Wanaofikiria uchaguzi mwingine Zanzibar wanapoteza muda

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
“SISI wapinzani tunafanya kazi vizuri na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Dk Ali Mohamed Shein. Tupo kwa ajili ya kuleta maendeleo ya wananchi wa Zanzibar bila ya kujali itikadi za vyama vya siasa.”

Hiyo ni kauli ya Said Soud Said ambaye ni Waziri asiye na Wizara Maalumu na Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha AFP Wakulima alipofanya mazungumzo na gazeti hili. Yeye ni miongoni mwa mawaziri watatu kutoka vyama vya upinzani waliochaguliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kutoka upinzani baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa marudio Machi 20 mwaka huu.

Kabla ya hapo, Dk Shein aliwateua viongozi hao kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia nafasi za uteuzi wa rais. Mbali na Soud wengine ni Hamad Rashid Mohamed wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) pamoja na Juma Ali Khatib kutoka chama cha Ada-Tadea. Soud anasema anamshukuru Rais wa Zanzibar kwa uamuzi wake huo wa hekima na busara ambao ameufanya akiwa na matarajio makubwa kwamba viongozi wa vyama vya upinzani wana uwezo wa kumsaidia katika kuongoza Zanzibar.

Anasema dhamira ya kweli ya Rais Shein ya kuleta maendeleo na kupambana na umasikini kwa kujenga mazingira ambayo yatawakomboa wananchi wake inaonekana kwa kuwahusisha wapinzani kwenye serikali yake ili wamsaidie kuchapa kazi. Anasema huu ni mwezi wa sita tangu kuwepo katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na amekuwa akifanya kazi zake na kutekeleza majukumu aliyopewa kwa nguvu zote na uwezo kwa kushirikiana na mawaziri wenzake.

Anasema kuwepo kwao ikiwemo michango katika Baraza la Wawakilishi kumeondosha dhana ya wananchi wengi kwamba upinzani wenye uwezo ni chama cha wananchi CUF tu. “Kazi yangu kubwa ni kumsaidia rais na kumshauri katika masuala mbalimbali ikiwemo yanayotokea Pemba kwa sababu mimi nipo Pemba na kule tumefanya kazi kubwa katika kipindi kifupi. Kule sasa watu wametambua kwamba upinzani wenye ufanisi kwao sio tena wa CUF pekee,” anasema.

Ukimuuliza swali hili, kwa nini uliamua kushiriki katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 huku baadhi ya vyama vya siasa vikiugomea kwa madai kwamba ulikuwa si halali na hakuna sababu za kufanyika uchaguzi mwengine, Soud anajibu: “Uchaguzi wa kwanza Oktoba 25 uliharibiwa makusudi na CUF wakiwa na lengo na pupa ya kushika madarakani, matokeo yake mbinu na ujanja wao ziligundulika na taasisi zinazosimamia uchaguzi.

“Kwa hivyo uliitishwa uchaguzi wa marudio ambapo chama changu cha AFP hakikuwa na sababu za kususia uchaguzi ule kwa sababu umeitishwa na taasisi zinazotambuliwa kwa mujibu wa sheria. Na yeyote aliyeamini kwamba uchaguzi uliopita angelishinda, kimantiki hakuwa na sababu ya kuogopa kushiriki tena uchaguzi wa marudio,” anasema.

Anafahamisha kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar uchaguzi mkuu unasimamiwa na kuendeshwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), hivyo kitendo cha kufuta matokeo na kuitishwa kwa uchaguzi mwengine kilikuwa sahihi kutokana na sababu wanazozijua wao (ZEC). “Chama changu hakikuwa na sababu ya kususia uchaguzi wa marudio kwa sababu umeitishwa na chombo halali chenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi mkuu nchini. Sikuwa na sababu ya msingi ya kugomea uchaguzi ule na hata waliogoma bado sababu wanazotupa hazina mashiko,” anasema.

Ni kwa mantiki hiyo Soud anasema uchaguzi umekwisha na hivyo anawataka wananchi wa Zanzibar kufanya kazi na kusubiri neema zilizotangazwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinazotokana na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Anawataka wananchi wa Zanzibar kamwe wasikubali kuyumbishwa na kubabaishwa na watu wachache wenye tamaa ambao bado wanaamini kwamba uchaguzi mwingine utafanyika kwa sababu wa marudio ni batili.

“Mimi nawasihi wananchi ikiwemo wa Pemba wafahamu kwamba uchaguzi umekwisha na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo madarakani chini ya Rais Shein. Hakuna uchaguzi mwingine hadi mwaka 2020,” anasema. Kuhusu uongozi wa Dk Shein katika kipindi cha miezi sita, Soud anasema Rais Shein amefanya kazi kubwa ya kutekeleza kwa vitendo ilani ya chama chake (CCM) pamoja na ahadi zake ikiwemo kulipa pensheni ya jamii kwa wazee waliofikia umri wa miaka 70.

Anasema ni nchi chache katika Bara la Afrika zilizoweza kulipa pensheni kwa wazee wastaafu waliofikia umri wa miaka 70, kitendo ambacho kinastahili kupongezwa kwa nguvu zote kwani muungwana akiahidi basi hutekeleza. Anasema ahadi hiyo tayari imeanza kutekelezwa kwa vitendo kupitia Wizara ya Fedha ambayo imefanya hivyo baada ya kufanikiwa kukusanya mapato na kuvuka malengo yake.

