Wanapingana na wenzao wa Arusha?KKKT Zanzibar yamtosa Lowassa

Lunyungu

JF-Expert Member
Aug 7, 2006
8,873
1,894
na Tamali Vullu, Zanzibar

KATIKA hali inayoweza kuonyesha kuporomoka kwa hadhi ya Waziri Mkuu aliyelazimika kujiuzulu kutokana na kashfa, Edward Lowassa, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Jimbo la Mission Zanzibar, juzi lilimfuta kuwa mgeni rasmi katika harambee ya kanisa hilo.

Baada ya kufutwa, Lowassa kama mgeni rasmi, nafasi hiyo ilichukuliwa na Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Alex Malasusa, ambaye aliongoza shughuli hiyo.

Harambee hiyo, ilipangwa kufanyika siku kadhaa zilizopita huku mipango ikiwa ni kumfanya Lowassa kuwa mgeni rasmi lakini iliahirishwa baada ya kuibuka kwa kashfa ya Richmond iliyomlazimisha Lowassa kujiuzulu wadhfa wake huo.

Habari kutoka kwa watu wa karibu na uongozi wa kanisa hilo, zinasema mabadiliko yanahusishwa na kujiuzulu kwake wadhifa aliokuwa nao kutokana na kuhusishwa na Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond. Lowassa alijiuzulu wadhifa wa uwaziri mkuu Februari 7, mwaka huu.

Habari zinaeleza kuwa harambee hiyo ilikuwa ifanyike Februari 24 mwaka huu, lakini kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi iliahirishwa hadi ilipofanyika juzi.

Hata hivyo, licha ya Lowassa kutohudhuria, ilitangazwa katika harambee hiyo kuwa alichangia sh 3,000,000.
Akizungumza katika harambee hiyo iliyofanyika katika kanisa hilo lililoko Mwanakwerekwe, Zanzibar, Askofu Malasusa alielekeza hotuba yake katika suala la ufisadi, na kueleza kushangazwa kwake na viongozi kuhujumu uchumi wa nchi bila kuwaonea huruma wananchi wengi maskini.

Alisema wananchi wengi nchini wanaishi maisha ya dhiki, kwa wengi wao kushindwa kutumia maji ya bomba tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanzania wala barabara zao hazijawekwa lami.

“Ni lazima tuwe na huruma. Wananchi wengi hawajui maji ya bomba tangu tupate uhuru nchini na barabara nyingi hazina lami,” alisema.

Hata Mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi, ambaye alishiriki harambee hiyo, naye alizungumzia kuhusu viongozi wanaowadhulumu wananchi na kutaja mifano kadhaa kutoka katika Biblia katika kuelezea hoja yake.

Akinukuu vifungu vya Biblia, Mengi alisema kuwa wakati Yesu alipomtembelea Zakayo nyumbani kwake, alieleza kuwa mtu aliyedhulumu kitu anapaswa kurudisha mara nne, ili aweze kusamehewa.
“Ingawa Biblia inatamka mtu aliyedhulumu kitu kurudisha mara nne, lakini kama (viongozi wetu waliowadhulumu wananchi) watashindwa, warudishe hata mara moja. Tuhamasishane turudishe, ili tuweze kujenga shule na kufanya vitu vingine vya maendeleo, kisha ndipo tuwasamehe,” alisema Mengi.

Pia alisema ingawa katika sala siku zote watu wanasema mali wanazotafuta ni kwa ajili ya Bwana, lakini maneno hayo hawayatekelezi kwa vitendo.

“Siku zote tunaposali tunasema mali tunazotafuta ni za Bwana, lakini maneno haya hatuyatekelezi kwa vitendo… toa kitu kwa Bwana, ili unapokufa uendelee kuishi katika mioyo ya watu.

“Apandae haba atavuna haba, apandae kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzumi wala kwa lazima. Mmeona Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu,” alisema Mengi akinukuu maneno kutoka katika Biblia.

Awali, akisoma risala, Mzee wa kanisa hilo, Jumbe Katala, alisema harambee hiyo ni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya ibada kwa Mtaa wa Dunga na Usharika wa Kivunge, zote za mjini Unguja.

Alisema mbali na ukosefu wa nyumba za ibada, changamoto nyingine zinazowakabili ni upungufu wa nyumba za watumishi na upungufu wa wachungaji.

Alisema lengo la harambee hiyo ni kukusanya sh milioni 50, lakini lengo hilo lilivukwa katika harambee hiyo baada ya kukusanywa sh milioni 65.

Katala alisema ujenzi wa nyumba hizo za ibada utakwenda sambamba na ujenzi wa kituo cha afya na shule ya awali.

Akizungumzia kuhusu maeneo ya kujenga nyumba za ibada visiwani humo, Askofu Malasusa, alisema wakati akijibu risala hiyo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imeahidi kuwapatia ushirikiano na imeshawapatia eneo kisiwani Pemba.

“Ninachowaomba muishi bila upendeleo na ubaguzi, Serikali ya Zanzibar inapenda watu wa dini zote….Rais Abeid Karume alinikaribisha na kunieleza kuwa wana historia ya kuishi na watu wa dini mbalimbali,” alisema Askofu Malasusa.

Aidha, aliwasihi Wakristo wenzake kutumia fedha zilizopatikana kwa lengo lililokusudiwa na kusema iwapo zitatumika vinginevyo, itashusha morali ya watu waliojitolea kuchangia.

“Kamati ya harambee izingatie hilo, tushirikiane ili kanisa liendelee kuwa kioo cha jamii,” alisema.



Source: TanzaniaDaima
 
Back
Top Bottom