• Wabunge CCM, wapinzani wazozana
na Tamali Vullu, Dodoma
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Samuel Sitta, jana alijikuta akizomewa na wabunge wa kambi ya upinzani huku wakimwita msaliti, kwa kuwa mmoja wa waasisi wa chama kilichonyimwa usajili cha CCJ.
Wabunge hao walifikia hatua hiyo baada ya Sitta mwenyewe kuanza kuwaambia wabunge wa kambi hiyo kwamba ni wanafiki kwa kukataa posho wakati baadhi yao wamekuwa wakipokea kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Majibu ya Sitta ambaye amekuwa kiongozi wa shughuli za Bunge akikaimu nafasi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, yalikuja wakati akitoa ufafanuzi wa kauli iliyoibua zogo ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR- Mageuzi), kwamba serikali ya Rais Jakaya Kikwete ni legelege kwa vile imeshindwa kukusanya kodi.
Hata alipotakiwa na kiti cha Spika kufuta kauli hiyo, Kafulila alikataa na kusisitiza kwamba yuko tayari kufa, ndipo Sitta alipoamua kusimama kutuliza mzozo huo.
Sitta ambaye wiki iliyopita alitumia nafasi hiyo kumshambulia Edward Lowassa, alisimama na kuwasihi wabunge wa CCM kuwa watulivu, kwani wapinzani kazi yao ni kubeza kila kitu kinachofanywa na serikali.
"Wabunge wa upinzani kazi yao ni kubeza kila kitu kinachofanywa na serikali, lakini sisi tutahukumiwa na wananchi. Siku zote wapinzani mambo yao ni ya unafikinafiki," alisema Sitta na kuibua zogo zaidi.
"Nitatoa mfano, baadhi yao wanadai posho za vikao ni kuwaibia wananchi, lakini wapo baadhi yao walichukua posho hizo miaka mitano iliyopita. Warejeshe posho hizo ndiyo wananchi watawaelewa… na wataendelea kuwa wapinzani," alisema.
Hata hivyo, maelezo ya Sitta hayakuweza kuzima mzozo uliokuwapo kwani wabunge wengi wa upinzani walisimama wakitaka mwongozo wa mwenyekiti, lakini aliahirisha Bunge kutokana na muda wa kikao kwisha.
Licha ya muda kwisha, baadhi ya wabunge wa upinzani waliwasha vipaza sauti na kuanza kumzomea kwa kumwita msaliti kwa vile alikuwa mmoja wa waasisi wa CCJ. Katika zomeazomea hiyo, wabunge hao walikuwa wakiimba CCJ, CCJ.
Kabla ya Sitta kuingia kwenye mzozo huo, kauli ya Kafulila kwamba serikali ya Kikwete ni legelege, ilionekana kuwakera sana wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kutokana na kauli hiyo, Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangwala, alisimama na kuomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Mhagama, akimtaka Kafulila kufuta kauli hiyo kwa kuwa ni ya kuudhi.
"Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mbunge afute kauli kuwa serikali ya CCM ni legelege na haijashindwa kukusanya kodi. Kauli hii imeniudhi, serikali inakusanya kodi na imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka," alisema.
Baada ya maelezo hayo, Mwenyekiti Mhagama alimtaka Kafulila kufuta kauli hiyo, lakini alikataa kwa maelezo kuwa maneno hayo ni nukuu ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Pia alisema mpaka sasa serikali haijafanikiwa kuongeza kiwango cha kodi kwani wakati ikikusanya kiwango hicho dola moja ilikuwa sh 1,000, lakini sasa dola imepanda na kufikia sh 1,600.
Kutokana na maelezo hayo, Mhagama alisema kuwa hoja ya Kafulila ina mantiki, lakini haiendani na maelezo aliyokuwa akitoa, kwani ameitumia vibaya nukuu hiyo na kusisitiza Kafulila kufuta kauli hiyo.
Wakati Mhagama akieleza hayo, baadhi ya wabunge walikuwa wamewasha vipaza sauti vyao na kusikika wakipinga suala hilo huku wale wa CCM wakibeza hoja hiyo.
Pamoja na hayo, Kafulila alieleza kushangazwa na hali hiyo na kusema huo ndio ukweli na kwamba yupo tayari kwa lolote.
"Nashangaa tunachukua muda mrefu kujadili suala hili. Huu ni ukweli mchungu na nipo tayari kuufia," alisema Kafulila.
Awali akichangia hoja ya bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Kafulila alisema inasikitisha kuona kuwa wakati nchi inaelekea kusherehekea miaka 50 ya Uhuru, bado bajeti ya sekta ya afya ni tegemezi.
Alisema hali hiyo inatokana na tatizo la kimtazamo katika serikali na kumtaka waziri asikubali bajeti ndogo na hata ikiwezekana ajiuzulu.
"Leo dunia nzima sisi ndio tuna uwiano mbovu kati ya daktari na wagonjwa. Ni aibu bajeti ya sekta ya afya kuwa tegemezi kwa asilimia 97. Haiwekezani.
"Serikali haitozi kodi. Serikali imeshindwa kukusanya pesa, inasikitisha kwa sababu sekta ya afya inahusu maisha ya Watanzania," alisema.
Kafulila alisema hazungumzii suala hilo kama mpinzani, bali ni ukweli na kuongeza kuwa serikali hata inashindwa kuwekeza katika masuala mengine ya afya kutokana na utegemezi.
"Kuna matatizo mengi zaidi ya ukimwi, lakini kutokana na kuwa tegemezi tunashindwa kuwekeza katika masuala mengine ya kiafya," alisema.
Mbunge huyo alieleza kuwa watoto wa wabunge na mawaziri wanatibiwa katika hospitali bora ndani na nje ya nchi, lakini watoto wa wanyonge wanatibiwa katika hospitali ambazo hazina hata dawa.
Kutokana na kauli hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, alisimama na kuomba mwongozo wa mwenyekiti na kumtaka mbunge huyo kutotoa kauli za jumla jumla.
Kauli hiyo ya Maige, iliibua minong'ono miongoni mwa wabunge wa upinzani na mwenyekiti kusimama na kuwataka wabunge kuheshimu nidhamu ya Bunge.
Baada ya maelezo ya mwenyekiti, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu, alisimama na kuwataka wabunge kuzungumza kwa nidhamu.
"Mtoto wangu ni daktari Muhimbili na wanangu wanatibiwa katika hospitali za kawaida. Baba yangu anatibiwa
Hospitali ya Katesh na mimi natibiwa huko, naomba Kafulila ukubali taarifa hii," alisema Nagu.
Hata hivyo, Kafulila alikataa taarifa hiyo na kuongeza kuwa familia ya mbunge na waziri zinatibiwa bure.
"Hii ndiyo sababu inayofanya msiwekeze kwenye sekta ya afya… waziri wakati mwingine usikubali bajeti ndogo namna hii, hapa tutakuchanachana shati," alisema.
Kafulila alisema inawezekana serikali kuwekeza katika sekta ya afya vijijini, kwani nchi hii ni tajiri.
"Tanzania ni nchi tajiri, lakini ni taifa la saba kwa kupatiwa misaada duniani, tunaongozana na nchi zenye machafuko. Haiwekezani," alisema huku akionyesha jarida la Ecomomist.
Akizungumzia bima ya afya, Kafulila alisema kitendo cha kutopatikana dawa ni utapeli kwa wananchi.