa na kuhamia Upinzani. Kwa sasa yuko CHADEMA.
Endelea Kuhabarika
Ya Lowassa na kizaazaa cha rushwa
Ya Lowassa na kizaazaa cha rushwa II
Uchaguzi wenye rushwa huzaa serikali ya