Wasichana 4,000 kufukuzwa shule kisa mimba, haikubaliki | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wasichana 4,000 kufukuzwa shule kisa mimba, haikubaliki

Discussion in 'Jukwaa la Elimu (Education Forum)' started by MziziMkavu, Jun 25, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jun 25, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,615
  Trophy Points: 280
  Habari kwamba zaidi ya wanafunzi 4,000 wa shule za msingi na sekondari nchini kote wamekatisha masomo yao kati ya mwaka 2010/2011 kutokana na sababu za kubeba ujauzito kitendo ambacho ni kinyume cha kanuni za uendeshaji shule nchini, ni za kushtua na kusikitisha sana.


  Habari hizo zilizoandikwa na gazeti hili jana zilifichuliwa na Shirika la Utafiti wa Kitabibu la Afrika (AMREF) katika kongamano la ‘afya ya uzazi ni haki ya kijana, tuitetee’ lililofanyika mkoani Iringa mapema wiki hii, na kuhamasisha jamii kutambua tatizo linalokabili watoto wa taifa hili.


  Katika kongamano hilo, ilielezwa kuwa mimba hizo kwa kiwango kikubwa zinachangiwa na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi kwa wanafunzi hivyo kusababisha wasichana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 19 kukatisha masomo yao kutokana na kupata mimba na kuozwa katika umri mdogo.


  Ingawa ukosefu wa elimu hiyo ni moja ya changamoto za tatizo hilo, lakini pia mifumo ya kisera na sheria nayo kwa upande mmoja imechangia ama kuwadidimiza watoto wa kike kuingia katika mitego ya kubeba ujauzito na hata wakati mwingine kuchukuliwa kimzaha tu ndani ya jamii kuwa ukatishwaji wa masomo kwa sababu ya mimba siyo jambo linalostahili kutazamwa kwa darubini kali ndani ya jamii ili kunusuru watoto wa kike katika janga hilo.


  Hakuna ubishi kuwa wanafunzi 4,000 wasichana ni wengi kwa maana nyingi, kwanza idadi hiyo ni kubwa hasa inapokuwa ni ya mwaka mmoja tu, pili, ni kubwa hasa inapotazamwa kwa maana ya idadi ya wasichana wanaobahatika kupata elimu nchini kwani mbali ya kuwa wengi kuliko wavulana, mila na desturi zinawanyima fursa ya kusoma.


  La tatu na la umuhimu mkubwa ni kwamba idadi hiyo inazidi kuthibitisha pasi na shaka yoyote kwamba ingawa tendo la kutunga mimba linahusisha watu wawili, tena wa jinsia mbili tofauti anayeadhibiwa ni mmoja kati yao, na huyu ni msichana kwa kuwa tu ni rahisi kuthibitisha kwamba ana mimba lakini mvulana au mwanaume aliyehusika na ujauzito huo huachwa bila kupatwa na madhara yoyote.


  Katika mifumo yetu kama taifa tumejijenga kuonyesha kuwa mimba ni mzigo wa msichana au mwanamke, ndiyo maana hata pale msichana anapojua wazi kuwa muhusika wa mzigo huo ni nani, mara nyingi yeye mwenyewe au kwa kushauriwa huchelea kumtaja kwa matarajio ama ya kutokuvuruga mahusiano au kuwa mtoto atakayezaliwa atakosa matunzo kutoka kwa baba yake, hali hii imefanya tatizo la mimba shuleni kuwa la wasichana na siyo la wavulana.


  Kwa upande mwingine ukitazama sheria zetu, kama vile Sheria ya Elimu namba 25 ya mwaka 1978, inasema wazi kuwa mwanafunzi haruhusiwi kuolewa akiwa shuleni, tafsiri ya sheria hii kwa wingi ni kwamba mimba ni matokeo ya ndoa na hivyo wanaokutwa nazo hufukuzwa shule, lakini mwamume aliyempa mimba atashitakiwa mahakamani na ili afungwe kifungo cha miaka 30; hapa pia kuna udhaifu mkubwa.


