PostGE2025 Wanasiasa, raia, wanaharakati, wakosoaji wanalalamikia utekaji, tukimbilie kwa nani??

Conversations and stories after Tanzania's 2025 General Elections

Ghwema

Member
Joined
Dec 6, 2025
Posts
7
Reaction score
7
Ndani ya vipindi tofauti kwa Mwaka 2024 na 2025 tumeshuhudia ongezeko la matukio ya Watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha, kutekwa nchini Tanzania na bado kumekuwa kukiripotiwa kwa matukio kadhaa ya aina hiyo kuendelea.

Hali hii inanigusa kwa kuwa inavunja misingi ya haki, uhuru wa kujieleza na usalama, matukio hayo mara nyingi yamehusishwa na Siasa na ndio maana waathirika wakubwa ni Wanaharakati wa Kisiasa, Waandishi wa Habari, Wadau wa Habari, Wakosoaji wa Mtandaoni na raia wa kawaida wanaoonekana kuwa mstari wa mbele kukosoa.

RIPOTI YA LHRC
Ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) imebainisha kati ya Mwaka 2020 na 2024 kulikuwa na matukio 87 ya utekaji, kati ya hayo 31 yalitokea Mwaka 2022 na 33 yalitokea Mwaka 2024.

Ripoti imeonyesha kati ya Mwaka 2020 na 2024 Watanzania waliouawa kinyume cha Sheria na Vyombo vya Usalama kama vile Jeshi la Polisi na Askari wa Wanyamapori (Jeshi Usu) walifika 36.

Soma - Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Yasikitishwa na Matukio ya Utekaji na Kupotea kwa Watu Nchini

UCHAGUZI WA TANZANIA
Miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, familia nyingi zilianza kuripoti kupotea kwa wapendwa wao. Wapo waliopatikana, hofu ikatawala, wengine wakapatikana wakiwa wazima, wengine wakiwa majeruhi na wengine ilipatikana miili yao tu.

Ripoti kutoka kwa Mashirika ya Haki za Binadamu zimeonesha kuwa hali hiyo imechangia kuua ari ya Wananchi kushiriki katika michakato ya Demokrasia ikiwemo katika chaguzi.

Utekaji umechangia imani ya Watu kwa Vyombo vya Dola kushuka, mashuhuda na waathirika wa matukio hayo wameishia kuishi kwa hofu.

FAMILIA MWANZA YAISHI KWA HOFU
Kuna Familia moja ndani ya Mwanza ilimpoteza kijana wake Jerison aliyekuwa Mwanaharakati, alitoweka, ikasemekana ametewa alipokuwa maeneo ya Kishihiri Center karibu na Kasanda Hotel, Saa 10:30 Jioni.

Mashuhuda walieleza watekaji walitumia gari aina ya Cruiser nyeupe na kwamba licha ya kutoa taarifa Polisi hawajawahi kufanikiwa kumpata, hivyo wameishia kuwa familia yenye majonzi.

Mama wa kijana huyo anasema mwanaye (Jerison) alikuwa na ndoto nyingi kubwa ambazo zinaonekana kubaki kuwa ndoto tu.

Matukio ya utekaji yaliyotrend…
Ally Kibao:
Mwanachama na kiongozi wa CHADEMA, alitekwa kwa kushushwa kutoka ndani ya basi, Watekaji wajitambulisha kuwa ni Wanausalama, siku kadhaa baadaye mwili wake uliokotwa.

Pia soma:
-
Dar: Ali Mohamed Kibao, kiongozi wa CHADEMA auawa na mwili kutelekezwa Ununio ukiwa umeharibika sana
- Padri Kitima: Ali Kibao amekamatwa kwenye halaiki mchana, wanasema tunyamaze? Uovu lazima tuukemee!

Mdude Nyangali: Mwanaharakati na Mwanasiasa wa CHADEMA, alitekwa nyumbani kwake Mei 2, 2025.

Deusdedith Soka: Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA, alitoweka Agosti 18, 2024, Dar akiwa na wenzake wawili Jacob Mlay na Frank Mbise, hawajulikami walipo hadi sasa.

Humphrey Polepole: Oktoba 6, 2025, Mwanasiasa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania – Cuba ilidaiwa ametekwa na Watu wasiojulikana akiwa Dar, miezi michache tangu ajiuzulu nafasi yake ya Ubalozi nchini Cuba kisha kutumia mitandao ya Kijamii kukosoa mambo mbalimbali ikiwemo kukikosoa chama chake cha CCM na utaratibu uliotumika kumpata Mgombea Urais kupitia chama Mwaka 2025.

Polepole alikuwa akisisitiza kukosekana kwa Utawala Bora, misingi ya haki, maadili na kukiukwa kwa Katiba.

Matukio ya siku za nyuma
Ben Saanane: Mwanachama wa CHADEMA, alitoweka Mwaka 2016 na hajulikani alipo mpaka leo. Azory Gwanda: Mwandishi wa Habari alitoweka Mwaka 2017 na hajulikani.

