Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,810
- 15,398
Picha haihusiani na habari hii..........
Kuna wakati mmeshawahi kusikia watu wakilalamika kwamba mume fulani amemuacha mkewe ambaye ana tabia nzuri, mcheshi, mvumilivu, mwaminifu na mweledi (anayeelewa mambo). Ukweli ni kwamba hizo ni tabia nzuri na zinachangia sana kwenye kuimarisha ndoa, lakini bado hazina maana sana kama mke hataweza kujua namna nzuri ya kuonyesha upendo wake kwa mume.
Kuna makosa ambayo hufanywa na wanawake katika juhudi yao ya kuonyesha upendo kwa waume zao bila wenyewe kujua kwamba wanafanya makosa. Ngoja niyadadavue makosa ambayo wanawake wengi huyafanya wakijua wanawaelewa waume zao:
1. Kwa mfano, mwanaume hajipendi, mwanamke anapojaribu kuikemea tabia hiyo anakuwa anajenga ukuta mkubwa sana kati yao bila yeye kujua. Inashauriwa, badala ya kumwambia moja kwa moja mumewe kwamba aache kutojipenda, inashauriwa ni vyema akamnunulia mumewe nguo na akizivaa amsifie sana kiasi kwamba mwanaume huyo atajiona kuwa kumbe akivaa nguo za kiwango au mtindo fulani anakuwa katika hali ya kuvutia kupita kiasi. Hapo mwanaume naye atajaribu kununua aina hiyo ya nguo. Kwa wanawake ambao waume zao wana tabia ya kutojipenda kimavazi wanaweza kujaribu hata leo ili wapime matokeo ya ujanja huu.
2. Wanawake wanafanya makosa pale wanaposhindwa kushukuru juu ya yale mazuri wanayotendewa na waume zao na badala yake kulalamika kwa yale ambayo hawakutendewa. Utakuta mwanaume anajaribu kufanya hiki na kile kwa sababu ya upendo alio nao kwa mkewe, lakini mwanamke huyo hata mara moja hashukuru au kuonyesha kwamba anathamini juhudi hizo za mumewe. Lakini pale mwanume anaposhindwa kumfanyia hiki au kile iwe ni kwa bahati mbaya au makusudi mwanamke hukata kama wembe kwa kauli zake za kulaani na kulalamika. Ni lazima wanawake wafahamu kwamba kwa maumbile wanaume hupenda sana kuonekana kuwa wamefanya mazuri au ni mashujaa kwa wake zao.
3. Kuna wanawake hawajui asante kwa waume zao hawajui kuonyesha kwamba walichofanyiwa hata kama ni kidogo wamefurahi na kukikubali. Wanawake hawa kwa bahati mbaya wakati huo huo huwa hawajui kuacha kulaumu pale wanapoona hawakufanyiwa yale waliyotarajia kufanyiwa na waume zao. Mwanamke anapaswa ajifunze kusema asante na kuonyesha kwamba ameridhika na alichotendewa na mumewe. Ajifunze pia kuacha kulalamika sana pale ambapo hakutendewa alichopaswa kutendewa.
4. Kuna wanawake ambao hupenda sana kuwaelekeza waume zao jinsi ya kufanya au hata kusema mambo fulani. Hebu fikiria juu ya mke ambaye anamuelekeza mumewe kwamba akioga bafuni asimwage maji hovyo kwa sababu kupiga deki ni taabu. Haya ni maelekezao ambayo humrudisha mume katika hali ya kuhisi kuwa yeye ni mtoto mdogo ambaye anapaswa kurekebishwa na kuelekezwa kipi na kipi siyo cha kufanya. Mume hapa atajihisi kabisa kwamba hapendwi kwani haoni kama anathaminiwa, ni mtoto mdogo.
5. Wanawake huwa wanakosea sana pale wanapoeleza kukerwa hisia zao kwa kuuliza maswali ambayo hayana majibu, maswali ya kupita, ambayo siyo ya moja kwa moja kuhusiana na maudhi .. unawezaje kufanya hivyo! Ni vizuri mwanamke akaelezea kilichomkera moja kwa moja kuliko kutumia njia ya kuzunguka ya maswali yasiyo na majibu. Sijui ndiyo nikueleweje? Ni miongoni mwa maswali haya yasiyompendeza mwanaume.