Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema Taifa (Bavicha), umemalizika kwa kumchagua John Heche (pichani) kuwa mwenyekiti mpya wa baraza hilo, ambaye anamrithi Mbunge wa Ubungo kupitia chama hicho, John Mnyika.
Alichaguliwa usiku wa kuamkia jana katika mchuano mkali wa uchaguzi huo uliofanyika viwanja vya PTA Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Heche ameshinda kwa kupara kura 143 kati ya kura 264.
Wagombea waliopitishwa na Kamati Kuu kuwania nafasi hiyo walikuwa tisa lakini watatu kati yao walienguliwa na kamati ya wazee kwa tuhuma za rushwa na kujenga makundi.
Makamu Mwenyekiti kwa upande wa bara amechaguliwa Juliana Shonza kwa kupata kura 115 kati ya kura 214, wakati Makamu Mwenyekiti Zanzibar amechaguliwa Sharifa Hamis kwa kupata kura 170 kati ya kura 265.
Mjumbe wa Baraza Kuu Zanzibar amechaguliwa Zainab Bakari aliyepata kura 180 kati ya kura 263 na kwa upande wa Tanzania bara waliochaguliwa kuingia kwenye Baraza Kuu la Bavicha ni Alex Mushi kura 80, Edward Kinabo 96, Frank Fumpa 66 na Sabrina Sungura ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum aliyepata kura 109.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Mabere Marando, alisema jana kuwa alitangaza matokeo hayo jana saa 12:00 asubuhi kwani shughuli nzima ya uchaguzi huo ilifanyika usiku kucha.
Alisema walipitishwa na Kamati Kuu kuwania nafasi ya mwenyekiti walikuwa tisa lakini kutokana na mienendo ya rushwa na vitendo visivyo vya kimaadili waliamua kuwaengua wagombea watatu.
Aliwataja wagombea walioenguliwa kuwa ni Grayson Nyakarungu kutoka Serengeti, Bernard Saanane wa Kilimanjaro na Metali Mwampamba, ambao alisema waligundulika kukiuka maadili.
Kamati Kuu ilipitisha majina tisa lakini ilitupa madaraka ya kukata majina ya watu ambao mienendo yao tutaona haifai, kamati hiyo ya wazee watatu, mimi, Edwin Mtei na Bob Makani, sasa tulifanya uchunguzi na kuwahoji baadhi ya wagombea tuliohisi wanafanya kampeni chafu na tukajiridhisha ndo maana tukawaondoa, alisema.
Alisema baadhi ya wagombea walikuwa wakifanya kampeni katika hoteli mbalimbali jijini Dar es Salaam na kuunda makundi ambayo alisema yalikuwa hatari kwa umoja wa chama hicho.
Akizungumza na NIPASHE mara baada ya kuchaguliwa, Heche alisema baraza lao lina mikakati ya kupigania haki, kupinga rushwa na kulinda haki za Watanzania.
Alisema wiki ijayo litaundwa Baraza la vijana kwa kuungana na wajumbe wa baraza kuu la Chadema.
Alisema ni mara yao ya kwanza kuunda Baraza la Vijana na kwamba watahakikisha wanakuwa mfano kwa taifa kutetea haki za wanyonge.
Mwenyekiti huyo alisema atashirikiana na wananchi katika nafasi hiyo ili kutimiza malengo yenye manufaa kwa jamii nzima.
SOURCE: NIPASHE 2011