real G
JF-Expert Member
- Feb 7, 2013
- 5,227
- 5,303
Amancio Ortega Gaona ni mfanyabiashara mkubwa sana wa nchini Hispania na kwa sasa ndiye mtu tajiri zaidi duniani kwa mujibu wa jarida la Forbes, akiwa na makadirio ya utajiri wenye thamani ya kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 79.5 mpaka kufikia tarehe 9 mwezi Septemba mwaka 2016. Amancio amezaliwa tarehe 28 mwezi Machi katika mji wa Busdongo de Arbás, León, Hispania. Ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto 4, na muda mwingi wa maisha yake ya utotoni amekulia katika mji huo aliozaliwa.
Ortega aliacha shule na kuhamia La Coruña akiwa na umri wa miaka 14, kwa sababu ya kazi aliyokuwa akifanya mzee wake katika shirika la reli. Baada ya muda kidogo alipata kazi katika duka la kushona mashati lililoitwa Gala na hapo ndipo alipojifunza jinsi ya kutengeneza nguo kwa mikono.
Maisha yake ya sasa yako mjini Galicia, huko huko Hispania, na anakaa na mke wake wa pili . Ortega ni mwanzilishi na mwenyekiti wa Inditex Fashion Group ambayo ni maarufu sana kwa bidhaa zake zinazotambulika kama ZARA ambazo ni nguo na vitu vingine kama viatu, urembo n.k.
Mnamo mwaka 1972, aliweza kuanzisha Confecciones Goa (Goa – ikiwa na herufi za kwanza za majina yake) ambayo ilikuwa inajishughulisha na uuzaji wa mataulo, ambapo Ortega aliweza kutengeza kwa kuwatumia maelfu ya wanawake katika mashirika yaliyoko katika mji huo.
1975, alifanikiwa kufungua duka lake la kwanza la ZARA akiwa na mkewe Rosalía Mera. Na sasa ZARA ni sehemu ya the Inditex Group (Industrias de Diseño Textil Sociedad Anónima) ambapo Ortega anamiliki 59.29%, bila kusahau maduka zaidi 6,000 ambayo yote sio nguo na yanayojumuisha Brands kama Zara, Massimo Dutti, Oysho, Zara Home, Kiddy’s Class, Tempe, Stradivarius, Pull and Bear, Bershka na wafanyakazi zaidi ya 92,000.
Ortega hupenda kuishi kawaida sana, mpaka 1999, hakukua na picha yake yoyote iliyochapishwa. Hapendi kabisa kuvaa tai na mara nyingi huvaa koti la blue, shati jeupe na suruali ya kijivu. Na zote zio nguo kutoka maduka ya ZARA. Na inasemekana huenda sambamba na watu wake wanatengeneza nguo kuanzia kwenye kubuni mpaka wakati wa matengenezo katika kampuni hiyo.
Mwaka 2000, alijitokeza katika kadamnasi kama kujiandaa na maandalizi ya kampuni yake kujitangaza katika soko la hisa mwaka 2001. Ilikua ni habari iliyojitokeza sana kwenye vyombo vya habari vya biashara huko Hispania. Aidha, Ortega amewahi kufanya mahojiano na waandishi watatu tu maishani mwake na siri zake hizo za kibishara na maisha, zilipelekea kuchapishwa kwa kitabu kama Amancio Ortega: de cero a Zara (From Zero to Zara).
Na ilipofika mwaka 2011, Ortega alitangaza kustaafu na kutoka Inditex ambayo ni kampuni mama ya bidhaa za ZARA, na kumuachia Makamu wa Rais na CEO Pablo Isla kuchukua nafasi yake katika kampuni hiyo. Na mwaka 2012 Ortega alichangia Euro milioni 20 kwa Caritas Internationalis, ambalo ni Shirika la misaada ya Kikatoliki.
Kwa hisani ya Swahili Times