MwanaCCM apotea Mwanza
Machi 2025: Kada wa CCM ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Daniel Chonchorio, Mkazi wa Jijini Mwanza alipotea katika mazingira ambayo yanadaiwa kuwa tata.
CHADEMA: WANACHAMA 52 WAMETEKWA
Oktoba 27, 2025, CHADEMA ilitangaza orodha ya majina ya Watu 52 wakiwemo viongozi wa chama hicho, wafuasi na wanachama wake, walioripotiwa kutekwa katika kipindi cha mwezi mmoja.

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia alieleza kati ya Oktoba 1 - 25, 2025, zaidi ya watu 52 wamechukuliwa na Jeshi la Polisi, huku wengine wakidaiwa kuchukuliwa na watu wasiofahamika maeneo mbalimbali nchini ndani ya siku 25 zilizopita.
Takwimu za Maria Sarungi
Oktoba 10, 2025: Mwanaharakati Maria Sarungi aliandika “Nimechukua kesi 191 za utekaji zilizotokea kati ya 2021 hadi 2025, 70% hawajapatikana, hizi ni kesi ambazo nimeletewa taarifa au kutumiwa / kuona mitandaoni. Muda umefika tuseme BASI!”.

Kijana wa chama apotea
Novemba 17, 2025 kulisambaa kwa taarifa za kupotea/kukamatwa kwa kijana Titho Philemon Dyakiye, Mzaliwa wa Wilaya ya Ngara.
Titho, mzaliwa wa Kijiji cha Nyamagoma, na mhitimu wa Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) - Mwanza alikuwa ni Mwanachama wa CHADEMA baadaye inadaiwa alijiunga na CCM, mpaka sasa haijulikani alipo na hakuna dalili za kumpata.

Polisi yakanusha kuhusika na utekaji
19 Juni 2025; Jeshi la Polisi Tanzania lilisisitiza kutohusika na matukio ya utekaji na mauaji yanayoripotiwa mara kwa mara. Hayo yalisemwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime.

Alisema "Katika matukio ambayo yameripotiwa katika Vituo vya Polisi na uchunguzi wa kina kufanyika na walioripotiwa kupotea kupatikana wakiwa hai au wengine wakiwa wamekufa, hadi sasa ushahidi kwa baadhi ya matukio umeonyesha sababu zake ni kujiteka."

Pia, Septemba 1, 2025, DCP David Misime alisema baadhi ya matukio hayo yanatokana na watu kujiteka wenyewe, wivu wa mapenzi, imani za kishirikina, migogoro ya kugombea mali, pamoja na nia ya kulipiza kisasi.

Pia soma:
-
Polisi: Baadhi ya matukio ya utekaji ni kujiteka wenyewe na migogoro ya kifamilia
- DCP Misime: Mchakato wa uchaguzi unaendelea vizuri, nchi inaendelea vizuri

Jumuiya ya Wanataaluma wa UDSM (UDASA) ilieleza katika taarifa yake kuwa Wananchi wakikosa imani na Wanausalama na Vyombo vyake vinaweza kutokea madhara makubwa katika Jamii, wakitolea mfano tukio la Afisa wa TRA kuuawa akidhaniwa ni Mtekaji.

Wito wangu…
Naomba mamlaka husika, Vyombo vya Usalama, Asasi za Kiraia na viongozi wetu wa Kisiasa kuhakikisha haki inalindwa.

Hatupaswi kuruhusu uoga kutawala nchi yetu, wala haki ya Mtu mmoja mmoja kuishi, kuzungumza na kushiriki siasa kufutwa kinguvu.

Mimi kama raia wa Tanzania nikiwakilisha Watanzania wengine, tunahitaji majibu na uwazi juu ya waliopotea, tunahitaji mfumo wa haki usio na upendeleo, tunahitaji uchaguzi huru na salama usioambatana na hofu ya utekaji au mateso.

Watanzania wengi hatuna nia ya kupinga mamlaka bali tunaomba haki, usawa na ulinzi kwa kila Mtanzania.

Demokrasia haiwezi kushamiri mahali ambapo uhuru wa mawazo unauawa kwa vitisho na mateso.

TUNASISITIZA WATANZANIA WANASTAHILI CHAGUZI HURU, SALAMA NA ZENYE KUHESHIMU HAKI ZA BINADAMU. SAUTI ZETU ZISIKIKE.
 
Sifa za dictator,anaanzisha jeshi lake nje ya utaratibu wa nchi
 
"Katiba hii imenipa Madaraka makubwa sana, siku atakuja mtu ataitumia atakavyo na kuwa kama Mungu". - Mwl. Nyerere 1982
 
Ni huzuni kuona matukio ya utekaji yanavyoongezeka hasa wakati wa uchaguzi. Serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti kulinda usalama wa raia na haki ya kujieleza.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…