  Kwa mfano kama kweli wasichana 4,000 walipewa ujauzito wakiwa shuleni mwaka 2010/11 ni jambo la kushangaza kuwa hakuna idadi yoyote ya maana ya wanaume waliofungwa jela kutokana na mimba hizo, hali hii inaonyesha kuwa adhabu zinazotolewa kwanza hazilengi kujenga na kumsaidia msichana ambaye anaathirika zaidi katika suala zima la kubeba ujauzito, pili linaweka mazingira magumu mno kwa mwanamume kukamatwa katika kosa hilo; ni wasichana wachache wenye ujasiri wa kuwataja waliowapa mimba, pia hawaoni faida zake ni bora kuficha ukweli kwa matarajio ya huduma kutoka kwa muhusika baada ya mimba.


  Tunakumbuka kuwa kwa kutambua jinsi sheria namba 25 ya Elimu ya mwaka 1978 inavyowakandamiza watoto wa kike wakiwa shuleni wapatapo ujauzito, mwaka 2008 Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania alitoa tamko (Presidential Decree) ambalo lina nguvu ya kisheria kwamba wasichana wote wanaopata ujauzito wakiwa shuleni, waruhusiwe kuendelea na masomo baada ya kujifungua.


  Pamoja na uzuri wote wa tamko hili, ni vigumu leo miaka minne badaaye kusema kwa uhakika ni kwa kiwango gani watoto wa kike wamenufaika na tamko hilo kwa kurejea shuleni baada ya kujifungua.


  Ni vigumu kwani hata takwimu tunazozungumzia hapa ni za mwaka 2010/11, kwa hali hiyo mambo bado ni mabaya kwa watoto wa kike. Inajulikana wazi, ukimwelemisha mtoto wa kike umeelemisha jamii, ni jambo la kushangaza kwamba pamoja na ukweli huu kuwa dhahiri, bado watoto wa kike wameendelea kunyanyapaliwa ndani ya nchi hii. Tubadilike sasa.

  CHANZO: NIPASHE
   
 2. Madela Wa- Madilu

  Madela Wa- Madilu JF-Expert Member

  #2
  Jun 25, 2012
  Joined: Mar 24, 2007
  Messages: 3,074
  Likes Received: 35
  Trophy Points: 135
  Ni udhaifu wa serikali ya Kikwete.

  Kwa serikali ya CCM 4000 ni tarakimu.

  lakini je iweje tunapewa idadi ya wasichana 4000 na hatupewi idadi ya wanaume 4000 waliowapa mimba??

  Tungependa kujua ni akina nani? wana umri gani wanafanya shughuli zipi na ni viongozi au ni wananchi wa kawaida?


  Mimba hazipatikani kwa kuvuta hewa, zinapatikana kwa kujamiiana.

  Nionavyo mimi watia mimba wanalindwa kwa nguvu zote zitokanazo na utendaji dhaifu wa serikali ya CCM.
   
 3. Lekanjobe Kubinika

  Lekanjobe Kubinika JF-Expert Member

  #3
  Jun 25, 2012
  Joined: Dec 6, 2006
  Messages: 3,067
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 135
  Hizo mimba wamejipa wenyewe? Nilitaraji waseme wanafunzi 8000 maana mambo ni wawiliwawili. Tena mimba zingine ni za walimu wao na makatibu watendaji wa ngazi mbalimbali wa vyama na serikali. Nyingine chache ni za wanafunzi wenyewe kwa wenyewe wakisisitiza ushirikiano wao shuleni. Kuongezeka namba hiyo ni hasa baada ya shule za JK ambazo kuta na paa la darasa likijengwa huitwa shule pasipo kujali mtoto na usalama wake shuleni na anpokaa na anafundishwaje. Nchi hii imejaa usanii tu.
   
Loading...