Wananchi Watahadharishwa Athari za Mafuriko

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,903
945

WANANCHI WATAHADHARISHWA ATHARI ZA MAFURIKO

Serikali imewatahadharisha wananchi kuacha kujenga na kufanya shughuli za kijamii kwenye maeneo ya bondeni ili kuepukana na athari za mafuriko zinazoweza kutokea na kuwasababishia madhara.

Tahadhari hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akijibu maswali bungeni jijini Dodoma, Septemba 05, 2023.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Stella Ikupa aliyetaka kujua Serikali imejipangaje kukabiliana na athari za mvua za El - Nino zinazotarajiwa kunyesha kuanzia Oktoba mwaka huu, Mhe. Khamis alisema elimu itaendelea kutolewa kwa wananchi ili waache kufanya maeneo ya mabondeni kuwa makazi.

“Ni kweli panapokuwa na mvua kubwa kama hizi mara nyingi hutokea madhara ambayo yanaharibu makazi na kugharimu maisha ya watu, hivyo Serikali katika kipindi hiki tunawapa elimu wasijenge kwenye maeneo ambayo yanakaa maji na kama wana mpango huo basi waondoke ili mvua zitakaponyesha wasipate madhara,” alisisitiza.

Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Nungwi Mhe. Simai Hassan Sadiki aliyetaka kujua mkakati wa dharura wa kunusuru athari za mabadiliko ya tabianchi eneo la Nungwi, Zanzibar, Naibu Waziri Khamis aliwahimiza wananchi kuendelea kupanda mikoko katika fukwe za bahari ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alifafanua kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha wananchi visiwani humo kufanya shughuli endelevu zisiharibu mazingira zikiwemo ulimaji na uvunaji wa mwani usioharibu fukwe.

Alisema kwa kutambua changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi, tayari Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeanza kuchukua hatua za kukabiliana nazo.

“Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 SMZ imetenga kiasi cha shilingi milioni mia sita na hamsini kwa ajili ya kufanya tathmini ya awali ya kuzuia changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Aidha, Naibu Waziri Khamis amesisitiza kuwa Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na SMZ zitashirikiana katika kutafuta fedha zaidi ili kudhibiti uharibifu unaotokea eneo la Nungwi.
 

Attachments

  • IMG-20230905-WA0069-860x574.jpg
    IMG-20230905-WA0069-860x574.jpg
    32.2 KB · Views: 3
  • maxresdefaultMKPOIU.jpg
    maxresdefaultMKPOIU.jpg
    60.7 KB · Views: 3
Back
Top Bottom