Elections 2010 Wanavyonisema Na Mbwa Yule Wa Manzese!

herrypeter1

JF-Expert Member
Jan 17, 2009
223
29
Mwalimu Nyerere alipata kusimulia kisa cha mbwa wa Manzese. Nilikuwa bado kijana mdogo sana niliposikia kisa kile. Ilikuwa mwanzoni mwa miaka ya 80. Ni kwenye kilele cha Sherehe za Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi. Sherehe zile zilifanyika pale Uwanja wa Taifa. Nilibahatika kuwapo uwanjani.

Baadhi ya mabango ya wafanyakazi yaliyopita mbele ya Mwalimu siku ile yaliwakilisha ujumbe juu ya hali ngumu ya kimaisha iliyokuwa ikiwakabili wafanyakazi; mishahara midogo na mengineyo.

Wakati huo, Serikali ya Mwalimu ilikataa masharti ya Shirika la Fedha Duniani na Benki ya Dunia pia. Hii ni kwa sababu, licha ya athari nyingine mbaya kwa masharti hayo kwa nchi yetu, uhuru wetu wa kujiamulia mambo yetu nao ulikuwa hatarini.

Ilipofika wakati wa kutoa hotuba yake, Mwalimu Nyerere alisema;

“ Ndugu zangu watu wa Dari Salama ebu nisikilizeni; kulikuwa na mbwa wawili, mmoja wa Manzese na mwingine wa Oysterbay. Ikatokea siku moja mbwa wa Manzese akatembea hata akafika Oysterbay.

Kwenye moja ya nyumba za huko Oysterbay akamwona mbwa mwenzake aliye ndani ya geti. Mbwa yule wa Manzese akasogea getini huku akimshangaa mbwa wa Oysterbay. Mbwa yule wa Oysterbay alinenepeana huku manyoya yake yakiwa yameteremka hadi machoni. Mbwa wa Oysterbay naye alimshangaa mwenzake wa Manzese. Mbwa yule wa Manzese alionekana kukondeana huku masikio yake yakiwa yameteremka hadi shingoni. Mbwa wa Oysterbay kwa mshangao akamwuliza mwenzake wa Manzese; “ Hivi nawe ni mbwa kama mimi?!
“Naam, miye ni mbwa kama wewe.” Alijibu mbwa wa Manzese.
“ Sasa mbona umekondeana hivyo, njoo humu ndani kwa bwana wangu nawe uwe kama mimi.”
Mbwa wa Manzese akajibu;


“ Lakini wewe umefungiwa, mwenzio niko huru!”

Sitakisahau kamwe kisa kile alichosimulia Mwalimu Nyerere pale Uwanja wa Taifa. Naamini katika alichokisema Mwalimu. Nitaendelea kuamini hivyo hata katika muda wangu uliobaki humu duniani. Mwalimu alizungumzia dhana ya uhuru. Ingawa ni neno fupi sana, lakini neno uhuru lina maana kubwa. Asiye na uhuru ni mtumwa.
Mimi ni mtu huru. Na siku zote nimepigania nibaki kuwa mtu huru. Kwa uhuru kabisa nakutana na kuongea na watu wengi; vijijini na mijini. Nakutana na kuongea na wasomi na wasio wasomi, matajiri na masikini. Sijapata maishani mwangu kulazimishwa au hata kulipwa ujira ili niongee au niandike mawazo yasiyo yangu au nisiyokubaliana nayo.
Ni bahati mbaya pia, katika jamii yetu, kila anayeandika makala magazetini kama nifanyavyo, basi, atasemwa kuwa ni mwandishi wa habari. Wengi hawatofautishi baina ya mwandishi wa habari na mwandishi wa makala.

Napenda sana kuandika fikra zangu huru kwa azma ya kuchochea mijadala. Jana niliandika fikra zangu kwenye Jamii Forums. Nimefanya hivyo huko nyuma. Lakini jana nimepata watu wengi walioshiriki mjadala. Wametoa fikra zao, kuna walionitukana pia. Nimeshazoea. Nayasoma matusi hayo, nikiamini, hata kwenye matusi hayo kuna cha kujifunza. Kufahamu fikra za watoa matusi hayo.

Na hakika, kuna wanaofikiri wananifahamu. Wamenipa majina, wamenihusisha na huyu na yule. Kimsingi hawanijui. Wamekuwa ni wakandamizaji wa fikra huru na wanaamini kila anayeandika mawazo yasiyofanana na yao, basi, amenunuliwa. Huu ni udhaifu, ni unyonge wetu pia. Hatujiamini.

Nitaendelea kuandika fikra zangu huru, napenda sana kuandika mawazo yangu. Nimefanya hivyo tangu nikiwa Sekondari pale Tambaza, tena kwa kuazisha kijarida cha shule. Niliandika mwenyewe kwa mkono, nilikuwa na wasomaji wangu pia. Tuliokuwa nao Tambaza miaka ile ya 80 ni mashahidi wa hilo.

Najua kuwa wakati mwingine kuna wanaokerwa na niandikayo. Hao wapo siku zote. Hatuwezi kufanana kimitazamo. Na tumekuwa wepesi sana, kila tusomapo mawazo ya mtu, kutafuta droo ya kabati la kumpachika. Siku hizi kuna droo za CCM, CHADEMA, CUF, Uislamu, Ukristo, Uchaga, Usukumuma na kadhalika.Na ni bahati mbaya sana, kuwa wengi tumeisahau “Droo ya Tanzania”. Hii ni droo muhimu sana na ilipaswa iwe ya kwanza. Kwa kila tutendalo liwe kwa MASLAHI YA TANZANIA KWANZA. Maslahi ya Taifa. Na Hilo Ni Neno La Leo.
 
Back
Top Bottom