Soud ambaye ni mkazi wa Pemba katika jimbo la uchaguzi la Wawi anasema kwamba hali ya kisiwa cha Pemba kwa sasa ni shwari sana na wananchi wanataka maendeleo tu na siyo siasa. Anasema amepata nafasi ya kutembelea wananchi ikiwemo vikundi vya ushirika pamoja na Saccos za akinamama ambapo wapo tayari kujikusanya na kujiunga kwa ajili ya kupata mikopo na kuendeleza maisha yao.

Anasema ni ukweli kwamba wabunge na wawakilishi waliopita kutoka katika chama cha wananchi CUF waliwadanganya wananchi kwa kutumia kura zao kwa ajili ya kujinufaisha pamoja na kutumia vibaya fedha za Mfuko wa Jimbo la Uchaguzi. Anasema matumizi mabaya ya kura za wananchi wa majimbo ya Pemba kwa wawakilishi na wabunge wa CUF yamewafanya wananchi kuwa nyuma hata akinamama wameshindwa kuwasaidia katika vikundi vya ushirika pamoja na vyama vya kuweka na kukopa (Saccos).

“Wananchi wengi Pemba wameniambia sasa wapo tayari kujiunga katika vikundi vya ushirika na kuanzisha Saccos kwa ajili ya kupunguza ukali wa maisha na umasikini,” anasema. Soud anasema wananchi wa Pemba wamechoka kudanganywa na wanasiasa wenye uchu wa madaraka na kwamba sasa wapo tayari kupokea maendeleo yenye kuleta mabadiliko chanya katika maisha yao,” anasema.

Kuhusu madai kwamba huko Pemba kulikuwa na migomo na hali ya wananchi kutoshirikiana Soud anakiri kwamba awali ilikuwepo hali hiyo lakini sasa imetoweka kwa sehemu kubwa. Anasema yeye binafsi alifanya harusi ya mtoto wake na kupika chakula ambacho kililiwa na wananchi wote wa eneo la jimbo la Wawi. “Sasa wananchi wamegutuka na wanataka maendeleo na sio kauli za vitisho vya migomo na kutiana hasara wananchi wenyewe kwa wenyewe,” anasema Soud.

Kuhusu swali la nini kifanyike katika kupambana na tatizo la umasikini na kuzuia kundi la vijana kukimbia Pemba na kwenda Unguja au Tanzania Bara, Soud anasema huu ni wakati mwafaka kwa SMZ kuimarisha zaidi maeneo huru ya kiuchumi Pemba.

Anasema kisiwa cha Pemba sasa kimeimarika katika eneo la miundombinu yake pamoja na barabara na nishati ya umeme. Hivyo anasema kazi kubwa inayopaswa kufanywa na Serikali ni kushajiisha wawekezaji kuwekeza Pemba kwa ujenzi wa viwanda ambavyo vitazalisha ajira. “Tatizo la vijana wa Pemba kukimbia kisiwa hicho ni ukosefu wa ajira tu. Huu ni wakati mwafaka kwa serikali kushajiisha wawekezaji kuwekeza maeneo huru ya uchumi Micheweni Pemba kwa ajili ya kuzalisha ajira kwa vijana,” anasema Soud.
 
Uchaguzi wa marudio wa Zanzibar ulikuwa huru na wa haki. Japo ulisababishwa na mchakato haramu au batili, alichofanya Jecha ni mbakaji wa Demokrasia mchana kweupe huku akishangiliwa, ila anayebakwa asipopinga ubakwaji huo atahesabiwa ameridhia, hivyo CUF waliridhia ubakwaji wa Jecha, kulikopelekea Uchaguzi wa marudio wa Zanzibar, batil isipobatilishwa, hugeuka halali, vivyo hivyo, haramu isipoharimishwa hugeuka halali, ndicho kilichotokea Zanzibar, no one aliharimisha haramu ile au kuibatilisha batil ile, hivyo Uchaguzi ule wa marudio wa Zanzibar ni halali na ulikuwa huru na wa haki.

Pasco
 
Uchaguzi wa marudio wa Zanzibar ulikuwa huru na wa haki. Japo ulisababishwa na mchakato haramu au batili, alichofanya Jecha ni mbakaji wa Demokrasia mchana kweupe huku akishangiliwa, ila anayebakwa asipopinga ubakwaji huo atahesabiwa ameridhia, hivyo CUF waliridhia ubakwaji wa Jecha, kulikopelekea Uchaguzi wa marudio wa Zanzibar, batil isipobatilishwa, hugeuka halali, vivyo hivyo, haramu isipoharimishwa hugeuka halali, ndicho kilichotokea Zanzibar, no one aliharimisha haramu ile au kuibatilisha batil ile, hivyo Uchaguzi ule wa marudio wa Zanzibar ni halali na ulikuwa huru na wa haki.

Pasco
Dhambi haiwezi kutokuwa dhambi kwa kuwa haikupingwa
 
Back
Top Bottom